HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 5, 2024

KUKAMATWA KWA JAHAZI LENYE SHEHENA YA MADUMU YA MAFUTA YA KUPIKIA 1000

 


Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji kinaendelea na operesheni mbalimbali katika kudhibiti uhalifu ukanda wa Bahari ya hindi, katika hatua hiyo Januari 4, 2024 majira ya jioni maeneo ya Fungu Yasini,Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi, Kikosi kazi cha Polisi Wanamaji Dar es Salaam wakitumia boti ya Polisi walikamata jahazi likiwa limebeba shehena ya mafuta ya kupikia yakiwa kwenye madumu ya lita 20, likitokea Zanzibar kuelekea Bandari bubu Kunduchi.

Jahazi hilo liitwalo MV. HUDA lenye namba za usajili Z. 2957 likiongozwa na nahodha MOHAMED s/o FUMU (36) mkazi wa Bagamoyo akiwa na wenzake wa nne (4), likiwa na madumu ya mafuta ya kupikia yapatayo 1000 ya lita 20 aina ya Gold Spoon.

Aidha upelelezi wa awali umeonesha kuwa mzigo huo ulitakiwa kushuka katika bandari ya Mbweni ambapo taratibu za kulipa ushuru wa forodha zingekamilika na badala yake mtuhumiwa huyo alielekea katika bandari bubu ya Kunduchi ili kushusha mzigo huo.

Jeshi la Polisi kikosi cha wanamaji linaendelea kushirikiana na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na Idara nyingine za serikali ili kuhakiki mzigo huo na baadae taratibu nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa wafanyabiashara wasio na uadilifu, kufuata taratibu za mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) la sivyo watakamatwa, na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi. Pia Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji linaendelea kuwapongeza wananchi kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu na taarifa zao zinafanyiwa kazi haraka ikiwa ni pamoja na wahalifu kukamatwa.

Imetolewa na;

Moshi N. Sokoro - ACP

Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji (T)

Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad