HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 18, 2023

KONGAMANO LA 10 LA THS KUFANYIKA OKTOBA, MDH KUENDELEA KUTOA HUDUMA ZA UKIMWI

 Rais wa Kongamano la Afya Tanzania (Tanzania Tanzania Health Summit,(THS) Omary Chillo katikati akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 18, 2023 kuhusu kongamano la 10 la Kitaifa la Afya linalotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 3-5, 2023 katika Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Tathmini Afya ya Jamii kutoka Shirika la MDH, Dk Wilhelmuss Mauka akizungumza na Michuzi Tv leo Septemba 18, 2023 kuhusu kongamano la 10 la Kitaifa la Afya linalotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 3-5, 2023 katika Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

KONGAMANO la 10 la Afya Tanzania (THS), litakalofanyika Oktoba 3 hadi 5 mwaka huu,  linatarajia  kujadili mfumo wa afya, upatikanaji wa huduma za afya kwa wote na huduma za afya ya msingi.

Aidha, katika kongamano hilo, Shirika la MDH litaeleza namna lilivyohakikisha upatikanaji wa huduma za Ukimwi zinaendelea kutolewa licha ya mlipuko wa ugonjwa wa Marburg huko mkoani Kagera .

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Meneja wa Tathmini Afya ya Jamii kutoka Shirika la MDH, Dk Wilhelmuss Mauka amesema katika kongamano hilo watazungumzia afya ya pamoja na namna walivyotekeleza utoaji wa huduma kwa wenye Ukimwi wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg.

Lengo ni kutaka kuelezea namna walivyokabiliana nalo na kushirikiana na wadau, serikali na wagonjwa kupata huduma kama kawaida huku wakiendelea na utekelezaji wa huduma hizo Mkoa wa Kagera.

Ameeleza kuwa Afrika Mashariki na Afrika imekuwa ikikabiliwa na ugonjwa huo wa Marburg na Tanzania wamepata uzoefu ambao hawakuwahi kuwa nao awali kutokana na kuambukiza kwa kugusa.

"Wakati tunatoa huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi watu wanakuwa wengi na wamejazana hivyo MDH kwa kushirikiana na serikali walitafuta namna ya kuzuia maambukizi wakati wakiendelea kutoa huduma hizo," 

Amesema kama shirika lisilo la kiserikali watazungumza namna walivyoshirikiana na serikali kutoa huduma za afya huku wakipambana na ugonjwa huo kuanzia Machi hadi Mei.

Akizungumzia takwimu za ugonjwa wa Ukimwi, Dk Mauka alisema asilimia 95 ya Watanzania wanajua hali zao, asilimia 95 wameanza kutumia dawa na wengine wanaendelea na huduma za dawa.

"Malengo ya dunia ni kufikia mwaka 2030 kutokuwa na maambukizi mapya ya Ukimwi na vifo," alisema Dk Mauka.

Alishauri wadau kutoa elimu kwa Watanzania wote ili waweze kupata huduma ya kupima na dawa ili kuepuka maambukizi mapya ya Ukimwi.

Kuhusu bima, alisema serikali inatoa muongozo kuhusu masuala ya bima, hivyo kama wadau wanatakiwa kujipanga na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma zinapatikana.

Alisema kama shirika wataangalia maeneo mengine ambayo wanaweza kuisaidia serikali ili watu wote wapate huduma za afya bure.

Dk Dunstan Mshana  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), amesema mikutano ya nyuma ilikuwa na mafanikio na kwamba kuongeza kwa wadau katika mkutano huo utainua sekta ya afya.

Amesema wao ni watekelezaji wa sera kuwezesha ufanisi wa  zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya 

Ameeleza kuwa wanaweka utekelezaji mzuri wa Mfuko wa afya ya pamoja kwani kuna vituo vya afya zaidi ya 1,800 vimejengwa kwa miaka mitano hususan katika sehemu ambazo hazikuwa na huduma.

Amesema wamekuwa wakiajiri kujenga mazingira rafiki na kufikia wananchi katika huduma za afya na kuhakikisha kwamba ngazi za chini za huduma zinakuwa mali ya wananchi.

"Tunahakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kuhakikisha huduma nzuri za afya zinatolewa kwa ngazi zote na wananchi wafurahie," amesisitiza Dk Mshana.

Ameongeza kuwa wataendelea kuwawezesha na kuwasaidia wadau wote wa afya kutekeleza majukumu yao ya  vizuri.

Mkuu wa Divisheni ya Utafiti Wizara ya Afya Zanzibar, Rashid Maulid Rashid amesema kuwa sera ya kuboresha huduma za afya kwa kuzingatia ngazi za chini inawagusa na kwamba wanashirikiana na wadau kuhakikisha huduma za msingi zinaanzia chini.

Amesema kila kilometa tano kuna vituo vya afya kuhakikisha huduma za afya karibu na kwamba hivi sasa wana wana hospitali kwa kila Wilaya.

"Kuhusu Mfuko wa bima ya Afya wananchi kupata huduma za afya bila kikwazo na kwamba wananchi wote wa Zanzibar watapata huduma za afya za uhakika hata wenye kipato cha chini kwa kupata matibabu bure," amesitiza Rashid.

Joseph Mhagama Meneja Utawala Aphta amesema kuwa wameshiriki kongamano hilo tangu linaanza na kuelezea kuwa moja ya maeneo muhimu katika utoaji wa huduma za afya ni katika ngazi za chini.

Ameongeza ili kuhakikisha afya kwa wote ni lazima kuhakikisha ubora wa huduma za afya na katika kongamano hilo, watazungumzia ubora.

Katika kongamano hilo, wajumbe 1,000 kutoka mashirika ya ndani na kimataifa wanatarajia kushiriki na litazikutanisha taasisi 50 ambazo zimethibitisha ushiriki wao, wawekezaji katika huduma za afya, wabunifu, wataalamu, viongozi wa Serikali na viongozi wa sekta binafsi ili kujadili mwenendo na maendeleo ya  huduma za afya nchini Tanzania.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni Kuimarisha Mifumo ya Afya kwa ajili ya Huduma za afya kwa wote UHC, ikilenga Huduma ya Afya ya Msingi(PHC). 

Taasisi zinazoratibu mkutano huo ni Wizara ya Afya (MoH), Wizara ya Afya-Zanzibar, Baraza la Kiislamu Tanzania (BAKWATA), Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Muungano wa Vituo vya Afya Binafsi Tanzania (APHFTA) na TMHS Tanzania.

Mkuu wa divisheni ya utafiti Wizara ya Afya Zanzibar, Rashid Maulid Rashid akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 18, 2023 kuhusu kongamano la 10 la Kitaifa la Afya linalotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 3-5, 2023 katika Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad