HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 21, 2024

SHULE MPYA TISA ZA SEQUIP ZINAVYOVUTIA WANAFUNZI RUVUMA

 

Na Albano Midelo,Songea 

SHULE mpya tisa za sekondari  zilizojengwa mkoani Ruvuma kupitia Program ya Uboreshaji Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni tano  zimekamilika na kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.

Serikali kupitia SEQUIP awamu ya pili katika mwaka 2022/2023 imetoa zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari mpya za kata 176 kati ya hizo sekondari tisa zimejengwa mkoani Ruvuma,

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo ili kujenga shule mpya za sekondari za kata katika kata zisizo na shule na kata zenye wanafunzi wengi zaidi ukilinganisha na miundombinu ya shule zilizopo.

Wanafunzi  walioanza masomo katika sekondari hizo mkoani Ruvuma wameipongeza serikali kwa kuwajengea sekondari hizo ambazo zimemaliza changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kufuata sekondari.

Juma Issa na Khadija Kassim  ni wanafunzi wa sekondari mpya Kata ya Tinginya wilayani Tunduru ambayo wamesema kabla ya ujenzi wa sekondari hii,wanafunzi waliofaulu katika Kata hiyo walikuwa wanakwenda kusoma katika sekondari ya Nakapanya ambayo ipo umbali wa kilometa 40.

“Kutokana na umbali huo wanafunzi wengi waliacha shule,utoro ulikuwa mwingi na Watoto wa kike walipata mimba baada ya kukumbwa na vishawishi vingi’’,alisema Khadija Kassim.

Mariam Ismail ni Mwananchi kutoka Kijiji cha Tinginya amesema kabla ya sekondari hiyo wazazi walipata gharama kubwa kwa Watoto wao ikiwemo nauli ya kusafiri Kwenda sekondari ya Nakapanya ambapo baadhi ya wazazi walishindwa kumudu ambapo hivi sasa wanamshukuru Rais kwa kuwajengea sekondari hiyo.

Mkuu wa sekondari ya Tinginya Romatus Ndoa amesema walipokea kiasi cha shilingi milioni 560 ambazo zimetumika kujenga jengo la utawala,madarasa manane,vyumba vitatu vya maabara,jengo la TEHAMA,kichomea taka,minara miwili ya maji na vyoo matundu 12,

Amesema wanafunzi wameanza masomo tangu Januari mwaka huu ambapo sekondari hiyo ya kisasa na mazingira ya kuvutia imeondoa kabisa changamoto ya wanafunzi wa Kata ya Tinginya kusafiri umbali mrefu.

Teresia Ng’ombo ni Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Tuwemacho wilayani Tunduru ambaye amesema wamepokea wanafunzi  70 kati ya 87 waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika sekondari hiyo.

Zamda Yusufu na Siyawezi Libadi ni wanafunzi wa kidato cha kwanza katika sekondari ya Tuwemacho   wamesema ujenzi wa sekondari hiyo umemaliza tatizo la wanafunzi kusafiri kilometa 45 hadi sekondari ya Namasakata kufuata shule.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Mputa wilayani Namtumbo  Filbert Mbunda  amesema sekondari hiyo imepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wapatao 157 kati yao waliomaliza darasa la saba mwaka 2023 ni 135 na waliomaliza darasa la saba mwaka 2022 ni 22.

Amesema kabla ya kuanza sekondari hiyo wanafunzi wote waliokuwa wanafaulu darasa la saba walipelekwa sekondari ya Mbunga iliyopo Kata ya Kitanda ambapo walikuwa wanatembea umbali wa kilometa 30 kila siku hali iliyosababisha wanafunzi wengi kuacha shule.

Naye Mkuu wa shule ya sekondari ya Lilondo Subira Mapunda amesema  baada ya shule hiyo kukamilika wamepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao walikuwa wanasafiri umbali wa kilometa 20 hadi sekondari ya Wino ambapo hivi sasa wanafunzi wanafurahia mazingira mazuri ya kujifunzia.

Ado Kawonga ni Kaimu Mkuu wa sekondari ya Mtopesi iliyojengwa katika Kijiji cha Lugagara Halmashauri ya Wilaya ya Songea amesema mara baada ya kukamilisha ujenzi wamepokea wanafunzi 71 wa kidato cha kwanza hivyo kumaliza changamoto ya wanafunzi kutembea kilometa 30 kila siku kufuata sekondari ya Kilagano.

Petro Liweli ni Mkuu wa shule ya sekondari ya Dkt.Lawrence Gama iliyopo Kata ya Mkuzo Manispaa ya Songea  amesema wamepokea jumla ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 200 ambao wameanza masomo mwaka huu .

Katika Programu ya SEQUIP Awamu ya kwanza Mkoa wa Ruvuma  ulitengewa zaidi ya shilingi bilioni 7.7 kujenga sekondari mpya za kata 11 ikiwemo sekondari moja ya Mkoa kwa ajili ya Watoto wa kike ambayo imejengwa wilayani Namtumbo na imeanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha Tano mwaka 2023. na wanafunzi w kidato cha kwanza 2024.Baadhi ya majengo katika sekondari mpya ya Dkt Lawrence Gama iliyojengwa kupitia program ya SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 560.6Baadhi ya wanafunzi wa sekondari ya wasichana ya Dkt Samia Suluhu Hassan iliyopo wilayani Namtumbo.Sekondari hii imejengwa kupitia program ya SEQUIP kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni nne.

Baadhi ya wanafunzi katika sekondari ya Tuwemacho Wilaya ya Tunduru ambayo imejengwa kupitia program ya SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 560.5 


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad