HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 21, 2024

MTOTO MIAKA SITA AUWAWA BABATI

 


MTOTO mwenye miaka 6 mwanafunzi wa darasa la awali shule ya msingi Mapea kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara ameuawa kwa kuchinjwa na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili kisha kutupwa mtoni kijiji cha Mapea kwenye mashamba ya wawekezaji.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji cha Mapea Filemon Mbogo, tukio hilo la kusikitisha na la kutisha limetokea februari 20,2024 ambapo mtoto huyo Maria Chacha akiwa na wenzake wakiwa wanatoka shule walikutana na mtu ambaye  aliwataka waongozane naye kwenda kuchuma matunda aina ya mazambarau na walipofika mbele wenzake waliona ni mbali wakaamua kugeuka lakini mtu huyo alimbeba Maria na kuondoka naye.

Amesema wazazi wa mtoto huyo walibaini tuko hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wenzake waliokuwa wameongozana pamoja wakitoka shule ndipo wakatoa taarifa katika uongozi wa kijiji na wananchi kuanza kumtafuta saa saba mchana na kuukuta mwili wa mtoto huyo katika shamba la mwekezaji Odedra eneo lenye mto na vichaka vikubwa pamoja na miti aina ya mikuyu.

Mbogo amesema mtoto huyo alichinjwa shingoni kisha kiwiliwili kikatupwa kwenye mto na kuwekewa gogo juu huku kichwa kikiwa pembeni.
Ameongeza kuwa tukio hilo sio la kwanza kutokea kwani katika maeneo hayo ilishapatikana miili miwili na mpaka sasa mtoto mwingine haijulikani alipo kwa zaidi ya miezi mitatu.

Kamanda wa Polisi mkoani Manyara George Katabazi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akiwataka wananchi waendelee kuwaripoti wahalifu na kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi katika maeneo yao.

Wananchi wanasema wamechoka na wameiomba serikali kuzungumza na mwekezaji ili kuweka ulinzi katika mashamba hayo ambayo yamejaa vichaka vikubwa na kuvutia wahalifu kufika katika maeneo hayo.
Mpaka sasa hakuna taarifa za mtu kushikiliwa na jeshi la Polisi kutokana na mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad