Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SHILINGI Bilioni 700 kutoka benki ya dunia zitaelekezwa kwenye maeneo ya miundombinu ya umwagiliaji na zitakwenda kujenga miundombinu ya umwagiliaji Kwa wakulima wadogo.
Waziri wa kilimo Hussein Bashe ameyasema hayo leo Septemba 6, 2023 Wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kustahimili Chakula Tanzania (TFSRP) katika jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linaloendelea kufanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JINCC). Amesema kuwa fedha hizo ni kwaajili ya kusimamia mpango wa kustahimili mifumo ya chakula Tanzania (TFSRP).
Amesema lengo la nchi lilikuwa nikutafuta fedha Kwa ajili ya sekta ya kilimo na katika hilo walikuwa na mazungumzo na Benki ya Dunia ambapo leo wameweza kupata Dola milioni 300 Kwa ajili ya sekta ya kilimo.
Waziri Bashe amesema kuwa kulikuwa na majadiliano ya namna ya kutuza mazingira hivyo hawakuweza kutatua tatizo la mazingira kama hawawezi kuondoa tatizo la umasikini la watu kwahiyo walizungumza na Benki ya Dunia ili kuaza kupambana na umasikini kwa kuanzisha kilimo biashara kwa wananchi.
"Tumeweza kufikia mwisho na mpango huu unaaza kutekelezwa mwaka huu Kwa ajili ya kujenga miundombinu ni mpango wa miaka mitano lakini tutajitahidi tutumie fedha hizi ndani ya miaka mitatu na ndicho tulichokubaliana na moja ya makubaliano ni kujenga miundombinu ya umwagiliaji ya zaidi ya hekta 37 hii itasaidia kuongeza eneo letu la uzalishaji na bahati nzuri wakati wanakuja wao tayari sisi tulishakuwa na dizaini ya miradi ambayo tunataka kuifanya ."Amesema Waziri Bashe
Ameongeza kuwa "kutakuwa na uzinduzi na baada ya hapo tutakuwa tumemalizana na wao na fedha hizi ni mkopo Kwa ajili ya kuwekeza kwenye kilimo kwani Kwa muda mrefu benki ya dunia ilikuwa ikitoa fedha Kwa ajili ya kujenga barabara, kwahiyo mradi wa TFSRP utakuwa wa kwanza kupata fedha kwaajili ya kilimo Moja Kwa Moja."Amesisitiza Waziri Bashe
"Tunaamini kwamba hata kama nchi inakopa italipa deni hilo kutokana na shughuli za kiuchumi na nyingi zipo kwenye sekta ya kilimo na ili kuweza kuwafanya wakulima wazalishe na ni lazima kutatua matatizo yanayo waathiri mbegu, huduma za ugani na miundombinu ya umwagiliaji ili mkulima aweze kuzalisha mara mbili, mara tatu Kwa mwaka kwahiyo fedha hizo ni mkopo wa muda mrefu unakwenda moja Kwa moja kwenye kilimo." Amesema Waziri Bashe
Mpango wa Kustahimili Mifumo ya Chakula Tanzania (TFSRP) Serikali ya Tanzania inakabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwahiyo fedha hizo zitaongeza nguvu ili kuwa na ustahimilivu wa chakula.
Kwa upande wa Waziri wa Kilimo, Umwangiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Shaame Khamis amesema kuwa Mbinu mpya za biashara zitakazoanzishwa kupitia mpango huo zitaongeza uwekezaji wa mitaji ya Serikali na kulenga kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uhaba wa maji kwenye mifumo iliyopo ya umwagiliaji na kupunguza hasara baada ya kuvuna.
Pia amesema kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi kutaharakisha maendeleo endelevu katika kuongeza tija na ustahimilivu wa mifumo ya Chakula kwa visiwani na Tanzania bara.
Amesema fedha hizo zitaongeza uwezo wa uzalishaji shambani kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za kilimo (mbegu, utafiti na ugani), ambayo inasaidia kuhimili hali ya hewa.
"Kuboresha ufanisi wa matumizi ya maji ya shambani kama kinga dhidi ya ukame na kupunguza hasara za baada ya kuvuna zinazohusishwa na uzalishaji katika kilimo pamoja na uhifadhi bora pamoja na usindikaji wa chakula.
Kwa Upande wa katibu Mkuu wizara ya kilimo, Gerald Mweli amesema vipaumbele muhimu vya uwekezaji katika mpango wa TFSRP ni pamoja na kuongeza tija, kuboresha usalama wa chakula na lishe, na kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya mabadiliko ya tabianchi kupitia matumizi ya teknolojia bora kama vile umwagiliaji na mbegu.
Amesema ufanisi zaidi unahitajika ili kupambana na athari za uwekezaji wa umma na zana za sera hasa katika kutekeleza mpango wa TFSRP ambao umeundwa kama Mpango wa Matokeo (PforR) itaimarisha uvumbuzi na kuboresha maarifa na mifumo ikolojia inayohusiana na kuongeza ufikiaji wa teknolojia ya hali ya hewa, mifumo ya tahadhari ya mapema, na kuondokana na ukame.
Waziri wa kilimo Hussein Bashe akiwa na viongozi wengine waonesha vitabu vya mpango wa Kustahimili Mifumo ya Chakula Tanzania (TFSRP), uzinduzi huo umefanyika katika jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linaloendelea kufanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JINCC), leo Septemba 06, 2023.
Waziri wa kilimo Hussein Bashe akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mpango wa Kustahimili Mifumo ya Chakula Tanzania (TFSRP), uzinduzi huo umefanyika katika jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linaloendelea kufanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JINCC), leo Septemba 06, 2023.
Waziri wa kilimo Hussein Bashe akizungumza katika uzinduzi wa uzinduzi wa mpango wa Kustahimili Mifumo ya Chakula Tanzania (TFSRP) umefanyika katika jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linaloendelea kufanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JINCC), leo Septemba 06, 2023.
Picha ya pamoja.
No comments:
Post a Comment