Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele
(kulia) akiongoza Kikao cha Tume kilichokutana leo Agosti 17,2023 jijini
Dodoma. Pamoja nae ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa
(Mstaafu), Mhe.Mbarouk Salim Mbarouk.
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiwa katika kikao kilichokutana leo Agosti 17,2023 Jijini Dodoma.
*****
Na Mwandishi wetu, Dodoma.
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa vibali vya kutoa Elimu ya Mpiga Kura
katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Mbarali na Kata sita za
Tanzania Bara kwa asasi tatu za kiraia.
Taarifa ya Tume iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima imesema uamuzi huo umefikiwa baada
ya Tume kukutana katika kikao chake leo Agosti 17,2023 jijini Dodoma.
“Tume
imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia kifungu cha 4C cha sheria ya Taifa
ya Uchaguzi, Sura 343 na kanuni ya 3 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020, inayoipa Tume jukumu la
kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi na
asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kailima
amezitaja asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga
kura na maeneo watakayotoa elimu hiyo kuwa ni Alpha and Omega
Reconciliation and Peace Building (AREPEB), itakayotoa Elimu
Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali katika Jimbo la Mbarali, Umbrella of
Women and Disabled Organisation (UWODO) itakayotoa Elimu Halmashauri ya
Wilaya ya Madaba katika Kata ya Mtyangimbole na Bright Child Development
Tanzania (BRIGHT CHILD), Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika Kata
ya Mwaniko.
Aidha,
Tume imetoa kibali cha utazamaji kwa Asasi ya kiraia ya Bridge
Development Trust Organization (BRIDETO) ambayo iliomba kutazama
uchaguzi mdogo katika Kata ya Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Misungwi na Kata ya Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kailima
amesema katika taarifa hiyo kuwa, Tume imefikia uamuzi huo wa kutoa
kibali hicho kwa kuzingatia kanuni ya 16(5) ya Kanuni ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020
Amesema
katika utekelezaji wa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura, asasi hizo
zitapaswa kuzingatia Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Mwaka 2020
katika kipindi chote cha kutoa elimu hiyo katika uchaguzi mdogo.
Kwa
mujibu wa ratiba ya uchaguzi mdogo iliyotolewa na Tume, uteuzi wa
wagombea katika uchaguzi huo utafanyika Agosti 19, 2023 na Agosti 20
hadi Septemba 18, 2023 kitakuwa ni kipindi cha kampeni kwa vyama vya
siasa na wagombea, na Jumanne ya Septemba 19, 2023 itakuwa ni siku ya
uchaguzi.
"Tume
inatumia fursa hii kuzipongeza asasi zote za kiraia zilizopata kibali
cha kutoa elimu ya mpiga kura na utazamaji wa uchaguzi, na inazikumbusha
asasi hizo kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo
ya Tume katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yao. " alisema
Kailima katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Tume vibali hicho kitatumika kuanzia tarehe Agosti 18, 2023 hadi Septemba 18, 2023.
Thursday, August 17, 2023
NEC YATOA VIBALI KWA TAASISI NA ASASI KUTOA ELIMU NA KUTAZAMA UCHAGUZI MDOGO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment