HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 17, 2023

Wabunifu 100 wahitimu mafunzo ya Imbeju

Dar es Salaam. Tarehe 16 Juni 2023: Wabunifu 100 kati 196 waliochaguliwa kwenye programu ya Imbeju wamehitimu mafunzo ya wiki moja yaliyotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na COSTECH na Tume ya TEHAMA. Wahitimu hao ni wa awamu ya kwanza ili kupisha nafasi kwa kundi la pili litakalokuwa na wabunifu 96 watakaojengewa uwezo wa namna ya kusimamia fedha, ujasirimali, hati miliki na namna ya kupata masoko ya bidhaa au huduma wanazozitoa.

“Ilikuwa ni wiki nzuri sana kwetu. Wazoefu katika biashara na ujasiriamali wametufahamisha kuhusumambo ya kuzingatia na vile vya kuepuka kufanya. Kwa kifupi, wametusafishia njia ya kupita kuelekea kutimiza ndoto zetu,” amesema Janeth.
Akitoa neno la shukran kwa niaba ya washiriki wenzake, Janeth Lwena ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa kambi hii ya mafunzo kwani imekuwa ya msaada mkubwa kwao na kusisitiza kuwa ikiwezeakana, idadi ya washiriki iongezwe ili mchango wake uwaguse wengi.

“Tumepata maarifa na nafasi ya kuuliza maswali kwa wawezeshaji walio kuwa nasi hapa kwa wiki nzima. Naamini maarifa tuliyoyapata hapa yatakuwa namchango mkubwa kwenye uendeshaji na usimamizi wa kampuni zetu,” amesema Janeth, mwanzilishi wa kampuni ya Orionpax inayotoa programu za kompyuta nchini.
Akifunga mafunzo hayo na kutoa vyeti kwa washiriki, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amewapongeza wabunifu hao kwa uvumilivu waliouonyesha kwa muda wote wa mafunzo.

“Uvumilivu ni kitu muhimu sana kwenye ujasiriamali. Nawapongeza kwa jinsi mlivyotoa ushirikiano na napenda mfahamu kwamba tutaendelea kuwa nanyi katika hatua zinazofuata zitakazowasaidia kupata mentors (washauri) hata masoko ya bidhaa au huduma zenu,” amesema Tully.

Programu ya Imbeju ilizinduliwa Machi 12 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kwa mwezi mzima, CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Tume ya TEHAMA (ICTC) ilipokea maombi kutoka kwa wabunifu 709 ambayo yalipochujwa yalibaki 196 yaliyokidhi vigezo.
Wote waliowasilisha maombi yao, Tully amesema kuna utaratibu wa kuwawezesha kwa kurekebisha kasoro zilizokuwamo kwenye maombi yao.

“Hii ni fursa itakayomgusa kila mmoja. Tungependa kuwawezesha wabunifu wengi kadri iwezekanavyo.  Nawaomba nanyi mkawe mabalozi wazuri wa programu hii ili mwakani tutakapotangaza kupokea maombi, wabunifu wengi wajitokeze na kunufaika,” amesema Tully.

Mafunzo hayo yalifunguliwa Jumatatu ya wiki hii na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliyewapongeza washiriki na kuwasisitiza kuwa ubunifu wao wa kipekee, shauku yao isiyoyumba, na jitihada zao katika ujasiriamali zimewaweka mbele ya kundi kubwa la washiriki waliowasilisha maombi yao hivyo kuwa sehemu ya fursa hii.
“Tunapoianza kambi hii ya mafunzo, ni wakati muhimu katika safari yenu ya ujasiriamali kwani mtapata fursa ya kuboresha bidhaa na huduma zenu, mikakati na kupata ujuzi muhimu unaohitajika ili kuwawezesha kufanikiwa katika hatua hii ya mwanzo katika uendeshaji wa biashara.

Niwasihi kujifunza kwa umakini mkubwa ili kutumia mafunzo na uzoefu mtakaoupata kuboresha biashara zenu. Kumbukeni kuwa maarifa ni nguvu na kwa kujijengea ufahamu na ujuzi sahihi, mtakuwa tayari kukabiliana na changamoto na kuchukua fursa nyingi zilizopo mbele yenu. Na hapo ndipo mafanikio ya programu hii yatakapoonekana,” alisema Nsekela.



 
 



 



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad