HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 14, 2023

Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Imeridhika na Uendeshaji na Uendelezaji wa Kiwanda cha Maji cha Uhuru Peak


KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeridhika na uendeshaji na uendelezaji wa Kiwanda cha maji cha Uhuru Peak kinachoendeshwa na Suma JKT baada ya kuongeza uzalishaji wa maji.

Hivyo, imeyataka mashirika ya umma, Wizara na taasisi za serikali zinunue maji ya Uhuru Peak ili kuendeleza ukuaji wa kiwanda hicho.

Akizungumza leo walipotembelea kiwanda hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge la Tanzania Vita Kawawa amesema maagizo ya serikali yalielekeza taasisi za serikali wanapoandaa shughuli mbalimbali wanunue maji yanayozalishwa na Suma JKT.

Amesema hapo awali kiwanda hicho kilikuwa kinazalisha lita 3250 kwa saa na baada ya kufunga mitambo mipya yenye uwezo mkubwa wanazalisha lita 10,000 kwa saa na wamebadili muonekano wa chupa.

"Wameongeza ufanisi mkubwa ambao tumeshuhudia wenyewe kwani uwekezaji walioufanya kununua kiwanda kipya umegharimu Sh bilioni 1.6 na kuzalisha maji lita 10,000 kwa saa," amesema Kawawa

Ameongeza kuwa maji yapo na yanazalishwa kwa wingi ambayo yana viwango vya kutosha.

Kawawa amesema kazi iliyopo ni kutafuta masoko ili kufika katika mikoa yote kwani wamewekeza kibiashara hivyo, watengeneze miundombinu ya kufikia wateja wote waliowakusudia.

Kwa upande wake, Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele amesema kamati hiyo ilishinikiza utekelezaji kwa kupanua kiwanda na kufunga mitambo Ili kuzalisha maji kwa wingi.

"Wameridhika na kile ambacho waliagiza na tumetekeleza. Niwathibitishie watanzania kwamba tunadhamira ya kufanya biashara hii ya maji kwani ni salama," amesema Meja Jenerali Mabele.

Ameeleza kuwa mpango wao ni kuhakikisha maji hayo yanafika mikoa yote ya Tanzania.

Amesema tayari wameingia mkataba na Shirika la Reli Tanzania kwa mikoa yote inayopitiwa na reli ya kati iweze kusafirisha maji yao kwa gharama ile ile ili kutokuwa na utofauti wa bei kwa watu wa Morogoro na Kigoma.

"Tayari tumefanya majaribio wametusafidishia maji mpaka Dodoma na biashara ilikuwa nzuri bila shida yoyote lakini pia tutaongeza magari kwenda zaidi mikoani badala ya Dar es Salaam pekee," ameeleza.
Picha ya Pamoja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge la Tanzania Vita Kawawa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Kiwanda cha Maji cha Uhuru Peak kilichopo JKT Mgulani jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2023.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Kiwanda cha Maji cha Uhuru Peak kilichopo JKT Mgulani jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2023.











Matukio mbalimbali ya wabunge wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge la Tanzania wakipata maelekezo mara baada ya kutembelea Kiwanda cha Maji cha Uhuru Peak kilichopo JKT Mgulani jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2023.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad