HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 18, 2023

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AKEMEA UNYANYAPAA KWA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI -WAVIU

 

Na. Mwandishi Wetu

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe.Ummy Nderiananga amekemea vitendo vya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (WAVIU) na kuiasa jamii kuendelea kuwajali na kuwajumuisha katika shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Ametoa kauli hiyo Julai 17, 2023 wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa shughuli za WAVIU, katika Konga za watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI katika Wilaya za Moshi ambapo alifanikiwa kuzungumza nao na kukagua shughuli za uzalishaji wanazofanya.

Mhe. Ummy aliitaka jamii kutowanyanyapaa watu wanaoishi na VVU na kuwashirikisha katika shughuli za kijamii na za uzalishaji mali, huku akieleza kuwa ni watu muhimu na wenye mchango chanya kwenye kujiletea maendeleo yao na Taifa.

“Tuache unyanyapaa kwa WAVIU, tusiwabague, tuishi nao kama watu wengine, tuwapende na tujenge tabia ya kuwathamini, kujali na kuwajumuisha katika masuala mbalimbali ya uzalishaji huku tukiunga mkono jitihada za Serikali za kupinga unyanyapaa huo,”alisema Mhe. Nderiananga

Aidha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha vijana wanaoishi na maambukizi ya VVU kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Halmashauri zao kujiongezea mitaji na kujikwamua kiuchumi kwa kuwa na vikundi vya uzalishaji mali huku akiwakumbusha kuendelea kujali afya zao kwa kutumia dawa za kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI.

“Kwa tunaoendelea kutumia dawa za ARVs niwasihii sana tusiache wala kuzipuuza, tumeona zinasaidia wengi na nitoe rai kwa kila anayegundulika na maambuki ya Virusi vya UKIMWI, basi ni vyema aanze dawa hizi mapema ili aweze kuishi katika hali bora zaidi,”alisisitiza

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu alitumia nafasi yake kukumbusha vijana kujitokeza kwa wingi kupima na kujua hali zao huku akiwakumbusha kuwa ndilo kundi linaloathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU na UKIMWI.

“Pamoja na jitihada za Serikali katika mapambano haya, bado vijana mnakazi kubwa ya kuendelea kujilinda kwa njia zote muhimu zinazoshauriwa na wataalam wa afya huku mkikumbuka kuachana na tabia zote hatarishi zinazoweza kuchochea mtu kupata maambukizi haya,”alieleza Mhe. Babu.

Awali akitoa taarifa fupi ya hali ya UKIMWI kwa Mkoa wa Kilimanjaro, mratibu wa masuala ya UKIMWI Mtambuka Bi. Jesca Nyaki alisema kiwango cha maambukizi kimeendelea kupungua kwa kuzingatia takwimu zilizopo, ambapo kimepungua kutoka asilimia 7.3 kwa mwaka 2003/24 hadi asilimia 2.6 mwaka 2016/17.

Mwenyekiti wa Konga ya Moshi Vijijini Bw. Baltazar Minishi ameishukuru Serikali kwa uwezeshwaji na huduma za afya wanazozipata kutoka serikalini kwani zimeboreshwa na kuleta tija kwa WAVIU.

Aidha Bw.Baltazar Munishi ameomba serikali iwapatie Ofisi kwa ajili ya Utekelezaji wa shughuli zao,ambapo Mkurugenzi wa Halmashuri ya Moshi Bw. Shadrack Muhagama ameahidi kutatua changamoto hiyo na kuwapatia Ofisi kwa kadri itakavyowezekana.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Ummy Nderiananga akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu kuhusu masuala ya UKIMWI katika mkoa wake, wakati alipomtembelea ofisi kwake Kilimanjaro Julai 17, 2023.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu akizungumza kuhusu masuala ya UKIMWI katika mkoa wake wakati wa ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipofanya ziara mkoani humo.Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe.Ummy Nderiananga akikagua shughuli za uzalishaji zinazofanywa na konga za watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kutoka Wilaya ya Moshi Mjini alipowatembelea ikiwa ni sehemu ya ziara yake kukagua shughuli zao.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Ummy Nderiananga akizungumza na wanachama kutoka kwenye Konga za watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, Wilaya ya Moshi Mjini na Vijijini alipowatembelea.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Ummy Nderiananga akipokelewa na baadhi ya wanachama wa Konga za WAVIU Wilaya ya Moshi Mjini na Vijijini.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Ummy Nderiananga akiwa katika picha ya pamoja na WAVIU kutoka Konga ya Wilaya ya Moshi Mjini na Vijijini mara baada ya kukagua shughuli za uzalishaji mali wanazozifanya Julai 17, 2023.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Ummy Nderiananga akimsikiliza kiongozi wa Konga ya ARIEL Group Bw. Robert William wakati akikagua baadhi ya bidhaa wanazotengeneza katika konga yao, ikiwemo matofali wakati wa ziara yake alipokutana na kuzungumza na wanachama kutoka Konga za watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Moshi.


(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU NA TACAIDS)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad