HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 2, 2023

KAFULILA AANIKA UKWELI SEKTA YA UBIA KATI YA SEKTA YA UMMA NA BINAFSI ZINAVYOWEZA KUTEKELEZA MIRADI YA KIMKAKATI

 


-Ukiwemo mradi wa Ujenzi wa barabara ya mwendo kasi ya kulipia kutoka Dar- Moro

-Azungumzia namna Serikali itakavyookoa mabilioni ya fedha miradi kitekelezwa

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

KAMISHNA wa Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ,Wizara ya Fedha na Mipango, David Kafulila ameeleza mikakati mbalimbali inayoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inayogharimu fedha nyingi inatekelezwa na Serikali kwa njia ya ubia.

Kwa mujibu wa Kafulila ni kwamba iwapo miradi hiyo ikatekeleza na sekta binafsi maana yake ni kwamba fedha ambazo zilipaswa kutumiwa na Serikali zinaweza kwenda kutumika kwenye miradi ambayo haina mvuto kwa sekta binafsi.

Ameyasema hayo leo Mei 2,2023, jijini Dar es Salaam, baada ya kufunguliwa kwa kikao kazi cha siku tano kati ya Serikali na wataalam kutoka taasisi ya Benki ya Dunia inayojihusisha na utoaji wa mikopo na misaada ya kiufundi kwa sekta binafsi( International Finance Corporation) kwa ajili ya kupitia na kujadili miradi ya kimkakati ambayo Serikali inataka itekelezwe kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP).

"Kikao kazi hiki cha siku tano kinachoanza leo mpaka Mei 6 kitakuwa mahususi kujadili sekta mbili ,sekta ya miundombinu ya umeme pamoja na miundombinu ya uchukuzi.Kwa hiyo tumewakutanisha watalaamu  Mamlaka nne zinazotoka uchukuzi kama TRC, TANROADS, TPA na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege(TAA)

"Upande wa nishati tumewakutanisha TANESCO pamoja na REA lakini vile vile kwa miundombinu ya Dar es Salaam tumewaita DART, kwa hiyo hizi ndio mamlaka Saba ambazo zinashiriki kwenye kikao kazi hiki kwa muda wa siku tano mahususi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa namna gani ya kupanga na kutekeleza miradi.

"Inafahamika Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara katika kusukuma ajenda ya sekta binafsi, kuhakikisha inatoa mchango wa kutosha, sekta binafsi ndio injini ya uchumi sasa kwenye ubia kati ya sekta ya umma na binafsi msingi wake ni kwamba sekta binafsi itekeleze baadhi ya maeneo ambayo sekta ya umma.

" Kwa maana ya Serikali haijatekeleza,nimetoa mfano mdogo sasa hivi tuko kwenye hatua ya kutafuta mwekezaji kwa ajili ya kujenga barabara kutoka Kibaha mpaka Morogoro ambako kuna vipande viwili , lipande cha Kibaha mpaka Chalinze kilometa 78.9 na kipande cha Chalinze kilometa takriban 120 na barabara hii Serikali imejigharamia maandalizi yake Kwa Sh.bilioni 7.1,"amesema.

Amefafanua ujenzi wa barabara hiyo ambayo itamilikiwa na kampuni binafsi itawekeza takribani dola bilioni 800 ,hivyo wananchi wanapaswa waone kwamba kwa kuandaa mradi vizuri kwa kutumia Kampuni ambayo ni ya Kimataifa kutoka Korea wanakwenda kutumia sh.bilioni Saba kuandaa mradi ambao utavutia mtaji wa sekta binafsi kujenga hiyo barabara na kuitekeleza kwa muda wa mkataba.

Amesema barabara hiyo yenye thamani ya zaidi ya trilioni mbili kama Serikali ingejenga yenyewe ingetumia kiasi hicho cha fedha lakini sekta binafsi ikijenga maana yake ni yenyewe imeweka hapo fedha badala ya Serikali,kwa hiyo tafsiri yake kiasi cha fedha hiyo ambayo Serikali ingekiweka hapo itakipeleka maeneo mengine.

"Kwa hiyo lengo la kikao kazi hiki ni kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo wa mamlaka zetu hizi kwa kuanzia miundombinu ya barabara na umeme ili kusudi ziweze kutekeleza miradi mikubwa , tunayo nafasi na fursa kubwa kutekeleza miradi mikubwa kwenye TANESCO,TANROAD na maeneo mengine

"TANESCO kwa mfano sasa hivi kitengo cha PPP na TANESCO tunashirikiana kuandaa miradi mitatu ya uzalishaji wa umeme kwa njia ya jua (Sola) ,Same ,Dodoma na Singida, miradi hii mitatu itakwenda kugharimu zaidi ya dola milioni 300 ,ambazo ni sawa na Sh.bilioni 650, kwa hiyo kiasi hicho ambacho kingewekwa na Serikali kutekeleza miradi kama hiyo kitakuja kuwekwa na sekta binafsi,"amesema

Kafulila amesema kwa hiyo fedha iliyotakiwa kuwekwa na Serikali itatumika kwenye maeneo mengine ambayo hayana mvuto wa sekta binafsi. Kwenye barabara kuna maeneo yenye mvuto kama barabara za Dar es Salaam, mradi wa kujenga barabara za Dar es Salaam ziko Out ring roads,ni mradi mkubwa ambao utagharimu zaidi ya trilioni mbili huku Akifafanua mradi wa kujenga barabara mwendo kasi ya Kibaha mpaka Morogoro ni zaidi ya dola milioni 800.

"Kujenga mradi wa barabara kutoka Isongole kule Tunduma mpaka Mbeya ambayo ndio boda yenye msomgamano mkubwa kuliko boda yoyote katika Afrika Mashariki,ile boda ina kilometa zaidi ya kilometa 200 na ujenzi wake utagharimu zaidi ya trilioni mbili.Kwa hiyo miradi ya barabara hii tu ya Dar es Salaam out ring roads,Kibaha Chalinze mpaka Morogoro, Isongole mpaka Tunduma kule mpakani, ni miradi ambayo inamvuto wa kutekelezeka kwa utaratibu wa PPP

"Miradi ya umeme hii tumeizungumza ya Sola tunawakaribisha wawekezaji wawekeze kwenye maeneo haya, ingawa kuna wawekezaji wameshaanza mazungumzo na Serikali kutekeleza miradi mitatu ya Sola katika maeneo hayo.Lakini kuna miradi ya usafirshaji wa umeme,Serikali ikiwekeza kwenye kusafirisha umeme usafirishaji umeme inatumia fedha nyingi sana.

"Lakini upo uwezakano wa sehemu ya hii transmission line kutekelezwa na sekta binafsi na Serikali ikaokoa fedha ambayo ingewekwa hapo ili kusudi iende maeno ambayo hayana mvuto wa sekta binafsi.Ukienda kwenye reli ,reli tunayozungumza Community reli , kwa mfano ya Dar es Salaam ni mradi mkubwa sana peke yake unaweza ukagharimu dola bilioni nane.

"Ni mradi mkubwa sana ambao Serikali ukisema utekeleze itaongeza deni , itaongeza kodi , lakini ikitekelezwa kwa sekta binafsi itapunguza uwezekano wa kupata deni na kuongeza kodi. Kwa hivyo hii ni miradi michache ambayo tunaizungumza.Tunamiradi kwa mfano uendeshaji wa reli kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma.

"Ni miradi ambayo inamvuto wa kuendeshwa na sekta binafsi,tuna reli kule za Mtwara hadi Mbambabay ni miradi ambayo inamvuto wa sekta binafsi mradi ule wa Mtwara unagharimu zaidi ya dola bilioni tano kwa tathimini ambayo imefanyika. Kwa hiyo kwenye reli na bandari ni maeneo ambayo yanamvuto mkubwa na yanagharimu fedha nyingi Serikali kuwekeza,"ameeleza.

Ameongeza iwapo watajipanga vizuri na wakaiweka sekta binafsi kutekeleza miradi hiyo Serikali itapunguza presha ya miradi hiyo kutekelezwa na Serikali na fedha ya Serikali ikawekezwa kwenye maeneo mengine ambayo hayana mvuto kibiashara

"Kwa kifupi hayo ndio yametukutanisha hapa ,tukaa hapa kwa siku tano kuumiza bongo,uzoefu wa duniani unaonesha nini kuhusu sekta hizi moja baada ya nyingine,sisi hali yetu inaonesha nini, nini tunakikosa,nini tunacho na hicho ambacho hatuna inagharimu kiasi gani kwenye mpango wa miaka mitano wa 2021/2022 hadi mwkwa 2025/2026.

"Kwa hiyo utaona hii sekta ya Ubia unaumuhimu kiasi gani katika kutekeleza miradi katika kipindi cha miaka mitano, ilikadiriwa kwamba sekta binafsi peke yake ilete mtaji wa takribani dola bilioni tisa ambazo ni sawa na takribani trilioni 21, na hizo trilioni 21 au dola bilioni tisa ni mpango mzima wa miradi ya maendeleo katika miaka mitano ambayo ni trilioni 114

"Unaweza kuona sekta ya Ubia ina umuhimu kiasi gani kufanikisha utekelezaji wa mpango wa miaka mitano ambao kwenye miradi ya maendeleo unagharimu sh.trilioni 114, hivyo tuko hapa kuona uzoefu wa duniani nini kinafanyika kwenye sekta na sekta na ili kwa pamoja kama alivyozungumza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya fedha kwa niaba ya Katibu Mkuu tutoka hapa ni miradi ambayo inagharimu Sh trilioni 21."

Kamishna wa Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ,Wizara ya Fedha na Mipango, David Kafulila
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad