BENKI ya Mwanga Hakika Limited imepata faida ya shilingi bilioni 4.06 kabla ya kodi kwa mwaka ulioishia December, 2022, ikilinganishwa na faia ya shilingi milioni 871.78 mwaka wa 2021.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa benki hiyo Bw Hussein Abdalla Chomete, wakati akisoma taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, kweney mkutano mkuu wa tatu wa wanahisa, uliofanyika Mwanga, mkoani Kilimanjaro, mwishoni mwa wiki.
“Ongezeko hili la faida na sawa na asilimia 365, ambapo ukuaji huu umesababishwa na ongezeko la biashara ya benki yetu ya Mwanga Hakika uliopelekea kukua kwa amana za wateja”, alisema.
Bw Chomete aliendelea kusema kuwa amana za benki hiyo ziliongezeka kwa asilimia 52 kutoka shilingi bilioni 52.72 mwaka wa 2021 na kufikia shilingi bilioni 86.06.
“Mtaji halisi wa benki pia uliongezeka kutoka shilingi bilioni 16.03 mwaka 2021 na kufikia shilingi bilioni 17.11 kwa mwaka wa 2022; mafanikio haya yametokana na wanahisa kuongeza hisa zao”, alisema.
Aidha alisema thamani ya mikopo iliyotolewa iliongezeka kutoka shilingi bilioni 48.55 mwaka wa 2021 na kufikia shilingi bilioni 80.69 kwa mwaka wa 2022, jambo amalo alisema limetokana na ukuaji wa kitabu cha mikopo kwa wateja kwa mwaka 2022.
Bw Chomete aliendelea kusema kuwa Bodi ya wakurugenzi imeendelea na mipango itakayohakikisha wanahisa wanapata faida na kutoa gawio kwa wanahisa wake ambapo alisema hiyo ni sehemu ya Dira ya benki hiyo.
Katika taarifa yake Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Bw Jaghjit Singh imeendela na mpango mkakati wa 2021-2025 ulioandaliwa na taasisi hiyo kwa kuweka msisitizo katika kuboresha huduma za wateja na kupanua wigo wa biashara.
“Katika mkakati huo mpya, benki inaendelea kujikita katika kuimarisha mifumo mbalimbali ya kiteknolojia na kidijitali ili kuweza kuwafikia wateja wengi Zaidi na kutoa ushindani katiak soko la ndani na baadae la kimataifa”, alisema.
Bw Singh aliendelea kusema kuwa faida ya benki hiyo inatarajiwa kuongezeka na kufikia shilingi bilioni 9 kwa mwaka wa 2023 na kwamba muelekeo ni mzuri kutokana na ukweli kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, tayari faida kabla ya kodi ilifikia shilingi bilioni 4.24.
“Katika kipindi hicho tunatarajia kutoa mikopo yeney thamani ya shilingi bilioni 127.40 kutoka mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 80.69 iliyotolewa mwaka wa 2022; hdai kufikia Juni 30, mwaka huu, tayari tulishatoa mikopo yenye thamani ya bilioni 102.81”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa amana za benki hiyo zinatarajiwa kuongezeka na kufikia shilingi bilioni 132 ikilinganishwa na thamani ya shilingi bilioni 80 zilizokuweko hadi kufikia December, 2022.
Aliongeza, “Kwa mwaka wa 2023, benki imeendelea kuimarisha mtaji wake kupitia faida, kwa kuendelea kufanya biashara Zaidi na kuendelea kukidhi vigezo vya Benki Kuu ya Tanzania ambapo kufikia Juni, 2023, mtaji wa benki kisheria ulikuwa ni shilingi bilioni 22.18 hii ikiwa ni juu ya ukomo wa chini wa Benki kuu wa mtaji wa shilingi bilioni 15 kwa benki ya kibiashara”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa MHB Mhandisi Ridhuan Mringo, alisema malengo ya baadaye ya benki hiyo ni kuhakikisha inakuwa moja ya benki tano muhimu hapa nchini ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo.
“Katika kuhakikisha tunafikia azma hiyo, Bodi na menejimenti ya benki imeendelea kuboresha huduma mbalimbali chini ya kauli mbiu mpya ya benki isemayo Tunatafsiri Kesho Yako leo…Defining Tomorrow Today”, alisema.
Aliongeza, “Huduma zilizoboreshwa ni pamoja na zile za kiteknolojia ambapo sasa wateja wanaweza kuzipata kwa kutumia simu za kiganjani, ikwemo malipo ya Serikali, kununua umeme pamoja na mikopo ya kidijitali, kwa kutaja machache tu”.
Katika mkutano huo mkuu, wanachama waliidhinisha ya kuwa wakurugenzi wa Bodi walioteuliwa mwaka wa 2022, waendelee kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja ujao.
Wajumbe wa hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Eng Rithuan Mringo, Makamu Mwenyekiti Bw Raymond Thadeus, ambapo wajumbe ni pamoja na Bi Zuhra Ally, Eng John Msemo, Eng Thomas Uiso, Wakili Gilder Kibola, Bi Anna Mushi na Bi Sia Njau, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Singh anakuwa mjumbe wa Bodi hiyo kutokana na wadhifa wake kama mtendaji mkuu wa benki hiyo ili kukidhi idadi ya wajumbe wa Bodi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mwanga Hakika Bank, Mhandisi Ridhuan Mringo akizungumza na wanahisa wa Bemki hiyo wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka kuhusu maendeleo ya Benki hiyo.Kushoto ni Katibu wa Benki, Nancy Kissanga na Mhandisi John Msemo. Benki hiyo imeropoti faida ya 4.06 Bilioni kwa mwaka 2022 sawa na asilimia 365.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Mwanga Hakika, Mhandisi Ridhuan Mringo akisoma taarifa ya Benki kwa Wanahisa wa benki hiyo wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika Wilayani Mwanga, Kilimanjaro. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji,Jagjit Singh, Mkuu wa Idara ya Fedha wa Benki, Chomete Hussein na Katibu wa Benki, Nancy Kissanga pamoja na wajumbe mbalimbali.
Mkuu wa Idara ya Fedha wa Benki ya Mwanga Hakika Chomete Hussein (katikati) akitoa taarifa ya fedha kwa wanahisa wa benki hiyo katika Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyoka Mwanga Kilimanjaro.Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Jagjit Singh na Katibu wa Benki, Nancy Kissanga (kushoto).
No comments:
Post a Comment