HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 16, 2023

Takwimu sahihi nyenzo muhimu mapambano dhidi ya ukimwi

   

Na Zuhura Rashidi,Iringa.

 

UWEPO wa takwimu sahihi za wenye VVU unachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya mipango mikakati katika uratibu wa miradi ya kupambana na ukimwi imeelezwa mkoani Iringa jana.

Hayo yalisemwa na Maganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya  Mkoa wa Iringa, Dk. Mohamedi Mang’ula wakati wa ziara ya wawakilishi wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na ukimwi (PEPFAR), pamoja na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) hospitalini hapo ili kuangalia huduma mbalimbali za utoaji tiba kwa wenye VVU zinazofadhiliwa na mfuko huo kupitia USAID.

 Dk Mang’ula alisema hayo muda mfupi baada ya kukabidhiwa msaada wa kifaa cha kufanyia usajili wa wenye VVU kwa kutumia mfumo wa alama za vidole kilichokabidhiwa na Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bwana Craig Hart akishukuru ufadhili wa USAID uliochangia uboreshaji wa huduma za afya kwa wenye VVU hospitalini hapo.

“Tunaipongeza Kampuni ya Deloitte inayoendesha miradi hii inayofadhili na Mfuko wa PEPFAR katika mkoa wetu kwani imeweza kutusaidia kupata mafanikio makubwa katika kufikia malengo ya 95;95;95 katika kutambua wenye VVU, waliotambuliwa kuanza kupata tiba na suala la kufubaza virusi vya ukimwi”, alisema.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Afya Yangu Kusini, Dk. Marina Njelekela alisema wamekuwa na safari ndefu ila yenye mafanikio lukuki katika kutekeleza miradi inayofadhiliwa na PEPFAR kwa kupitia USAID.

Alisema misaada inayotolewa na PEPFAR kupitia Shirika la USAID  imesainia kuokoa maisha ya watanzania wengi katika kipindi hiki cha miaka 20 huku kukishuhudiwa uimarikaji mkubwa wa huduma kwa wenye VVU katika vituo mbalimbali nchini.

“USAID Afya Yangu Kusini tunasharehekea miaka 20 kwa kuboresha miradi ya PEPFAR USAID, tukipitia hatua mbalimbali za kimaendeleo moja ikiwa ni kuwajengea uwezo watoa huduma za afya katika vituo mbalimbali.

“Tumeboresha ubora wa utoaji huduma bora za VVU na Kifua Kikuu katika ngazi ya jamii, mwaka 2004 tukiwa na vituo vya kutolewa huduma 33 lakini kwa msaada wa PEPFAR kwa hadi  mwaka 2023 tumeweza kufikisha vituo 676.

“Deloitte pamoja na washirika wake wa kiufundi wa MDH na T-marc tunajivunia sana kusimamia miradi inayofadhiliwa na PEPFAR,  mwaka 2004 aina ya wagonjwa tulioanza nao kwa sasa imebadilika kabisa, sasa wapo na furaha na matumaini, wamewezeshwa, hawajisikii unyanyapaa”, alisema Dk. Marina.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraa la Taifa la Watu Wanaoishi na UVVU Tanzania (NACOPHA), Bwana Deogratius Rutwatwa wanaoendesha mradi wa ‘Hebu Tuyajenge’ alisema moja ya mikakati ya malengo ya mradi huo ni kuhakikisha pamoja na mambo mengine watu wenye maambukizi ya VVU wanatambua hali zao.

Ofisa mtendaji huyo alizungumzia suala la unyanyapaa kuwa moja ya changamoto inayosababisha watu wengi wenye VVU kushindwa kujitokeza kupata huduma za upimaji na kuunganishwa kwenye vituo vya tiba.

“Baadhi ya huduma tunazozitoa ni pamoja na elimu kwa wenye VVU  kuhusu namna bora ya kujzuia maambukizi mapya, kutambua wenza na watoto wenye VVU hivyo kuwaunganisha kwenye huduma za upimaji na kutoa usaidizi juu ya matumizi sahihi ya dawa za ARV’s.

“Kwa namna ya kipekee niupongeze Mfuko wa PEPFAR kupitia USAID kipindi hiki unapotimiza miaka 20 kwa mafanikio na jitihada zake katika kupambana na janga la ugonjwa wa ukimwi hapa Tanzania”, alisema.     


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la maendeleo ya kimataifa (USAID) Bw. Craig Hart (katikati)  akiangalia, wakati mmoja wa wenye VVU akijisajili katika mfumo wa alama za vidole mara baada ya mkurugenzi huyo kukabidhi msaada wa kifaa hicho kwa hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Mfumo huo unasaidia kupata takwimu sahihi za wenye VVU, jambo ambalo ni muhimu katika kufanikisha utoaji wa huduma bora . Hafla hiyo iliyofanyika mkoani humo jana inakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR) unaofadhili miradi ya kupabana na Ukimwi inayosimamiwa na (USAID)

Mkurugenzi wa mradi wa USAID Afya yangu kanda ya Kusini unaoendeshwa na Shirika la Deloitte, Dk Marina Njekela, akielezea utendaji na mafanikio ya mradi huo katika kutoa huduma bora kwa wenye VVU katika hafla hiyo Mjini Iringa jana.

 Baadhi ya wanawake waliowezeshwa na Mradi wa Hebu tuyajenge unaoendeshwa na Shirika la NACOPHA wakishangilia wakati wa ziara ya wawakilishi wa PEPFAR, USAID wakitembelea katika ofisi za shirika  hilo mjini Iringa jana.

Mwakilishi wa mabinti wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi Tanzania, Lucy Michael Mpwage, aliyezaliwa na maambukizi ya ugonjwa huo akitoa ushuhuda pamoja na changamoto za unyanyapaa alizokumbana nazo katika vipindi tofauti vya maisha yake na jinsi huduma za miradi ya USAID inayoendeshwa na Shirika la Deloitte ilivyookoa maisha yake. Ilikua ni wakati wawakilishi wa mfuko PEPFAR, USAID, mashirika yanayosimamia utoaji wa huduma kwa wenye VVU pamoja na waandishi wa wabari wakitembelea Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa jana, kuangalia mafanikio ya miradi hiyo .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad