HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 18, 2023

Ukweli kuhusu mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo

*Wafanyabiashara wakubwa wakwepa kodi tangu enzi za Awamu ya Nne watajwa kuwa chanzo cha mgomo

*Maamuzi ya Rais Samia ya kutuma timu ya mawaziri Kariakoo yazima mgogoro

*Kamati ya watu 14 kutoka Serikalini, wafanyabiashara yapewa jukumu la kumaliza mzizi wa fitna

Dar es Salaam
IMEBAINIKA kuwa wafanyabiashara wakubwa wanaokwepa kodi za forodha za kuingiza makontena ya bidhaa kutoka China na baadhi ya wanasiasa ndiyo waliokuwa chanzo kikuu cha mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo, huku wafanyabiashara wadogo wakitumika kama chambo na vipaza sauti kuchochea mgomo huo.

Wafanyabiashara hao ambao wanaagiza mzigo mkubwa wa bidhaa kutoka China, Uturuki, Dubai na nchi nyingine huku wakikwepa kodi wakati wanaingiza makontena yao ya bidhaa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, wamewachochea wafanyabiashara wadogo wa Kariakoo kugoma ili kushinika Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) isiwabane kwenye ukwepaji wao wa kodi.

Baadhi ya wanasiasa nao wameshiriki kuchochea mgomo huo kwa maslahi yao binafsi ya pesa na kisiasa.

Hivi karibuni umetokea mgomo wa wafanyabiashara kwenye soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambalo ndiyo soko kuu la bidhaa mbalimbali za jumla na rejareja zinazouzwa nchini na hata kwenye baadhi ya nchi jirani.

Mgogoro huo ulisababisha Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kutuma timu ya viongozi waandamizi, ikiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mwigulu Nchemba, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Ashatu Kijaji.

Baada ya kikao cha wazi cha mawaziri na wafanyabiashara, Serikali iliunda kamati ya watu 14, ikijumuisha maafisa waandamizi wa serikali na wafanyabiashara ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa malalamiko ya wafanyabiashara wa Kariakoo.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya soko la Kariakoo zimethibitisha kuwa wafanyabiashara wadogo wametumika kushiriki kwenye mgomo huo na wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza makontena ya bidhaa kutoka China na nchi nyingine ili kutengeneza mgogoro wa kisiasa.

"Kuna wafanyabiashara wanajulikana tangu enzi za Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ambao walikuwa ni vinara wa kukwepa kodi kwa kuingiza makontena ya bidhaa kutoka China, Dubai, Uturuki na nchi nyingine ndiyo chanzo cha mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo," kilisema chanzo kimoja cha habari.

"Wafanyabiashara hao vinara wa kukwepa kodi wamebanwa na TRA kwenye Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia, hadi makusanyo ya kodi yamevunja rekodi kwa kufikia wastani wa Shilingi trilioni 2 kwa mwezi ambayo haijawahi kutokea tangu tupate uhuru."

Baada ya kuona kuwa wamebanwa na TRA, hususan kwenye eneo la kudhibiti utozaji kodi wa makontena ya bidhaa kutoka China, na jitihada za kudhibiti maghala ya bidhaa kwenye maduka Kariakoo, wafanyabiashara hao wakubwa wakawachochea wafanyabiashara wadogo wa Kariakoo waanzishe mgomo wao uliodumu kwa siku kadhaa.

"Kusema ukweli TRA imefanya kazi nzuri ya kuwabana wakwepaji kodi hawa wakubwa kwa kutaka kila kontena la mizigo linaloingia nchini lilipiwe kodi stahiki. Hizi vurugu zote tunazoona Kariakoo ni matokeo ya hawa wafanyabiashara wakubwa wakwepaji kodi kutaka kuzua taharuki ili TRA iache kuwabana," alisema mfanyabiashara mmoja wa Kariakoo.

Baadhi ya matatizo waliyolalamikia wafanyabiashara ni utitiri wa kodi na tozo za Serikali kuu na Serikali za Mitaa, viwango vikubwa vya kodi ya TRA, rushwa miongoni mwa baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu wa umma wa TRA, TANROADS, LATRA na Polisi.

"Baadhi ya malalamiko ya wafanyabiashara wa Kariakoo, ikiwemo kuombwa rushwa na watumishi wachache wa TRA wasiokuwa na maadili, viwango vikubwa vya kodi na utitiri wa tozo za Serikali za Mitaa yana hoja. Lakini nyuma ya pazia waliochochoea mgomo huo ni hao wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza makontena ya bidhaa kutoka China na nchi nyingine," alisema.

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa kwa mwaka 2021 peke yake, Tanzania iliingiza bidhaa zenye thamani ya karibu dola za Marekani Bilioni 2.7 kutoka China, ambayo ni sawa na Shilingi trilioni 6.5, huku sehemu kubwa ya mizigo hiyo kutoka China ikiwa ni bidhaa zinazouzwa kwenye soko la Kariakoo.

"Lengo la wafanyabiashara wakubwa hawa ambao ni vinara wa kukwepa kodi ni kuchochea mgomo wa wafanyabiashara wadogo wa Kariakoo ili kuishinikiza Serikali iwaagize TRA waache kuwabana wakwepa kodi hawa kwenye mamia ya makontena ya bidhaa kutoka nje ambayo wanaingiza kila mwezi na kwenye maghala yao ambayo wanayatumia kukwepa kodi," alisema muuza duka mmoja wa Kariakoo.

"Tunaipongeza Serikali ya Rais Samia kwa kusikiliza kilio cha wafanyabiashara wadogo wa Kariakoo kuhusu ukubwa wa viwango vya kodi na utitiri wa tozo kutoka manispaa, lakini tunaomba Serikali iwe makini na hawa wafanyabiashawa wakubwa wakwepa kodi wanaotaka kututumia wafanyabiashara wadogo kufanikisha ukwepaji wao wa kodi."

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad