HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 21, 2023

Waendesha Pikipiki Dar Kuwaburuza Mahakamani Wanaotumia Jina Lao Vibaya.

 



Chama Cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam (CMPD) kimeelezea dhamira ya kufungua kesi dhidi ya taasisi inayofamika kama Shirikisho la Vyama vya Pikipiki ikiwa taasisi hiyo itashindwa kuomba radhi kwa chama hicho ndani ya saa 12 kwa kosa la kutumia jina la chama hicho kama mmoja wa wanachama wake wakati si kweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hii leo, Mwenyekiti wa CMPD Bw Michael Massawe alisema chama hicho hakitambui uwepo wa ‘shirikisho’ hilo kwasababu hakijawahi kushiriki wala kuhusishwa kwenye uanzilishishi wala uanachama wa ‘shirikisho’ hilo.

‘’Kwa watu hao kujitambulisha kama wanafanya uangalizi wa CMPD, ni upotoshaji wenye nia ovu ya kuleta mkanganyiko na hasara kwa wanachama wetu wa CMPD. Ifahamike kwamba tayari tumepokea taarifa nyingi kutoka kwa wanachama wetu ambao wamekuwa wakijikuta kwenye sintofahamu kutokana na taarifa zinazotolewa na hawa ‘shirikisho’ huku wakiwataja wanachama wetu kama sehemu ya wahusika wa mipango yao wakati si kweli,’’ alibainisha.

Taarifa hiyo ya CMPD imekuja siku chache tu baada ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Pikipiki kutoa taarifa kupitia moja televisheni hapa nchini kuhusiana na ujio wa kongamano la elimu ya usalama barabarani huku wakikitaja chama hicho cha CMPD kuwa miongoni mwa vyama vilivyopo ndani ya shirikisho hilo.

‘’Kitendo cha hawa ‘shirikisho’ kututambulisha kama wanachama wao na kuthibitisha ushiriki wetu kwenye matukio yao mbali na kuleta mkanganyiko kwa wanachama wetu pia wanatuingiza kwenye migongano na wadau wetu mbalimbali ambao tayari tupo nao kwenye makubaliano ya kiutedaji yanayoongozwa kisheria. Kupitia wadau hawa tayari tuna kalenda ya matukio yetu muhimu sasa wanaposikia tunahusishwa na matukio mengine bila wao kuwa na taarifa inawasababishia sintofahamu na kutishia makubaliano yetu,’’ alibainisha.

Katika kuthibitisha hatua hiyo, Bw Massawe alisema tayari chama hicho kimandaa ‘notisi’ ya kisheria kupitia mwanasheria wa chama hicho Kampuni ya Uwakili ya Msando Law Office kikilitaka shirikisho hilo kuwaomba radhi wanachama wa CMPD kutumia vibaya jina la chama chao bila uwepo wa makubaliano ya kisheria.

‘’Zingatia kwamba, tumepokea maelekezo kutoka kwa mteja wetu kukuelekeza ndani ya masaaa 12 utoe taarifa kuomba radhi Umma na wanachama wa CMPD kwa kuwapotosha kuhusu ushiriki wa CMPD kwenye ‘shirikisho’ hilo, na kuweka taarifa sawa kwamba CMPD hawafanyi kazi chini ya ‘shirikisho’ kama ulivyotangaza katika kituo cha televisheni cha Clouds.’’’ Ilisomeka sehemu ya ‘notisi’’ hiyo na kuongeza:

‘’Iwapo masaa hayo yatapika bila kutolewa kwa tamko hilo, shauri litafunguliwa mahakamani dhidi yako na utalazimika kulipa gharama zote za kesi na usumbufu.’’

Tangu usajili wake hadi sasa, CMPD imeweza kupata wanachama zaidi ya 40,000 (elfu Arobaini) wakiwa chini ya vituo 1,600 vilivyorasimishwa na Serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa Wa Dar es saalam sambamba na wataalam kutoka ofisi za Halmashauri zote za Dar es Salaam.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad