HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 4, 2023

VIONGOZI WATAKIWA KUSIMAMIA KWA WELEDI UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA KILIMO NA UVUVI

 

 



Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akizungumza, katika ufunguzi wa warsha ya Siku mbili ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri. Dodoma Leo



Picha ikionesha baadhi ya watendaji wa Mikoa na Halmashauri, wakifuatilia wasilisho waliposhiriki katika, warsha ya Siku mbili ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri. Dodoma Leo
Sehemu ya washiriki wa warsha ya Siku mbili ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri. Dodoma Leo


Na; Mwandishi Wetu – Dodoma

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka watendaji wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kusimamia vizuri utekelezaji wa Programu ya Kilimo na Uvuvi katika maeneo yao kwani ni sekta muhimu katika uchangiaji wa uchumi na usalama wa chakula nchini.

Ameyasema hayo mapema leo Jijini Dodoma, katika warsha ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri.

Dkt. Yonazi amesema kuwa Serikali imeona kuna ulazima wa kuwepo kwa usalama wa mbegu katika kilimo hivyo kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini ASA imeweza kuwekeza mbegu kwa wingi ili kuyafikia maono ya serikali.

“Serikali imeendelea kusimamia uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora ambapo hadi kufikia Aprili 2023, jumla ya tani 49,962.35 za mbegu bora zimepatikana sawa na asilimia 26.68 ya mahitaji ya tani 187,197 kwa mwaka,”Alisema Dkt. Yonazi.

Aliongezea kuwa, serikali imejitahidi kuweka nguvu katika upatikanaji wa mbegu hizo ili kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula nchini, na kwa upande wa sekta ya uvuvi imehakikisha kunakuwa na manufaa ya rasilimali zilizopo katika sekta hiyo kwani bado hazijatumika vizuri.

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali ina mpango wa kununua meli zitakazotumika katika uvuvi wa kina kirefu cha bahari na hivyo kuweza kuongeza lishe na hatimaye nchi kunufaiika na rasilimali za uvuvi.

Aliendelea kufafanua kuwa, Programu hii pia, itahusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na upanuzi wa vituo vya uzalishaji wa vifaranga vya samaki cha Kingolwira Morogoro.

“Lazima tushirikishe wadau ili tupeleke elimu ya kuweza kuzalisha vifaranga na kujenga mabwawa, natoa msisitizo kwa viongozi wa mkoa kuwa kuna jukumu la usimamizi, tuhakikishe tunasimamia vizuri mradi huu, kushauri na kuutekeleza kwa wakati.” Alisisitiza Dkt. Yonazi

Awali, akiongea wakati wa Ufunguzi wa Warsha hiyo Bw. Paul Sangawe Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, alisema lengo la programu hii kwa upande wa sekta ya uvuvi, ni kuendeleza ufugaji wa viumbe maji pamoja na kuanza uvuvi wa bahari kuu.

“Tunatazamia katika program hii meli zitanunuliwa kwa matumizi ya pande zote mbili za Muungano na kuwezesha nchi yetu kwa mara ya kwanza kufanya uvuvi katika bahari kuu ili kuweza kutumia rasilimali tulizonazo kwa ufanisi, lakini vile vile uzalishaji wa mbegu pamoja na usambazaji, na kuhakikisha fedha ambazo za mkopo ambazo tumepewa kutoka shirika la IFAD takribani dola 58.8 milioni,zinatumika kwa ufanisi na kuleta tija katika utelezaji wa program hii.” Alisisitiza

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchumi na Uzalishaji toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Afisa Kilimo Mkuu Dkt. Rehema Mdendemi amesema programu hii ya maendeleo ya kilimo na uvuvi itaenda kuboresha maisha ya wakulima na wavuvi , na kujitosheleza kwa usalama wa chakula na kuleta ajira hivyo program hii ni ya muhimu kwa serikali na wanachi kwa ujumla.   

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad