HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 16, 2023

SERIKALI YAITAKA MUHAS KUSIMAMIA MIRADI ILI KUONGEZA UDAHILI WA WANAFUNZI

Profesa Eligius Lyamuya wa Microbiology na Immunoology kutoka MUHAS  akionesha tuzo mara baada ya kukabidhiwa leo Novemba 16, 2023 wakati wa Kongamano la kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa MUHAS
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msofe (Kulia) akimpa tuzo Mwanafunzi wa kwanza kusoma Chuo Cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt. Fredrick Kigadye kilipoanzishwa mwaka 1963.
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msofe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo  Novemba 16, 2023 wakati wa kongomano la miaka 60 ya Chuo Cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) tangu kuanzishwa kwake nchini.
Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya, Muhimbili (MUHAS) Prof Apolinary Kamuhabwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo  Novemba 16, 2023 wakati wa kongomano la miaka 60 ya Chuo Cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) tangu kuanzishwa kwake nchini.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya, Muhimbili(MUHAS) zamani Prof. Projustine Muganyizi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa kongamano la Chuocha MUHAS   linafanyika jijini Dar es Salaam leo Novemba 16, 2023.

Na Karama Kenyunko Michuzi tv 
SERIKALI  imekitaka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)  kusimamia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi Ndaki ya Tiba (HEET) utakaojenga  Kampasi ya Mloganzila na Kigoma Ujiji ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa asilimia 30.

Pia imekitaka chuo hicho kufanya tafiti zaidi ambazo zitaboresha sera za afya za muda mfupi na mrefu  ili kusiwepo madhara katika afya za wananchi.

Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msofe  ameyasema hayo leo Novemba 16, 2023 jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la miaka 60 ya MUHAS kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.


Amesema uanzishwaji wa ndaki hiyo unaendana na maono ya chuo ya kufanya mageuzi na kuwa mji wa taaluma za afya kufikia 2050.

"Ni imani yangu mtaendelea kutekeleza mradi kwa kuzingatia ratiba na malengo mliojiwekea kwa kuzingatia viwango vya serikali na Benki ya Dunia. Amesema Prof. Mkenda.

"Mradi huu ukisimamiwa utaongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa asilimia 30 katika maeneo 14 ya kipaumbele kwa uchumi wetu wa kati wa viwanda,"amefafanua Prof. Mkenda.

Pia amewasisitiza kuzingatia rasilimali zilizopo kwani serikali inaboresha uchumi kwa kuleta mapinduzi ya viwanda na kuhakikisha maisha na afya za wanafunzi zinaboreshwa.

Akizungumzia kuhusu tafiti, Prof. Mkenda amesema, chuo hicho kinaongoza kwa tafiti nyingi za afya nchini na kwamba zimeweza kuleta mapinduzi kwenye sera na miongozo inayotumika ndani na nje ya nchi hususan katika kuboresha huduma za afya, kutoa matibabu sahihi na kuzuia magonjwa.

Amesema, tafiti hizo zimechangia kukiweka chuo katika nafasi nzuri kwenye uanzishwaji wa vyuo vikuu bora nchini, barani Afrika na duniani kwa ujumla na kwamba ukuaji wa vyuo vikuu Tanzania hususan vinavyotoa elimu na kufanya tafiti za afya ni miongoni mwa mafanikio makubwa ambayo nchi inaendelea kujivunia katika sekta ya elimu na afya.

Profesa Mkenda amesema kuwepo kwa nia thabiti ya serikali na sera rafiki, imechangia kuwa na vyuo 13 vya serikali vinavyotoa mafunzo ya shahada mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na udaktari.

"Ongezeko hili limesaidia kuongeza wataalamu katika sekta ya afya ambayo bado inakumbwa na uchache wa wataalamu. Tangu chuo kianzishwe kimezalisha wataalamu wa afya 20,000 kwa ngazi ya shahada ya awali na wataalamu bingwa 4,200 wa ngazi ya uzamili na uzamivu," amesema Profesa Mkenda.

 
Kwa upande wa  Profesa Appolinary Kamuhabwa, Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS, amesema katika miaka ya 1960 magonjwa makubwa yaliyokuwa yakiikabili nchi ni pamoja na Malaria, Kifua Kikuu, Ukimwi na Virusi Vya Ukimwi.

Amesema miongozo iliyotolewa kuhusu matumizi ya dawa na namna ya kuhudumia wagonjwa hao zimetokana na tafiti walizozifanya na washirika wengine hivyo, zimeboresha sera.

"Kwa sasa magonjwa ya kuambukiza ndio yameshika kasi kama kisukari shinikizo la damu, moyo na figo hivyo majibu ya tafiti zetu ndio tegemeo na pia inatupa muongozo katika mitaala yetu," 

Amesema matokeo ya utafiti ambazo zimefanyika chuoni yamekuwa na mchango mkubwa katika kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya afya yanayoikabili jamii.

"Tafiti zimesaidia kuboresha sera na miongozo ya matibabu na kuboresha huduma na mifumo ya afya. Watafiti wa Muhas wamekuwa vinara nchini na duniani kutokana na ubora wa tafiti zao na mchango mkubwa waliouonesha katika ubobezi wao," alisema Profesa Kamuhabwa.

Amesema chuo hicho kimeongeza idadi ya shahada za uzamili hadi kufikia 84 na kinaendelea kutoa kipaumbele na kuandaa wanafunzi wa shahada za uzamivu ambao ndio msingi wa tafiti.

"Chuo kimeongeza idadi ya mahusiano ya kitafiti na vyuo na taasisi nyingine kufikia washiriki 136 wa ndani na nje ya nchi hivyo na hivyo kuratibu zaidi ya miradi 130 ya utafiti kwa mwaka huu jambo ambao  linaendelea kukua na kupanua mazingira ya ufundishaji na utafiti kwa kuchukua nafasi kubwa ya kutoa ushauri wa kitaaluma kwenye masuala ya afya katika taasisi, serikali na jumuiya ya kimataifa". Amesema Prof.  Kamuhabwa

Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Projestina Muganyizi amesema chuo hicho kimepiga hatua katika kufanya tafiti kwani kina wanataaluma zaidi ya 400 ambao wanafanya utafiti.

Amesema chuo hicho kimewasaidia kutoa miongozo mbalimbali iliyowasaidia kuboresha sekta ya afya kwani zamani walikuwa wanafunzi wasiozidi 45 na walikuwa tunatumia hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na  wagonjwa walikuwa wanahudumiwa na wanafunzi wengi kuliko sasa wagonjwa ni wachache kuliko wanafunzi," amesema Profesa Muganyizi.

Wakati wa kongamano hilo la miaka 60 ya MUHAS tangu kuanzishwa kwake wametambua mchango wa Mwanafunzi pekee aliyesoma chuo hicho mwaka 1963 kilipoanzishwa pamoja na mchango wa wafanyakai wa chuo tangu kuanzishwa kwakwe mpaka sasa kwa kuwapa tuzo.
Matukio mbalimbali wakati wa Kongamano la miaka 60 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya, Muhimbili(MUHAS) leo Novemba 16, 2023.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad