HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 23, 2023

SOMBI ATOA VIFAA VYA TEHAMA KWA SENATE

Aahidi UVCCM itaendelea kuwashika mkono vijana

Na MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Rehema Sombi, amesema umoja huo utaendelea kuwaunga mkono vijana wote wanauokiunga mkono Chama katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.

Ahadi hiyo ameitoa leo Novemba 21, 2023 alipokabidhi vifaa mbalimbali vya kiofisi kwa Senate ya Vyuo na Vyuo Vikuu hatua iliyotokana na ombi la kufanya hivyo alipozitembelea Senate mbalimbali kwa lengo la kuimarisha utendaji wao.

Rehema amewataka vijana waliopata fursa ya kupata elimu katika ngazi na taasisi mbalimbali kuhakikisha wanasoma kwa bidii na maarifa makubwa.

“Leo imekuwa faraja kubwa kwangu kuwa mahali hapa na kutekeleza ahadi hii ya kuwaletea vifaa ya TEHAMA pamoja na ‘stationaries’.

“Kama mnavyojua kuwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ni chombo kinachowaunganisha vijana wote wa Tanzania wanaounga mkono sera, siasa na itikadi ya Chama Cha Mapinduzi.

“Shabaha ya Chama kuunda Umoja wa Vijana wa CCM ni kuwa shule ya kuandaa wanachama safi, viongozi bora wa CCM imara. Kwa mnasaba huo, UVCCM inaendelea kuandaa vijana kuwa raia wema kwa taifa letu na kwamba chombo hiki ni sawa na tanuri la kuoka makada wazuri wa Chama chetu,” amesema.

Amesema kuwa umoja huo una wajibu wa kuongoza shughuli zinazohusu maendeleo na maslahi ya vijana nchini.

Kwa mujibu wa Rehema, kutokana na msingi huo ndio maana zilianzishwa senate za vyuo vikuu za UVCCM ikiwa njia mojawapo ya kuwatambua vijana wenye vipawa na kuwaandaa kulitumikia taifa “vijana ambao watakuwa na imani ya Chama chetu na watakubali kuishi katika misingi ya taifa letu.”

“Binafsi kwa niaba ya umoja wa vijana nilipata wasaa wa kutembelea senate za vyuo kadhaa ambapo pamoja na mambo mengine mlinieleza ukosefu wa vifaa vya TEHAMA na stationaries.

“Nimeendelea kufanya juhudi kuhakikisha nawaona wadau wa maendeleo. Naushukuru Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, Bi. Justina Mashiba kwa kuonesha nia na kutoa mchango katika kugusa wanafunzi na elimu ya juu na kutupatia vifaa hivi ambavyo leo naviwasilisha kwenu,” amesema.

Amesisitiza kuwa UVCCM itaendelea kuwa kamisaa wa kuhakikisha inatambua mchango wa vijana wanaounga mkono juhudi za Chama walioko vyuo vikuu kupitia senate na kuwa daraja la kuwaunganisha na wanachi katika ujenzi wa maendeleo ya taifa.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad