HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 12, 2023

Watoto 11,000 hadi 14,000 Huzaliwa na Ugonjwa wa Selimundu kwa mwaka, Serikali Yazindua mwongozo wa Matibabu

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu aliyeshika jarida rasmi la Selimundu la Lancet akionesha kwa wanakongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu akiwa na viongozi wa afya wakizindua jarida rasmi la Selimundu la Lancet jijini Dar es Salaam leo Julai 12, 2023 wakati wa kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) la kujadili mbinu ambazo zitaweza kupunguza tatizo la ugonjwa wa selimundu hapa nchini.

SERIKALI imesema takribani watoto 11,000 hadi 14,000 wanazaliwa na ugonjwa wa Selimundu kwa mwaka nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tano ulimwenguni kwa wagonjwa wengi.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo Julai 12,2023 wakati akizungumza katika uzinduzi wa kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) la kujadili mbinu ambazo zitaweza kupunguza tatizo la ugonjwa wa selimundu pamoja na uzinduzi wa jarida rasmi la Selimundu la Lancet. Amesema  asilimia saba ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ni watoto chini ya miaka mitano.

Pia Serikali imezindua muongozo wa matibabu ya selimundu nchini unaoainisha hatua za kufanya matibabu, utoaji wa dawa ili kupunguza tatizo hilo na kufanya utambuzi wa watoto wachanga wanapozaliwa.

Prof. Nagu  amesema muongozo huo unaelekeza kufanyika vipimo vya vinasaba kwa wachumba kabla ya kuoana ili kupunguza uwezekano wa kupata watoto wenye selimundu.

Ameeleza kuwa muongozo huo unalenga kufanya utambuzi kwa watoto zaidi ya milioni mbili wanaozaliwa kila mwaka na kuhakikisha wanapata matibabu mapema ikiwemo chanjo, dawa za antibiotiki ili wasipate changamoto zitokanazo na selimundu.

Pia amesema muongozo huo utahakikisha kuwa watoa huduma wao wanajua namna bora ya kuwahudumia kwa usahihi wenye matatizo hayo hivyo, kuboresha matibabu ya watoto hao.

"Serikali inafanya jitihada kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuwatambua watoto mapema katika hospitali zote saba ikiwemo ya taifa, Kanda na Rufaa za Mikoa ili kuhakikisha matibabu ya watoto yanakuwa mazuri na bora," ameeleza Prof. Nagu.

Akizungumzia kuhusiana na dawa za ugonjwa huo Prof.Nagu, amesema watahakikisha dawa ambayo inabadilisha maisha ya watoto wenye selimundu ya Hydroxyurea inapatikana hapa Tanzania kwa kutengenezwa nchini.

Ameeleza kuwa dawa hiyo ikitengenezwa nchini itapunguza gharama na kuhakikisha inakuwepo muda wote badala ya kusubiri itoke nje ya nchi.

Pia amesema kwa sasa Bohari ya Dawa (MSD) inatoa dawa hiyo muda wote na kwamba serikali imetenga fedha kwajili ya kununua dawa hiyo ambayo ipo kwenye miongozo ya dawa na kusaidia hospitali na vituo vya afya kuagiza.

"Nipende kuwakumbusha waganga wafawidhi wa hospitali kuhakikisha dawa hii inapatikana kwenye vituo vyote vya afya kwani ipo na inapatikana wakati wote." amesema

Kuhusu upandikizaji uloto, Profesa Nagu amesema matibabu hayo hupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo na hupatikana katika Hospitali za Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema gharama za matibabu hayo ni makubwa kwa sababu inahitaji kufanyika vipimo vingi na vikubwa ambavyo hupatikana ndani na nje ya nchi.

Amesema dawa ambazo zinahitajika kupewa watoto baada ya kupata matibabu hayo ni "Katika bajeti ya mwaka 2023/24 serikali imetenga Sh bilioni tano kwa ajili ya upandikizaji na kwa sehemu kubwa itatumika kupandikiza uloto na figo," alisema.

Amesisitiza kuwa wako tayari kufanya kazi na watafiti Kuhakikisha zinajibu matatizo ya Watanzania.

Akizungumzia kuhusiana na tafiti, Kaimu Makamu Mkuu wa chuo cha MUHAS, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema kuwa tafiti walizofanya zimechangia maboresho ya huduma za ugonjwa wa selimundu nchini ikiwemo upandikizaji wa uloto na kuanza kwa uchunguzi wa watoto wachanga.

Amesema katika kongamano hilo wamewasilisha utafiti uliofanyika kuhusu ubadilishaji wa vinasaba vyenye selimundu kwa watoto wachanga ili kukabiliana na ugonjwa huo.

"Utafiti huu unalenga wale watoto watakaozaliwa na vinasaba vya selimundu wataondolewa vinasaba hivyo na kuwekewa vinasaba visivyo na ugonjwa kwenye damu zao hii itasaidia kuondoa kabisa ugonjwa huu." amesema Prof. Kamuhabwa
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam leo Julai 12, 2023.
Kaimu Makamu Mkuu wa chuo cha MUHAS, Profesa Apolinary Kamuhabwa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam leo Julai 12, 2023.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu akionesha tuzo.

Picha ya pamoja.



Baadhi ya wadau wa wakiwa katika uzinduzi wa kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) la kujadili mbinu ambazo zitaweza kupunguza tatizo la ugonjwa wa selimundu pamoja na uzinduzi wa jarida rasmi la Selimundu la Lancet.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad