HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 25, 2024

PROFESA MALEBO:UHAMAJI WA HIARI KUTOKA NGORONGORO NI KWA LENGO LA KULINDA HAKI ZA BINADAMU NA UHIFADHI

 

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Tanzania imesema kuwa inatekeleza uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka Ngorongoro ili kulinda haki za binadamu na uhifadhi.

Hayo ameyasema Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania kuwa Prof. Hamis Malebo wakati akiwasilisha ujumbe Mkutano wa 23 wa Jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) nchini Marekani ulichoanza Aprili 15 Aprili, 2024 na kuhitimishwa Aprili 26

Profesa Malebo, ameueleza mkutano huo kuwa, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya mapitio shirikishi ya hali ya maisha ya wananchi na uhifadhi katika Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCA) na kubaini umuhimu wa kuweka uwiano sawa wa uhifadhi wa maliasili na utamaduni, maendeleo ya jamii na maendeleo ya utalii.

Amesema kwa kutambua haki za binadamu, ambazo zimekuwa sauti ya wanaharakati na wahifadhi mbalimbali na kwa kuzingatia masharti ya Katiba yaTanzania na matakwa ya ulinzi na uhifadhi wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa 1972 na sheria za nchi, ni wazi kwamba, wananchi wanaoishi katika Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro wameathiriwa na migogoro ya binadamu na wanyamapori, magonjwa ya wanyamapori, kukosa haki ya kuwa na makazi ya kudumu, kudorora kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kukosa maji safi na salama, na umiliki wa ardhi.

Profesa Malebo amesema kwa mfano kuwa katika kipindi cha 2018 hadi 2023 watu 65 waliuawa na 205 walijeruhiwa na wanyama pori kama vile Simba, Chui, Fisi, Kiboko, Nyati na pamoja na Tembo.

Amesema Wananchi walio katika Hifadhi ya eneo la Ngorongoro wanaachwa nyuma katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Prof. Malebo ameeleza kuwa, kwa kufuata misingi ya haki za binadamu, Serikali imefanya mashauriano na jamii ya wakazi wa Ngorongoro katika kipindi cha miaka 32 ili kwa pamoja kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto za kijamii na kiuchumi zinazowakabili wananchi wake wanaoishi katika ardhi ya hifadhi.

Hata hivyo amesema Mikutano ya uhamasishaji imefanyika kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya tawala za Wilaya na Mikoa juu Wakazi wanaoishi katika walioko katika Mamlaka ya Ngorongoro mbalo ni eneo lililohifadhiwa walipewa elimu kuhusu sheria zinazosimamia utendakazi wa NCA ambazo haziruhusu wala kutoa kibali chochote cha kisheria kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi wala kutoa haki ya umiliki wa ardhi katika eneo hilo la hifadhi ambalo pia ni eneo la Urithi wa Dunia.

Aidha wakazi hao walifahamishwa kuhusu manufaa yanayohusiana na kuhama kwao kwa hiari Kwenda katika maeneo yaliyo nje ya hifadhi nchini Tanzania.

Akifafanua juu ya mkakati wa kuhama kwa hiari.
Prof. Malebo alibainisha kuwa, kwa kuongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mikataba ya Umoja wa Mataifa, Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu, maazimio ya vyombo vingine muhimu vya haki za binadamu na Azimio la Vienna, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka hifadhi ya eneo la Ngorongoro.

Serikali pia inawezesha zoezi hilo na inabeba gharama za uhamaji, fidia na inatoa mkono wa shukrani kwa wananchi wanaohama kwa hiari Kwenda nje ya eneo la hifadhi.

Profesa Malebo amesema Serikali inahakikisha wanajamii wanaoishi katika ardhi iliyohifadhiwa wanasaidiwa kuhama na kwenda kuishi katika maeneo ambayo wataendelea na kutekeleza tamaduni zao kwa uhuru tofauti na ambako kwa sasa wanaishi kwa kukabiliwa na changamoto zinazotishia maisha, utamaduni na kuchochea umaskini.

Prof. Malebo pia aliueleza mkutano huo kuwa, Serikali ya Tanzania imepanga kwa umakini uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka katika Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni hatarishi kutokana na ugumu wa maisha na migogoro na wanyamapori jambo ambalo linatoa fursa kubwa za kupunguza maafa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wakazi na eneo hilo la Urithi wa Dunia.

Amesema Serikali iliainisha maeneo nje ya hifadhi ambapo wakazi wa Ngorongoro wataweza kuhamia kwa hiari na kuendelea na shughuli zao za kujitafutia riziki kwa amani kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na kumiliki ardhi na kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi.

Wajumbe wengine wa Tanzania wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja na Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bi. Hindu Zarooq Juma, Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Pellage Kauzeni, Afisa Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Agnes Gidna, Kaimu Meneja wa Urithi wa Dunia katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Bw. Edward Kutandikila, Mwanasheria wa Serikali na Bw. Erick J. Kajiru, Afisa Mwandamizi Mkuu katika Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad