HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 13, 2023

TLP YAPEWA SIKU SITA KUWASILISHA MAJIBU YA MALALAMIKO YA WAGOMBE

 

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetoa siku sita kwa Chama cha Tanzania Labour Party(TLP) kuwasilisha majibu ya malalamiko yaliyotolewa na wagombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Chama hicho kuhusu kuahirishwa kwa mkutano maalumu wa chama hicho bila kufuata utaratibu.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa Machi 9, Mwaka huu na Makamu Msajili wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Sisty Nyahoza, imeitaka TLP kupitia kwa viongozi wake kuwasilisha majibu ya suala hilo ifikapo Machi 15 ili msajili aweze kujua nini hasa kilichopelekea uchaguzi huo kuhairishwa.

Awali kabla ya barua hiyo kutoka katika Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, wagombea watano wa nafasi ya Uenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, waliiandikia barua Ofisi ya Msajili wakidai kuahirishwa pasipo kufuatwa utaratibu mkutano wa maalumu wa chama hicho ambao pia ungehusisha kufanyika kwa uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa

“Hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 5B cha sheria ya vyama vya Siasa, Sura 258, uongozi wa TLP mnapaswa kuwasilisha maelezo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kujibu malalamiko yaliyotolewa na wagombea hao ili Msajili wa Vyama vya Siasa ajue ukweli kuhusu suala hilo” ilisema barua hiyo.

Kimsingi malalamiko yaliyowasilishwa na wagombea hao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa yamedai na kupinga hatua ya Katibu Mkuu wa Chama hicho Richard Lyimo kuahirisha Mkutano maalumu bila kufuata utaratibu, jambo walilodai kuwa limeharibu taratibu za kufanyika kwa uchaguzi huo.

Hata hivyo hatua hiyo imekuja ikiwa taratibu zote za kufanyika kwa mkutano huo uliotanguliwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Taifa uliopitisha majina matano yanayowania nafasi hiyo likiwemo la Katibu Mkuu ambaye saa chache kabla ya kufanyika uchaguzi huo aliahirisha mkutano huo kwa sababu ambazo baadhi ya wajumbe wamesema hazina mashiko.

Wajumbe hao wakiwemo waliotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, wamedai hatua ya Katibu Mkuu kuahirisha mkutano huo imetokana na hofu yake kuona kuwa angeshindwa katika uchaguzi huo kutokana na uwepo wa mmoja wa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti ambaye ndiye anaonekana kukubarika.

“Lyimo yeye ndiye aliyeitisha uchaguzi, huku yeye pia ni mgombea, sasa wagombea wengine walivyojitokeza kuchukua fomu ambapo pia alifanya siri, akaonekana kama amevurugwa na kuamua kuleta mizengwe akiogopa kushindwa, kuna wakati alitaka jina lake lipitishwe peke yake kwenda kwenye mkutano mkuu suala ambalo wajumbe hakukubaliana nalo” alisema mmoja wa wajumbe
Aidha uchunguzi umebaini mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo Injinia Ivan Maganza ambaye kwa kipindi kirefu amefanya kazi vizuri na aliyekuwa Mwenyekiti wa TLP Taifa na mwanzilishi wa chama hicho Hayati Augustino Mrema, ndiye anayeonekana kuwa tishio kwa Katibu huyo kutokana na kukubalika kwake.

Injinia Maganza ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa TLP, amejijengea ushawishi mkubwa kwa wanachama wa chama hicho kutokana na kuwa na historia nzuri ndani ya chama hicho akiaminiwa kuwa atasaidia kukijenga kiuchumi endapo atashinda ushaguzi huo.

Awali Makamu Mwenyekiti wa TLP Taifa Bara Domina Rwechungula, alidai kusikitishwa na mwenendo wa sasa wa Chama hicho na kudai kuwa alichofanya Katibu Mkuu huyo wa Chama ni kutaka ‘kubaka’ demokrasia ndani ya chama kitu alichosema katu hawatoacha kifanyike.

Amesema ukiacha wagombea hao watano ambao wajina yao yalipitishwa, yeye pia alikuwa mmoja wa wagombea ambapo baadae aliamua kujitoa baada ya maswali yake hasa wapi fedha za uchaguzi huo zimepatikana kukosa majibu kutoka kwa Katibu Mkuu huyo Richard Lyimo ambaye ndiye aliyefanikisha zikapatikana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad