Na. Jacob Kasiri - Iringa.
Shirika
la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Idara ya Mahusiano kwa
Jamii (Ujirani Mwema) katika Hifadhi ya Taifa Ruaha imekabidhi vifaa
vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 31 kwa ajili ya mradi wa
maji safi na salama unaotarajia kuanza hivi karibuni ili kumtua mama
ndoo kichwani na kumpunguzia hadha ya kutembea umbali mrefu kufuata
huduma hiyo. Zoezi la kukabidhi vifaa hivyo limefanyika leo tarehe
31.08.2023 katika kijiji cha Tungamalenga kilichopo Halmashauri ya
Wilaya ya Iringa.
Vifaa hivyo vilivyonunuliwa na TANAPA ni
pamoja na mipira ya kupitishia maji (GS Pipe medium na Polly pipe 63 mm)
kwa ajili ya kutandazia chini zaidi ya kilometa 2 na vifaa vingine vya
mradi wote. Wanufaika wa mradi huo wamechangia nguvu kazi kwa kuchimba
mitaro na shilingi milioni 3.2. Shirika linaamini mradi huo
utakapokamilika unapunguza changamoto ya ukosefu wa maji katika kijiji
hicho.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi
Godwell Meng’ataki, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema "ninayo
furaha kubwa kutoa vifaa hivyo ikiwa ni faida inayotokana na utalii,
hivyo naahidi kushirikiana nanyi hadi mradi huu utakapokamilika."
"Kwa
takribani miaka 12 TANAPA imetekeleza miradi mingi sana. Kama shirika
tumetekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 13 ikihusisha
miradi zaidi ya 327 ya afya, elimu,maji na mpango wa matumizi bora ya
ardhi kijiji cha Tungamalenga kikiwa ni miongoni mwa vijiji hivyo. Kwa
mantiko hiyo tunawajibika kwa wananchi kutekeleza miradi ili
kuwapunguzia adha", alisema Kamishna Meing’ataki.
Hata hivyo,
Kamishna huyo aliongeza "tunapokabidhi vifaa hivi tujue msingi wake
mkubwa ni uhifadhi. Tunaposhirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo
wananchi hawa katika uhifadhi na kuibua miradi kama hii, tunapata faraja
kama shirika kuona wananchi wanatambua thamani ya Maliasili zao".
Aidha,Naibu
Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Steria Ndaga, Mkuu wa Kanda ya Kusini
aliwaambia wananchi hao licha ya kukabidhiwa vifaa kwa ajili ya mradi wa
maji, kijiji cha Tungamalenga ni wanufaika zaidi wa miradi mingine ya
ujenzi wa madarasa na nyumba mbili za walimu walizojengewa hivyo
wailinde na kuitunza, pia aliwataka wawe mstari wa mbele kufichua
vitendo vya ujangili vinavyoendelea katika hifadhi hiyo.
Akikabidhi
vifaa vya mradi wa maji safi na salama kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya
Iringa Mhe.Veronica Kessy, Katibu Tawala Bw. Michael Semindu alisema,
"kukamilika kwa mradi huu utaondoa changamoto ya maji hapa. Najua tanki
lililopo lina ujazo wa lita 60000 na lilijengwa takribani miaka 20
iliyopita kipindi idadi ya watu ilikuwa ni chini ya 2500, kwa sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2022, kijiji hiki kina zaidi ya wananchi 3600.
Niwashukuru Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kutambua adha hii"
Kulingana
na taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Afya,mtu
mmoja anatakiwa atumie maji lita 50 kwa mahitaji yake yote ya msingi kwa
siku. Hivyo uwiano uliopo katika kijiji chaTungamalenga hakikidhi
matakwa ya umoja wa Mataifa, hivyo TANAPA imeona ni vema kutekeleza
mradi huo ili kutatua adha ya maji safi na salama.
Mmoja wa
wanufaika Bi. Jennifer Joseph hakusita kuonyesha furaha na hisia zake
aliposema " shida ya maji kwetu ni tatizo kubwa na la muda mrefu,
unaenda kuteka maji umbali mrefu ukirudi nyumbani muda wa wanafunzi
kurudi kula unakuwa umetimia na hujaanda chakula na kusababisha watoto
kurudi shule bila mlo wa mchana. Tunawashukuru TANAPA kwa kutuondolea
kero hii".
"Kwa hiki tunachokishuhudia leo cha kukabidhiwa vifaa
hivi tunaahidi kuilinda Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa nguvu zetu zote, kwa
wale waliokuwa wanakula nyamapori na kuiita mchicha tutawasemea bila
woga," aliongeza Bi. Jennifer.
Kijiji cha Tungamalenga ambacho
wananchi wake ndio wanufaika wa mradi huo kiko takribani kilometa 20
kutoka Lango kuu la Hifadhi ya Taifa Ruaha.
No comments:
Post a Comment