HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, March 3, 2024

HALMASHAURI YA WILAYA TUNDURU KUTUMIA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 1.085 KUJENGA SOKO JIPYA LA MADINI

 

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Wakili Julius Mtatiro aliyevaa kofia ya pama,akitoa maelekezo kwa mhandisi wa ujenzi wa wilaya hiyo Ramadhan Magaila baada ya kukagua ujenzi wa soko jipya na la kisasa la kuuzia madini litakalogharimu Sh.bilioni 1.085 hadi kukamilika.

Na Mwandishi wetu, Tunduru
HALMASHAURI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imeanza ujenzi wa mradi wa soko kubwa na la kisasa la madini ya vito ili kudhibiti uuzaji holela wa madini unoafanywa na watu wasiokuwa waaminifu.

Soko hilo litasaidia Halmashauri na serikali kwa ujumla, kuongeza mapato kupitia tozo na kodi mbalimbali kwa sababu watu wote watatakiwa kuuza na kununua madini sehemu moja.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Marando wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa soko hilo litakalogharimu Sh.bilioni 1.085 kwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro.

Marando alisema,soko hilo la kisasa litakuwa na jumla ya vibanda 153 na litazuia utoroshaji wa madini kwani hakutakuwa na sababu ya wachimbaji kwenda mbali ili kuuza madini na litarahisisha sana mamlaka husika kufuatilia kwa ukaribu utoroshwaji wa madini.

Alisema,biashara ya madini katika wilaya hiyo imeongeza na kuna maombi zaidi ya 130 kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wanaotaka kuja kununua madini katika wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa Marando,katika wilaya ya Tunduru kuna masoko mawili tu ya kuuzia madini ambayo ni Tudeco na Generation yenye vibanda 54 ambavyo kwa sasa havitoshelezi.

Alisema,kutokana na kuongezeka kwa biashara hiyo serikali kupitia Halmashauri ya wilaya imeona ni vyema kujenga soko kubwa litakalokidhi mahitaji ya watu wengi na kuwa chanzo kikubwa cha mapato.

Aidha alisema,kulingana na sheria ya madini inatakiwa kuwa na soko moja tu la kuuza na kununua madini, kwa sababu kuwa na masoko mawili kunasababisha utoroshaji mkubwa wa madini,hivyo serikali kukosa mapato.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro alisema,kujengwa kwa soko hilo ni hatua kubwa na muhimu kwa wilaya ya Tunduru na amempongeza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri Chiza Marando kwa kuibua vyanzo vipya vya mapato.

Alisema,soko hilo ni muhimu kwa uchumi wa wilaya na nchi kwani litawezesha kudhibiti utoroshaji wa madini na kuzuia tabia inayofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kununua madini majumbani na wengine kuanzisha masoko haramu kwenye maeneo ya machimbo.

Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo,amemuagiza mkurugenzi wa Halmashauri pindi ujenzi wa soko hilo utakapokamilika kufunga masoko yaliyopo na wanunuzi wote watatakiwa kuhamia kwenye soko jipya.

Mtatiro, amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri kukamilisha ujenzi wa soko hilo haraka ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wadau wengine wa madini kuondoka kwenye masoko ya zamani.

Mfanyabiashara wa madini Abdulkadil Ali,ameipongeza serikali kujenga soko la kisasa kwa kuwa litatoa nafasi kwa watu wengi kufanya shughuli zao kwa uwazi na kuchangia uchumi wa nchi yetu.

Alisema,soko hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuingiza zaidi ya Sh.milioni 300 kwa mwaka kama ushuru na kupitia kodi za madini serikali itapata zaidi ya dola 30,000.

Abdukadil ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Len’s Group of Companies Ltd alisema,fedha hizo zitachochea maendeleo na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad