HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 19, 2023

CHANGAMOTO ULIPAJI FIDIA KWA WANAOVAMIWA NA TEMBO KONDOA YATUA KWA KATIBU MKUU CCM

 

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV-Kondoa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amemuelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii kuangalia namna ya kutatua changamoto ya ulipaji fidia kwa wananchi ambao wameathiriwa na wanyama pori wakiwemo tembo ambao katika maeneo mengi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi wamekuwa wakilalamika kucheleweshwa kwa fidia pamoja na malipo kidogo.

Chongolo ameyasema hayo leo Juni 19,2023 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Itaswi iliyopo Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma baada ya kutembele Shina Namba Sita ambalo liko nyumbani kwa Balozi Msafiri Antony.

Akiwa katika kata hiyo Chongolo amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kuvamiwa na tembo wa hifadhi ya pori la Akiba Mkungunero na hivyo kuharibiwa mali na mazao yao lakini pia wamekuwa wakicheleweshewa malipo ya fidia .

Kutokana na malalamiko hayo , Chongolo amesema ni kweli tembo wamekuwa wengi kwasababu ya umakini unaofanywa na watu wa uhifadhi lakini suala la fidia hawajaridhika nalo , hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kondoa kuandika orodha ya wananchi wote ambao wameathiriwa na tembo na atakapoondoka Dodoma awe ameipata orodha hiyo.

“Naomba nipate orodha hiyo halafu nione huyo mtu anayekwamisha fidia ili nikapambane naye mbele ya safari.Msiwe na wasiwasi na mtaona matokeo ya utekelezaji , msiniamini sasa ila mniamini fedha zitakapokuja.Lakini suala la pili ni ukubwa wa fidia , mtu ana heka 10 mwingine ana heka mbili wewe roho mbaya ya nini.

“Kwanini usiandike fidia ya kweli ya mtu wa heka 10 , na mtu wa heka mbili basi heka mbili, fedha sio zako , athari sio zako wewe uchungu wa kitu kisicho chako unatoka wapi? Kwanini tunabeba roho mbaya, wewe unamshahara mwisho wa mwezi lakini unaanza kuhangaika na kumuonea hata huyu mwenye haki yake ambayo amehangaika kulima anachotaka ni fidia .

“Tuachane na tabia za ubinafsi na roho mbaya tutengeneze mazingira ya kutenda haki, mtu mwenye heka 10 apate fidia yake ya heka 10 na mwenye heka 30 apate cha heka 30.Tubadilike na mimi hili jambo nalichukulia kwa uzito mkubwa, kila unakoenda ambako wananchi wanapakana na hifadhi changamoto ni kubwa hatuwezi kwenda namna hii,”amesema.

Amesisitiza atazungumza na wahusika akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii na atampa orodha ili aishughulikie wananchi wapate fidia wanazostahili huku akifafanua Waziri hawezi kuchelewa katika kushughulikia changamoto hiyo.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chiongolo akitoa maelekezo mbele ya Afisa Muhifadhi na Kamanda wa pori la Akiba Mkungunero Floravick Kalambo kuhusu malalamiko ya wananchi  kuvamiwa na tembo wa hifadhi ya pori la Akiba Mkungunero,uhalibifu wa mali na mazao yao ikiwemo na suala la fidia kwa waathirika

Afisa Muhifadhi na Kamanda wa pori la Akiba Mkungunero Floravick Kalambo akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi kuhusu kuvamiwa na tembo wa hifadhi ya pori la Akiba Mkungunero na hivyo kuharibiwa mali na mazao yao,mbele ya Katibu Mkuu wa CCM pamoja na Wananchi wa Kata ya Itaswi iliyopo Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma








Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini ambaye pia ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akieleza changamoto mbalimbali zinazowakera Wananchi mbele ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ili kuzipatia majibu na ufumbuzi wakati wa kikao cha shina Kata ya Itaswi.




Wananchi mbalimbali wakifautilia yaliyokuwa yakijiri kwenye kikao








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad