NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
BENKI
ya NMB imemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia
Suluhu Hassan kwamba itaendelea kuwa mdau kinara wa Serikali yake katika
kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Watanzania.
Ahadi hiyo
imetolewa jana Agosti 31 na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Ruth
Zaipuna, wakati akitoa shukrani na salamu kwa Rais Samia, wakati
akifunga Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2023), lililofanyika
kwa wiki moja kwenye Viwanja vya Paje, Mkoa wa Kusini Unguja.
Kizimkazi
Festival limekuwa likitumika kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo
inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT),
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), pamoja na wadau zikiwemo
taasisi binafsi, ambako Rais Samia alizindua miradi miwili mikubwa
(Agosti 29 na 30) iliyofanywa na NMB.
Bi. Zaipuna alimhakikishia
Rais Samia kwamba, NMB itabaki mstari wa mbele katika kusapoti jitihada
zake na zile za Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi za kuwaletea
maendeleo Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla, huku akibainisha kuwa
miradi miwili iliyozinduliwa kupitia tamasha hilo, itatoa mchango mkubwa
wa maisha bora kielimu na kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
"Jana
(Agosti 30), tumezindua Tawi la NMB Paje, ambalo umelizindua wewe
mwenyewe, tunaamini tawi hili linaenda kuwa suluhu ya changamoto za
huduma za kibenki walizokuwa wanakabiliana nazo wakazi wa Paje, ambao
walilazimika kusafiri kilomita 60 kufuata huduma hizo katika tawi letu
la Mwanakwerekwe.
"Tunaamini ujio wa Tawi la NMB Paje, utachagiza
ongezeko la Watanzania wanaotumia huduma za kibenki, ambao kwa takwimu
zilizopo sasa wapo asilimia 22 tu. NMB tunalitambua hilo, ndio maana
kupitia tawi hili, tutatoa elimu ya fedha kwa wananchi, wakiwemo
wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi na wajasiriamali.
"Kama
tunavyofanya popote tunapofungua tawi jipya, kutoa sehemu ya faida yetu
kupitia Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), hapa Kusini Unguja wewe
mwenyewe umeweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Skuli ya Maandalizi ya
Tasani, kule Makunduchi, ambayo (ujenzi na samani za ndani) itatugharimu
Sh. Mil. 600 hadi itakapokamilika Disemba mwaka huu, ili kuruhusu
watoto wa maeneo jirani kuanza masomo Januari 2024," alibainisha Bi.
Zaipuna.
Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu huyo alimpongeza Rais Samia
kwa wazo chanya lililozaa Tamasha la Kizimkazi, ambalo limekuwa mhimili
na chachu ya miradi mbalimbali ya maendeleo endelevu ya kielimu na
kiuchumi miongoni mwa Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla wake.
Kwa
upande wake, Rais Samia aliipongeza NMB sio tu kwa ushiriki endelevu wa
kufanya miradi ya maendeleo kwa miaka kadhaa, bali pia kwa kusapoti
Serikali kupitia tamasha hilo, ilikofanya mambo muhimu kwa ustawi wa
Wazanzibar kielimu na kiuchumi, mwaka huu kupitia miradi yao miwili ya
Skuli ya Maandalizi Tasani na Tawi jipya la NMB Paje.
"Ahsanteni
wadau wote wa maendeleo mliofanya uwekezaji mkubwa katika Sekta za Elimu
na Uchumi. Shukrani kwa NMB ambayo inagharamia ujenzi wa Skuli ya
Maandalizi Tasani, ambako nimeweka Jiwe la Msingi juzi, tayari kwa
ujenzi unaoenda kutoa elimu ya awali kwa watoto wetu wa Makunduchi.
"Jana,
nimezindua Tawi jipya NMB Paje na kitu cha kufurahisha ni kuona licha
ya uchanga wa tawi, lakini kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wateja.
"Na
habari njema kwa wote ni kuwa na mimi ni mteja wa NMB, ingawa nimekuwa
hivyo kwa muda mrefu kabla hata ya ufunguzi huu wa jana," alisisitiza
Rais Samia na kuzidi kuipongeza NMB na taasisi kadhaa za fedha kwa
udhamini endelevu kwa miaka mingi ya tamasha hilo.
No comments:
Post a Comment