NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MAKAMU
wa Rais Dk. Philip Mpango, amekiri kuvutiwa na uwezeshaji kwa wabunifu
wazawa unaofanywa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), aliyoitaka
kuhakikisha inaenda mbali zaidi kwa kukifanyia kazi kilio chao cha
kutaka kuwapatia Mafunzo ya Mifumo ya Kielektroniki, Ili kuwaongezea
ufanisi katika bunifu zao.
Dk. Mpango ameyasema hayo Jumanne ya
Agosti 1, alipotembelea Banda la COSTECH, wakati wa uzinduzi wa Maonesho
ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane (Tanzania International
Agricultural Trade Show 2023), kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini
Mbeya, ambako alikuwa mgeni rasmi na kuyazindua kwa kuitaka Wizara na
mamlaka husika kutoa tuzo na zawadi za fedha kwa wabunifu wazawa
Akiwa
COSTECH, Dk Mpango alivutiwa zaidi na mbunifu Adam Kinyekile 'Street
Engineer,' aliyewezeshwa na tume hiyo kubuni Mashine Maalum ya kuchakata
mazao, ikiwemo kupukuchua nafaka, kusaga nafaka zisizo na mafuta,
kuvuta maji ya kumwagilia mazao na kuyabeba mazao hayo baada ya kuvunwa
mashambani kupeleka ghalani, ambapo alipokuwa akitoa hotuba ya jumla ya
uzinduzi rasmi mbele ya wahudhuriaji, alirudia kuimwagia sifa COSTECH,
kwa uwezeshaji kwa kijana huyo na wenzake.
Dk. Mpango aliipongeza
COSTECH kwa kuthamini bunifu za vijana wa Kitanzania, ambako
alishuhudia bandani hapo bidhaa za Kilimo, Ufugaji na Ufundi kutoka kwa
vijana walioshiriki Mafunzo Atamizi, kisha akasikiliza kero na
changamoto zao na kuahidi kuzifanyia kazi, huku akiitaka tume hiyo
kuwaongezea vijana wabunifu Mafunzo ya Kielektroniki, kama alivyoomba
Kinyekile Ili kuongeza ufanisi wa bunifu zao, kwani liko ndani ya uwezo
wao.
Akizungumzia ubunifu wa Mashine hiyo, Dk. Mpango alimpongeza
Adam kwa ubunifu huo, lakini akamshauri kutenganisha kazi za mashine
zitokanazo na ubunifu wake Ili kupunguza gharama yake ambayo inaweza
kuwa ghali kwa mkulima wa kawaida kuimudu na kubainisha kuwa
itakapotenganishwa na kila moja ikafanya kazi tofauti, zitashuka bei na
kuwapunguzia mzigo wakulima.
"Kwanza nikupongeze kwa ubunifu huu,
tunahitaji vijana wa Kitanzania wabunifu kama wewe. Nitumie fursa hii
kuwaomba vijana wote wabunifu wenye uwezo wa kutengeneza Mashine za
kuchakata mazao kama hizi wafanye hivyo, COSTECH ipo hapa kwa ajili ya
kuwasaidia kama walivyokusaidia wewe na vijana wenzako.
"Mamilioni
uliyopewa na COSTECH ni mengi, sio haba kwa mkulima kuyamudu, kwahiyo
nashauri utenganishe mashine hizi Ili kupunguza gharama kwa mnunuzi
ambaye ni mkulima," alisema Dk. Mpango na kuitaka tume hiyo kuwasaidia
wabunifu hao Ili kubuni mashine tofauti tofauti zinazotumia Mifumo ya
Kielektroniki kama alivyoomba Adam.
Awali, Afisa Uratibu na
Utafiti wa COSTECH, Dk. Deogracious Protas, alimueleza Makamu wa Rais
kuwa, licha ya Sh. Mil. 99 walizotoa kwa Adam, tume yake imesaidia
Mafunzo Atamizi ya vijana wanaojihusisha na Kilimo, Uvuvi na Ufugaji,
sambamba na kutoa mitambo yenye thamani ya Sh. Mil. 400 kuboresha
usindikaji kwa Kituo cha Utafiti cha TARI Makutupola kilicho chini ya
JKT Makutupola, ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa zabibu
inayosindikwa hapo kuzalisha mvinyo bora.
Dk. Protas alimuahidi
Makamu wa Rais kuwa tume yake italifanyia kazi agizo lake la kutaka
iwasaidie wabunifu wazawa kupata Mafunzo ya Kielektroniki Ili
kuwawezesha kubuni kwa faida bidhaa zenye mifumo hiyo kwa ustawi wa
wakulima na Sekta ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kwa ujumla, Ili iweze
kutoa mchango kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza mchango wa Sekta
hiyo katika kukuza Pato la Taifa.
Makamu wa Rais akipata maelezo kutoka kwa Afisa uratibu na utafiti wa COSTECH, Dk Deogracious Protas wakati alipotembelea Banda kwenye maonyesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya . Kulia Mbunifu wa Mashine ya kuchakata mazao. Adam Kinyekile.
Makamu wa Rais, Dk Philp Mpango akimsikiliza Mtafiti wa Mifugo,Mark Mark wakati akitoa maelezo ya Dawa mbalimbali alipotembelea Banda la Tume ya Sayansi na Teknolojia COSTECH kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
No comments:
Post a Comment