Teresia Mhagama na Zuena Msuya
WAZIRI Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa amesema kuwa, suala la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ni moja ya vipaumbele vya nchi na kwamba Serikali inahakikisha kuwa uandaaji wa Dira na Mpango Mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unafanyika kwa kasi na kwa umakini ili kuanza kutekeleza azma hiyo.
Amesema hayo tarehe 19 Mei, 2023 jijini Dodoma wakati akiongoza Kikao cha Tatu cha Kikundi Kazi cha Taifa cha Nishati Safi ya kupikia ambacho kilishirikisha Mawaziri wanaosimamia sekta zinazohusika na mradi huo wakiongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba ambae ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri ya Kikundi Kazi hicho. Makatibu Wakuu wa Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wadau kutoka Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo pia walihudhuria.
Kikao hicho ambacho ni cha ngazi ya Kamati ya Mawaziri ya Kikundi Kazi cha Nishati Safi ya Kupikia kilikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili rasimu ya Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia 2033 na Mpango Mkakati wa utekelezaji wake pamoja na rasimu ya mapendekezo ya uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, taarifa ya uchambuzi wa miongozo mbalimbali inayohusu nishati safi ya kupikia pamoja na maboresho yaliyofanyika baada ya kikao cha Waziri Mkuu kilichofanyika tarehe 23 Machi, 2023.
“Serikali imeamua kwenda nalo kasi suala hili la nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa mazingira kwani nishati ambayo si salama kama kuni na mkaa inatumika kwa kiasi kikubwa kwa kupikia hivyo tutakapoanza kutekeleza Dira hii, kwa kiasi kikubwa tutapunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda afya za wananchi.” alisema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, aliipongeza Kamati ya Uongozi ya Makatibu Wakuu inayoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kutoa mwongozo na maelekezo yaliyosaidia kuboresha nyaraka hizo muhimu. Aidha, aliwapongeza Kamati ya Wataalamu pamoja na Sekretarieti ya Kikundi Kazi kwa maandalizi ya nyaraka hizo.
Aidha, ameiagiza Kamati ya Wataalamu ya Kikundi Kazi cha Taifa cha Nishati Safi ijumuishe maoni yote yaliyotolewa yakiwemo ya Wadau wa Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo ili kuboresha Dira na Mpango Mkakati na ziwasilishwe ofisi ya Waziri Mkuu tarehe 26 Mei 2023.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba alisema kuwa, kikao hicho kilichoshirikisha wadau kutoka Sekta binafsi na Washirika wa Maendeleo kimepokea maoni yaliyotolewa kwenye kikao hicho ambayo yatasaidia kuboresha rasimu hizo za Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo, Muundo wa Mfuko wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na Taarifa ya Uchambuzi wa Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali inayohusika na nishati ya kupikia ili kuweka uwiano.
Alisema kuwa, suala la utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia limezingatia miongozo mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kama Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs-2030) ambapo lengo namba 7 linazungumzia masuala ya upatikanaji wa nishati safi na bei nafuu.Makamba alisisitiza kuwa Dira hii inakataza matumizi ya mkaa wa asili ambao una athari kwa afya na mazingira, hivyo uwekezaji katika mkaa mbadala wenye viwango vinavyotakiwa uendelee.
No comments:
Post a Comment