HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 30, 2023

WAFANYABIASHARA RUVUMA WAFUNDISHWA FURSA ZILIZOPO KATIKA SOKO HURU LA AFRIKA

 

Na Albano Midelo,Songea

WAFANYABIASHARA wa Mkoa wa Ruvuma wamejengewa ufahamu kuhusu fursa zilizopo katika Soko huru la Afrika (EfTTA) ili kupata uelewa na kuhamasika kutumia soko huru la Afrika na kuuza bidhaa kutokea
Tanzania.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea yameratibiwa na Taasisi ya Tan Trade iliyopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara,na kufunguliwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Joel Mbewa.

Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo Katibu Tawala amelitaja lengo la mafunzo hayo kuwa ni mikakati ya kutumia fursa za kimasoko zilizopo katika eneo huru la biashara barani Afrika kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Amezitaja faida za mafunzo hayo kwa wafanyabiashara mkoani Ruvuma kuwa ni wafanya biashara kupata uelewa wa kutosha juu ya fursa zinazopatikana katika sekta wanazofanyia kazi na kukua kwa idadi ya bidhaa zinazouzwa katika soko hilo kutokea Tanzania.

Faida nyingine za mafunzo hayo amezitaja kuwa ni kuboresha bidhaa zinazozalishwa ili kukabiliana na ushindani uliopo katika soko huru la Afrika,kuongezeka kwa bidhaa zinazozalishwa na kumiliki soko husika na kupata wanunuzi wa malighafi zilizopo mashambani kutokana na kuwepo kwa soko la kutosha.

“Ni Imani yangu mafunzo haya yatawajengea uelewa mkubwa katika kutumia fursa hizo ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla’’,alisisitiza.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo,Afisa Biashara Mkuu wa Taasisi ya TANTRADE Crispin Luanda amelitaja eneo la Biashara Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) kuwa ndilo eneo kubwa zaidi la biashara huria duniani linaloleta Pamoja nchi 55 za Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya nane za kiuchumi za kikanda ili kuunda soko moja la bara la Afrika.  Hata hivyo amesema Tanzania ni Mwanachama rasmi wa AfCFTA toka mwaka 2021 ikiungana na nchi nyingine za Soko Huru la Afrika.

Amezitaja nchi hizo kuwa ni Ghana, Kenya, Rwanda Chad,Swaziland,Guinea,Mali,Namibia,Afrika ya Kusini, Jibouti, Mauritania, Uganda, Senegal, Kongo DRC,Togo, Misri, Ethiopia, Gambia, Sieraleone, Zimbabwe, Burkinafaso, Garbon, Equatorial Guineana Sao Tome.

Mtaalam huyo kutoka TANTRADE ametoa rai kwa wafanya biashara wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanatangaza biashara zao kwenye
maonesho ya kimataifa kama Sabasaba ili kujitangaza kimataifa.

Awali wafanyabiashara hao waliipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara,majini na angani katika Mkoa wa Ruvuma hali ambayo inarahisisha utendaji kazi katika biashara zao.

Hata hivyo walizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni Pamoja na kuchelewa malipo ya bidhaa zao kama mazao,ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu biashara na changamoto ya leseni ya biashara.

Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma na Taasisi ya TANTRADE imeahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi na kulifikia soko huru la Afrika kama ilivyo kwa wafanyabiashara katika nchi nyingine.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Joel Mbewa akifungua mafunzo ya kuwajengea ufahamu wafanya biashara wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu fursa zilizopo katika soko huru la Afrika yaliyofanyika kwenye uk,umbi wa Manispaa ya Songea.
Afisa Biashara Mkuu kutoka Taasisi ya TANTRADE iliyopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara akizungumza baada ya kutoaa  mafunzo ya kuwajengea ufahamu wafanya biashara wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu fursa zilizopo katika soko huru la Afrika yaliyofanyika kwenye uk,umbi.



Baadhi ya wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka mkoani Ruvuma mafunzo ya kuwajengea ufahamu wafanya biashara wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu fursa zilizopo katika soko huru la Afrika yaliyofanyika kwenye uk,umbi wa Manispaa ya Songea.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad