HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 29, 2023

SERIKALI IMEDHAMIRIA KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO-MAJALIWA

 




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo katika kuendeleza sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya kilimo kwenye mazao ya chakula na biashara.

Amesema lengo ni kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula na kila Mtanzania anayejishughulisha na kilimo aweze kunufaika kwa kufanya biashara na kukuza uchumi na mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Desemba 29, 2023) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Litama, Chinongwe, Likwachu, Luchelegwa na Nandanga akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa, Lindi.

Amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha Tanzania inakuwa kimbilio la wengine wanaohitaji chakula. “Tumuunge mkono Rais wetu kwenye mapambano yake ya kukuza sekta ya kilimo na amefanya makubwa kwenye sekta hii ikiwemo kuagiza kutengwa maeneo maalumu ya kilimo kwa ajili ya vijana”

Waziri Mkuu amesema licha ya Serikali kuwa na mikakati ya kuimarisha sekta ya kilimo, pia imeendelea kuboresha sekta nyingine za afya, elimu, maji, umeme, miundombinu na biashara ili kuhakikisha wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wanapata maendeleo.

‘’Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo kwa kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo yote nchini yakiwemo na ya wilaya ya Ruangwa.’’

Akiwa katika kijiji cha Chinongwe Waziri Mkuu alitembelea zahanati ya kijiji hicho ambayo miundombinu yake imefanyiwa maboresho na kumuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa ahakikishe anamuongeza daktari mmoja ili kuboresha huduma.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Afisa Elimu wa wilaya ya Ruangwa aakikishe anawahamisha walimu kutoka kwenye shule zenye walimu wengi na kuwapeleka katika shule zenye upungufu ikiwemo na shule ya msingi Litama yenye walimu wanne huku mahitaji ni walimu wanane.

Akizungumzia uboreshaji wa miundombinu, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongezea bajeti TARURA nchini ambapo kwa wilaya ya Ruangwa imeongezeka kutoka shilingi bilioni moja hadi shilingi bilioni 4.8, kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya barabara za ndani na madaraja, hivyo amewaomba wananchi waendelee kumuunga mkono.




IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

IJUMAA, DESEMBA 29, 2023.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad