HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 13, 2023

DKT. MOLLEL AISHUKURU JUMUIYA YA MARIDHIANO UJENZI WA ZAHANATI NAKWENI.

 

 

Na WAF- Simanjiro 

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameishukuru Jumuiya ya maridhiano nchini na Taasisi ya All for His Glory kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kusogeza huduma kwa wananchi kwa kumalizia zahanati iliyoanza kujengwa na wananchi wa kijiji cha Nakweni kata ya Shambarai Mkoa wa Simanjiro.

Dkt. Mollel amesema hayo alipofanya ziara ya kukagua na kupokea jengo la zahanati kutoka Jumuiya ya maridhiano na Shirika la All for his Glory ambalo licha ya kushiriki katika ujenzi wa zahanati hiyo wamejenga nyumba kwa ajili ya kuwapangisha watumishi wa zahanati kwa gharama nafuu na kuchimba visima vya maji kwa ajili ya kuhudumia zahanati hiyo na matumizi ya wananchi.

Amesema, Katika Mkoa  wa Manyara Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia imeleta zaidi ya shilingi Bilioni 32 za ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi katika eneo la Afya, huku katika Wilaya ya Simanjiro ikiletwa Bilion 4.9.

Aidha,  Dkt. Mollel amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuleta dawa na vifaa tiba pindi zahanati hiyo itapokuwa tayari kuanza kutoa huduma ili wananchi wanufaike na huduma hizo ambazo walikuwa wakizipata umbali wa zaidi ya Km 11 kutoka kijiji hicho. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro Mhe. Christopher Ole Sendeka amemshukuru Katibu wa Jumuiya ya maridhiano na kiongozi wa Taasisi ya  "All for his Glory" Mch. Maasa Ole Gabriel kwa kuunga mkono jitihada za Chama cha Mapinduzi kwa kumalizia zahanati ya Nakweni pamoja na kuchimba visima vya maji vitatu katika kata hiyo na kupunguza changamoto ya maji kwa wananchi. 

Amesema, ili kuunga mkono jitihada za Chama cha Mapinduzi na Serikali, kama Mbunge ameweka Milioni 7 ili kumalizia maeneo yote yaliyobaki, huku akisisitiza atahakikisha ujenzi wa kichomea taka na choo unafanyika na kumalizika ndani ya wakati ili wananchi wa kijiji hicho wanufaike na huduma hizo. 

Nae, Katibu wa Jumuiya ya maridhiano na kiongozi wa Taasisi ya "All for his Glory " Mch. Maasa Ole Gabriel amesema Jumuiya na Taasisi hiyo vitaendelea kushirikiana na Serikali kuwahudumia wananchi wenye uhitaji wa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za maji na afya.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad