HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 15, 2023

DKT. YONAZI: SEKTA YA KILIMO KUCHAGIZA PATO LA TAIFA.

 

Na. Mwandishi Wetu
 
SERIKALI imeendelea kutoa kipaumbele katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini kwa kuzingatia umuhimu na tija ya sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi Agosti 15, 2023 wakati akihutubia katika kikao cha Awali cha Wadau kwa ajili ya zoezi la Tathmini ya Nusu Muhula na Uandaaji Mpango wa Utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDFP II) kwa miaka mingine mitano kilichofanyika Jijini Dar es salaam.

Dkt. Yonazi alieleza kuwa sekta ya kilimo ni muhimu kwa Taifa na tegemeo kwa maisha ya wananchi wengi kwani huongoza inaongoza kwa uchangiaji mkubwa katika pato la Taifa, na robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya Nchi.

Aliongeza kuwa sekta ya kilimo imeendelea kuwa chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania ambapo katika mwaka 2021, sekta hiyo ilichangia asilimia 26.1 katika shughuli za kiuchumi katika Pato la Taifa.

Alifafanua kuwa, kilimo kimekuwa na uhusiano na sekta zisizo za kilimo kupitia usafirishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi na uuzaji nje ya nchi pamoja na malighafi kwa viwanda na masoko kwa bidhaa zilizotengenezwa akieleza kuwa hatua hiyo imechagiza ongezeko la bajeti kubwa katika sekta ya kilimo kwa miaka miwili mfululizo.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuyafikia malengo yake ikiwemo Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO).

“Nichukue fursa kulishukuru Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwa kuunga mkono juhudi hizi ambapo wamewezesha kwa kujengea uwezo timu ya wataalam wa ndani itakayoshirikiana na Mshauri Elekezi katika zoezi hili. Timu hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kutoa taarifa na maoni ambayo yatazingatiwa na Mshauri Elekezi kabla ya vikao vya wataalam na viongozi,”alisema Dkt. Yonazi.

Aidha, alishukuru ushiriki wa Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu wataalam wao kushiriki katika kikao hicho muhimu kwa sekta ya kilimo.

“Pia, napenda kulishukuru Shirika la Alliance for Green Revolution in Africa – AGRA kwa kuwezesha Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu zoezi hili la mapitio ya utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili - ASDP II kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza, yaani mwaka 2018 – 2023 na uandaaji wa mpango wa miaka mitano ijayo,”Alishukuru Dkt. Yonazi.

Awali Dkt. Yonazi alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ina dhamana ya uratibu wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili, kwa kutambua umuhimu wa programu hiyo na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji inaratibu zoezi la tathmini ya programu na uandaaji wa mpango wa programu katika kipindi kilichobaki kwa kushirikiana na wadau.

“Katika mapitio ya Mipango na Mikakati mingine, mapitio na uhuishaji wa ASDP II utahusisha uchambuzi wa nyaraka na maandiko mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini. Ni muhimu kila sekta kuhakikisha inatoa takwimu na taarifa za kutosha ili kuwezesha tathmini kuwa na uhalisia pamoja na kuwezesha mpango utakaoandaliwa kutekelezeka kwa ufanisi,”Alieleza.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad