HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 25, 2023

WAZIRI MKUU AKAGUA MIRADI WILAYA YA ITILIMA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwenye ukumbi wa Halmashauri, Machi 25, 2023. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,  Dkt. Yahaya Nawanda na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwenye ukumbi wa Halmashauri, Machi 25, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Baadhi ya watumishi wa wilaya ya Bariadi  mkoani Simiyu wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri, Machi 25, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
* Wabunge wa Simiyu wammwagia sifa Rais Samia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa shule ya sekondari ya Njalu katika kijiji cha Kimali, kata ya Nyamalapa, wilayani Itilima, mkoani Simiyu na kuagiza kwamba shule hiyo iwe ya mfano.

“Ujenzi wa shule hii usiishie kwenye madarasa na majengo ya utawala tu, bado inahitaji mabweni ya wavulana na wasichana, bwalo, viwanja vya michezo, nyumba za walimu na hapo baadaye tuwe na kidato cha tano na cha sita,” alisema.

Shule hiyo iliyojengwa kwa fedha za ndani za Halmashauri ya Itilima hadi sasa ina madarasa sita yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 45 kila moja.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Machi 24, 2023) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kimali kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule hiyo, mara baada ya kuikagua na kuweka jiwe la msingi.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala la umeme, Waziri Mkuu alisema wilaya hiyo imetengewa sh. bilioni 30 na kusisitiza kwamba mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme vijijini uko palepale.

Mapema, Waziri Mkuu alizindua mradi wa ghala la kuhifadhi mazao ya chakula katika kijiji cha Ikindilo, wilayani Itilima ambao umelenga kudhibiti sumukuvu kwenye mazao ya chakula.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Meneja wa mradi huo, Eng. Mohamed Kombo alisema ujenzi wa ghala hilo na miundombinu yake ulianza Agosti 9, 2021 na kukamilika Februari 15, 2023. Mradi unafadhiliwa na GAFSP, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Serikali Kuu.

“Lengo la mradi huu ni kusaidia kutoa elimu ya uhifadhi na kudhibiti sumukuvu kwenye mazao ya chakula ili kupunguza madhara yatokanayo na utumiaji wa mazao yaliyochafuliwa na kuvu inayosababisha sumukuvu,” alisema.

Alisema ujenzi umekamilika kwa asilimia 100, na mkandarasi amekwishakabidhi mradi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na ameanza kipindi cha uangalizi (defect liability period) cha mwaka mmoja.

Alisema Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa TANIPAC ipo katika hatua za mwisho za ununuzi ya vifaa vya ghala na maabara ikiwemo chaga za kuhifadhia magunia, mashine ya kupima sumukuvu (Aflatoxin screen-kit), mashine ya kupima unyevu, komputa ya mezani na mizani. Vifaa hivyo vinatarajiwa kufikishwa kwenye mradi Mei, mwishoni.

Alisema mradi ulitengewa sh. milioni 990.5 na mkandarasi amekwishalipwa sh. milioni 850 sawa na asilimia 86 mpaka sasa. “Gharama halisi ya ujenzi itajulikana baada ya kufanya ukaguzi na malipo ya mwisho baada ya kipindi cha uangalizi kukamilika (Final Account).

Wakati huohuo, Wabunge wa mkoa wa Simiyu walipopewa nafasi kusalimia wananchi wa maeneo hayo, kwa nyakati tofauti, walimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya elimu, afya, maji, barabara na umeme.

Walisema uwepo wa miradi hiyo umesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na mingine imechangia kuleta maendeleo ya haraka kwenye vijiji, kata na hata wilaya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad