HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 25, 2023

TCDC YASHAURIWA KUONDOA UPOTOSHAJI UNAOFANYWA KUHUSU USHIRIKA NA UMUHIMU WAKE

 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Kastori Msigara  ameiomba Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC)  kutatua changamoto za wakulima kwa kupunguza malalamiko  kuhusu Vyama vya Ushirika.

Amesema, malalamiko hayo yanatokana na upotoshaji wa dhana ya ushirika na kueleza Ushirika ni chombo kizuri ambapo kikisimamiwa ipasavyo wakulima watanufaika.

Msigara ametoa wito huo  leo tarehe 24/04/2023 wakati akipokea taarifa ya Mradi wa Mazao ya Bustani kutoka kwa wataalamu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika waliofika wilayani humo kutoa mafunzo ya siku 15 kwa Wakulima wa Halmashauri ya Moshi, Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Msigara ameongeza kuwa, wakulima wanapaswa kuelewa dhana ya Ushirika na kufaidi matunda ya Ushirika kwani ndiyo nguzo yao katika kufanya shughuli zao za kila siku.
“Ushirika ni Chombo kikubwa na muhimu kama kikitumika vizuri na ni wajibu wa Tume kuifanya Jamii kuupenda Ushirika na haya yanaweza kufanikiwa kwa uharaka kama Tume itaweza kushirikiana na Halmashauri” amesisitiza Msigara.

Tume ya Maendeleo ya Ushirika ipo Mkoani Kilimanjaro kwa zoezi la uhamasishaji kwa wakulima wa mazao ya Bustani yaani Mbogamboga, Maua, Viungo na Matunda kwa wakulima walio kwenye na wasio kwenye vikundi vya Kilimo cha Mazao hayo, ambapo leo tarehe 24/04/2023 uhamasishaji huo umetolewa katika eneo la Uchira na Kahe Mashariki. Uhamasishaji huo umetolewa kwa wakulima Wa kikundi cha Mbogamboga chenye wakulima 38. Uhamasishaji katika wilaya ya Moshi Vijijini utafanyika kwa siku 4 kuanzia leo.

Akitoa elimu ya Ushirika kwa wakulima wa mazao ya Bustani, Afisa Ushirika Ndimolwo Laizer amewaomba wakulima kuendelea kushikamana ili waweze kuunda ushirika uliyo imara na utakaojibu mahitaji yao.

Laizer ameongeza kuwa,  Tume ya Maendeleo ya Ushirika inapenda kuona wakulima wote wakijiunga na Ushirika ili waweze kunufaika na mambo mazuri yanayopatikana ndani ya ushirika kama kuuza mazao kwa pamoja, upatikanaji Wa pembejeo za Kilimo kwa urahisi na kwa bei nafuu ikiwa Ni pamoja na kuwa na uhakika wa kupata soko la mazao na bidhaa zitokanazo na mazao ya Bustani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad