Na Munir Shemweta, WANMM NJOMBE
Serikali imehitimisha rasmi mgogoro wa muda mrefu baina ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini Njombe na wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi katika halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Uamuzi huo unafuatia maridhiano yaliyofikiwa baina ya pande zote za mgogoro baada ya timu iliyoundwa na kuhusisha wawakilishi kutoka kwa wadai na wale wa KKKT, wataalam wa ofisi ya ardhi mkoa na halmashauri, TAKUKURU, Polisi na ofisi ya usalama mkoa kuwasilisha ripoti yake.
Akihitimisha mgogoro huo mkoani Njombe tarehe 9 Agosti 2023, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, katika kuhitimisha mgogoro huo wananchi wanaodai wanatakiwa kupokea viwanja 400 kama kifuta jasho pamoja na urasimishaji wa makazi kwa wale walioingia kwenye eneo lenye mgogoro bila kufuata taratibu.
‘’Pokeeni urasimishaji kwa wale walioingia bila utararubu kama kifuta jasho kwa kuwa mmeingia bila kufuata taratibu’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, Waziri wa Ardhi amelitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisis ya kusini Njombe kuhakikisha lina;inda maeneo yake na kubainisha kuwa, hakuna wakuwalindia maeneo yake na itakapotekea maeneo ya kanisa hilo kuvamiwa basi suala hilo lipelekwe katika vyombo vya sheria na si wizara ya ardhi.
Awali wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi walimueleza Waziri wa Ardhi masikitiko ya kuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu mgogoro huo uliodumu kwa takriban miaka 22 bila kupatiwa ufumbuzi.
Walieleza kuwa, mgogoro huo una sura mbili na kuzitaja kuwa ni maeneo waliyodai kumiliki ndani ya scheme na maeneo ambayo wakati kanisa la KKKT linapima ili kupata hati lilivuka na kuingia kwenye maeneo ya watu binafsi.
Aidha, wananchi hao wametaka kuatambuliwa kama wamiliki wa maeneo hayo na si wavamizi na kutaka kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
Utatuzi wa mgogoro baina ya kanisa la KKKT na wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe umekuwa ukiendelea kufanyika katika ngazi mbalimbali chini ya usimamizi wa Mkuu wa mkoa wa Njombe na kufikia maamuzi kuwa, KKKT itoe viwanja vya kifuta jasho kwa walalamikaji ili kumaliza mgogoro pamoja na kumega eneo la chuo lililojengwa nyumba na walalamikaji ili waendelezaji wabaki na maeneo waliyojenga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini Njombe na wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe Agosti 9, 2023.
Sehemu ya washiriki wa kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini Njombe na wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula Agosti 9, 2023.
Mbunge wa jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika akizungumza kwenye kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini Njombe na wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula Agosti 9, 2023.
Diwani katika halmashauri ya wilaya ya Njombe akitoa maelezo wakati wa kikao cha kutatua mgogoro kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini Njombe na wananchi wa kijiji cha Magoda na mtaa wa Lunyanywi mkoani Njombe kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula Agosti 9, 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
No comments:
Post a Comment