-CPA Mkama asema hatifungani hiyo imevunja rekodi, yawezesha kupatikana fedha kutekeleza miradi endelevu
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema Agosti 31, 2023 iliidhinisha maombi ya benki ya NMB kuuza toleo la kwanza la hatifungani iitwayo Jamii Bond yenye thamani ya Sh.bilioni 75
Hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya Programu ya Hatifungani ya miaka 10 yenye jumla ya thamani ya shilingi trilioni moja itakayotolewa katika fedha mbalimbali na kwamba hatifungani hiyo imeweka historia ya kuwa hatifungani kubwa zaidi yenye mlengo maalum kutolewa nchini Tanzania na Ukanda Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hayo yameelezwa leo Desemba 12, 2023 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) CPA Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la kwanza la hatifungani ya Benki ya NMB (NMB Kamii Bond) katika Soko la Hisa Dar es Salaam.
"Hatifungani imewezesha kupata fedha za kutekeleza miradi endelevu na yenye matokeo chanya kwa jamii.Idhini ilitolewa na CMSA baada ya benki ya NMB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania.
" Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya utoaji wa Hatifungani kwa umma; uwepo wa Muundo wa Hatifungani ulioandaliwa na benki ya NMB kwa kushirikiana na Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta za Fedha Barani Afrika (FSD Africa)...
"Na kukidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji na kupata ithibati kutoka kwa kampuni ya Sustainalytics ya nchini Uingereza, yenye utaalam kuhusu miradi endelevu kwa maendeleo ya jamii."
CPA Mkama amesema kwa namna ya pekee napenda kutambua mchango wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Union) hapa nchini, kwa kutujengea uwezo wa kitaalamu wafanyakazi wa Mamlaka na hivyo kuwezesha kuwa na ujuzi na weledi katika masuala ya hatifungani zinazokidhi matakwa endelevu na matokeo chanya kwa jamii.
Akifafanua zaidi amesema Mauzo ya Hatifungani ya NMB (NMB Jamii Bond) yalifunguliwa Septemba 25, 2023 na kufungwa Oktoba 27, 2023, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 212.94 kimepatikana, ikilinganishwa na Sh.bilioni 75 zilizotarajiwa kupatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 284.
Amesema kutokana na kiasi kilichopatikana kufikia Sh.bilioni 212.94, CMSA imeidhinisha Benki ya NMB kutumia kiasi chote kilichopatikana kutokana na uwepo wa mahitaji ya kutosha, kugharamia miradi endelevu na yenye matokeo chanya kwa jamii.
"Mauzo ya hatifungani hii yamekuwa na mwitikio chanya unaoashiria kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu uwekezaji katika masoko ya fedha hapa nchini, ambapo asilimia 98.7 ya wawekezaji walioshiriki ni wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 1.3 ya wawekezaji ni kampuni na taasisi."
Aidha amesema asilimia 99.9 ya wawekezaji ni wawekezaji wa ndani na asilimia 0.1 ni wawekezaji wa nje.Kwa upande wa kiasi kilichopatikana, asilimia 53.8 inatoka kwa wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 46.2 inatoka kwa kampuni na taasisi.
Pia asilimia 57.4 ya kiasi kilichopatikana inatoka kwa wawekezaji wa ndani na asilimia 42.6 inatoka kwa wawekezaji wa nje ya nchi huku akifafanua ushiriki wa wawekezaji mmoja mmoja wa ndani ni hatua muhimu katika kuongeza ukwasi katika soko na utekelezaji wa Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha.
CPA Mkama amesema hivyo wana kila sababu ya kuipongeza benki ya NMB na wadau wote walioshiriki katika kuwezesha mafanikio hayo na kueleza CMSA pia, ilitoa idhini kwa benki ya NMB kuuza hatifungani hiyo katika fedha za kigeni kwa mujibu wa kanuni na taratibu za masoko ya mitaji
Ambapo amesema kiasi cha Dola za Marekani milioni 73 kimepatikana, ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 10 zilizotarajiwa kupatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 730.
"Hatua hii imetoa fursa zaidi kwa wawekezaji wa kigeni, kampuni na mashirika kutoka nje ya nchi kuwekeza katika hatifungani ya NMB na hivyo kuchangia katika upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini.
"Kutokana na kiasi kilichopatikana kufikia Dola za Marekani milioni 73, CMSA imeidhinisha Benki ya NMB kutumia kiasi chote kilichopatikana kutokana na uwepo wa mahitaji ya kutosha, kugharamia miradi endelevu na yenye matokeo chanya kwa jamii.
"Hatifungani hii imepata mafanikio ya asilimia 284 kwa upande wa shilingi za kitanzania; na asilimia 730 kwa upande wa Dola za Marekani.Mafanikio haya ni uthibitisho wa imani waliyonayo wawekezaji kwa benki ya NMB na masoko ya mitaji hapa nchini.
" Kwani masoko ya mitaji Tanzania ni salama, himilivu, yenye ukwasi, na yanavutia na kukidhi matakwa ya wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.Mwitikio huu ni matokeo ya elimu ya uwekezaji inayoendelea kutolewa kwa umma na wadau katika sekta ya masoko ya mitaji kuhusu fursa na faida za kuwekeza katika masoko ya mitaji, "amesema.
CPA Mkama amesema mafanikio hayo yanatokana na mazingira wezeshi yanayotolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya kiongozi mahiri, Mhe. Dkt Samia Saluhu Hasan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na hayo amesema hivi karibuni, Serikali imeondoa kodi ya zuio kwenye faida inayotokana na uwekezaji kwenye hatifungani za kampuni, kama ilivyo kwa hatifungani za Serikali. Hiyo imekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kwenye masoko ya mitaji.
"Mazingira wezeshi yanayotolewa na Serikali yamekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya Sekta ya Fedha, hususan masoko ya mitaji ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 7.6 na kufikia Sh. trilioni 36.13 katika kipindi kilichoishia Novemba 2023, ikilinganishwa na Sh. trilioni 33.59 katika kipindi kilichoishia Novemba 2022.
"Thamani ya uwekezaji katika Hatifungani (Hatifungani za Serikali na Hatifungani za Kampuni) imeongezeka kwa asilimia 18.0 na kufikia Shilingi trilioni 19.76 katika kipindi kilichoishia Novemba 2023, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 16.75 katika kipindi kilichoishia Novemba 2022.
"Kwa mantiki hii, leo kutokana na korodheshwa kwa hatifungani ya NMB, thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni inaongezeka kutoka Shilingi bilioni 325.39 na kufikia Shilingi bilioni 721.13 sawa na ongezeko la asilimia 121.62.Hivyo, tuna kila sababu ya kuipongeza Benki ya NMB."
Pamoja na mambo mengine, uorodheshwaji wa hatifungani hiyo katika soko la hisa unawapatia fursa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale wanapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine; kujua thamani halisi ya hatifungani zao; na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizo, ambapo wawekazaji hao hupata riba kama faida itokanayo na uwekezaji huo.
Aidha, uorodheshwaji wa hatifungani za kampuni unaongeza utawala bora na ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni na kumwongezea mwekezaji wigo na fursa za uwekezaji. Hii inamsaidia mwekezaji kuwa na anuwai, jambo ambalo hupunguza athari za uwekezaji (Risk Diversification).
Ametoa mwito kwa benki za biashara, benki za wananchi, kampuni za bima, binafsi na mashirika ya umma kutumia fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuuza hisa na hatifungani kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ili kuongeza uwepo wa rasilimali fedha.
No comments:
Post a Comment