HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 4, 2023

WANANCHI WAISHIO PEMBEZONI MWA VYANZO VYA MAJI WAPATA ELIMU

 Na Fredy Mshiu

Wananchi wa Kijiji cha Minazi Mikinda Kitongoji cha Lubungo Wilaya ya Kibaha Vijijini wameelimishwa kuhusu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji (Mto Ruvu) kutoka kwa Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu.

Elimu iliyotolewa imehusisha kuwahasa wananchi kuacha tabia ya kufanya kilimo katika vyanzo vya maji, uchimbaji wa madini katika vyanzo, pamoja na kuingiza makundi ya mifugo katika vyanzo vya maji.

Akiongea na wananchi wa Vitongoji hivyo Mhandisi wa Mazingira DAWASA, Sophy Ayoub amewataka wananchi kuacha uharibifu wa vyanzo vya maji kwani ni hatari kwa sasa na vizazi vijavyo.

"Uharibifu wa vyanzo vya maji huchangia kwa kiasi kikubwa mto kukauka, kuingiza mifugo na kilimo katika vyanzo vya maji kunapelekea mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoleta ukame wa muda mrefu na maji kukauka katika vyanzo" ameeleza ndugu Sophy.

Sambamba na hayo wananchi wa Kijiji Cha Minazi Mikinda wameelimishwa juu ya Sheria ya utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya maji na wapi mahali sahihi wanapaswa kufanya shughuli za kilimo pamoja na ufugaji kutoka kilipo chanzo cha maji.

Ndugu, Yulian Mizola Afisa Maendeleo kwa jamii kutoka Bonde la Wami Ruvu ameyaasa makundi yote yanayohusika na uharibifu wa Mazingira katika mto Ruvu kuwa Sheria haitabagua mtu yeyote anayehusika na uharibifu wa vyanzo vya maji na adhabu Kali zitachukuliwa juu yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lubungo ndugu, Selemani Mgweno ameshukuru DAWASA pamoja na Bonde la Wami Ruvu kwa kuleta elimu hii kwa wananchi wa eneo lake ambao wengi ni wafugajj na wakulima.

"Elimu mnayotupatia Leo hii ni muhimu sana, sasa wananchi watakua na uwezo wa kutambua ni wapi wanastahili kufanya shughuli zao za ufugaji na kilimo Ili wasilete athari za kimazingira na kuharibi vyanzo vya maji"ameeleza ndugu Mgweno

Wananchi wa Kijiji Cha Minazi Mikinda wameonyesha utayari wa kuacha kufanya shughuli za kijamii katika vyanzo vya maji huku wakiahidi kuwa mabalozi kwa wenzao wengi juu ya ulinzi wa vyanzo vya maji.













No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad