Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Benki mpya ya kisasa nchini, Letshego Faidika imetumia sh milioni 24 kuwazawadia wateja wao 30 kupitia kampeni ya Kopa Tukubusti iliyomalizika Desemba 11 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Meneja Biashara wa benki hiyo, Martin Peter Mosha wakati wa kuchezesha droo ya mwisho ya kampeni ya Kopa Tukubusti makao makuu ya benki hiyo.
Mosha alisema kuwa kati ya wateja 30 waliokopa katika benki hiyo, 27 walizawadiwa fedha taslimu wakati wateja watatu walizawadiwa zawadi ya pikipikipi.
Alisema kuwa benki hiyo itaendelea kuwawezesha wateja wao kupitia ubunifu wa kampeni mbalimbali na kuinua vipato vyao.
“Kupitia kampeni ya Kopa Tukubusti, mteja anakopa kiasi chochote cha fedha ambacho kinamwezesha kuingia moja kwa moja kwenye droo na akishinda anazawadiwa fedha nusu ya mkopo aliokopa. Hivyo kama ulikopa Sh milioni 10, ukishinda, unazawadiwa sh milioni 5 ambayo inaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti yako,” alisema Mosha.
Alisema kuwa mbali ya kutoa mikopo kwa wafanyakazi wa serikalini (taasisi za umma), pia wanatoa mikopo wa wajasiliamali na pia mikopo ya magari.
“Benki ya Letshego Faidika ni mpya na ina ubunifu mbalimbali kwa lengo la kuwafaidisha wateja wetu, ni muhimu kwa jamii kuangalia jinsi gani wanaweza kujiunga na kufaidika na huduma zetu mbalimbali,” alisema.
Katika droo ya mwisho, Sadiki Mpangachuma, Harrison Mbona, Hatibu Mchopa na Chacha Zakayo walishinda zawadi ya fedha taslimu wakati Peter Imiliki wa Kilosa, Morogoro alishinda zawadi ya pikipiki.
Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Bodi ya michezo ya kubahatisha nchini, Neema Tatock aliipongeza benki ya Letshego Faidika kwa kuendesha droo hiyo ambayo inawafaidisha wateja wake.
Tatock alisema kuwa wameridhishwa na bahati nasibu hiyo ambayo ilikuwa na tija kwa wateja kwani mteja aliyekopa fedha anaweza kupunguza makali ya marejesho baada ya kushinda.



No comments:
Post a Comment