HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 18, 2023

TAASISI YA USTAWI WA JAMII WAWANOA WADADA WA KAZI, FAMILIA ZINAZOISHI NAO ZAASWA KUKAA NAO VIZURI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni akizungumza wakati wa kufungua mafunzo kwa wadada wa kazi kwaajili ya kuwajengea uwezo wa ukuaji na makuzi ya mtoto jijini Dar es Salaam leo Machi 18, 2023.
Baadhi ya wadada wa Kazi wakiwa katika Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Ustawi wa jamii jijini Dar es Salaam leo Machi 18, 2023.

Na Avila Kakingo, Michuzi TV.
FAMILIA zinazokaa na wadada wa kazi wanashauriwa kuishi na kukaa nao vizuri ili kupunguza ukatili wa watoto unaotokea majumbani.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 18, 2023. Ikiwa ni kuelekea siku ya Ustawi duniani ambayo hufanyika Machi 21 kila mwaka.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii watoa mafunzo mahususi kwa wanaokaa na watoto juu ya Malezi na makuzi ili waweze kuwaelewa na kuwa msaada chanya katika maendeleo na makuzi ya mtoto.

"Kila binadamu anamapungufu yake kwahiyo hata anapokosea, basi tumwelekeze vizuri kwa sababu hao ndio tunawaachia watoto kuanzia asubuhi hadi jioni tunapokuwa kazini au katika maeneo ya kutafutia vipato, kwahiyo tunavyowa'treat' vibaya wanaweza kuhamishia kwa watoto wetu,

kwa sababu wanamchango mkubwa katika malezi na makuzi ya watoto." Amesema Dkt. Joyce

Amesema kuwa Wazazi/walezi wakumbuke kuwa mtoto anajenga ukaribu sana na dada (Msichana wa kazi), kwahiyo yeye ndio anakuwa rafiki yake na mtoto anaweza kumwambia vitu vingi sana 'dada' na asimwambie Mama au baba yake.

"Sisi tunapaswa kuwa karibu sana na wadada wa kazi, tuwasikilize hata anapokushauri na kufatilia kile ambacho wadada wanashauri hata kama hajasoma lakini anaona mtoto wako pale nyumbani jinsi anaishi na wao ndio marafiki wakubwa wa watoto pale nyumbani." Amesisitiza

Amesema kuwa wasichana wa kazi zaidi ya 200 walijiandikisha kushiriki mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo wa kujiamini wakati wanavyolea watoto na kuishi bila kufanya ukatili.

Mhadhiri wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, na Mratibu wa kitengo ushiriki jamii, Danstan Haule amesema kuwa mafunzo hayo wa wadada wa kazi ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wadada wa kazi katika usafi, kujilinda na namna ya kuwasiliana pale wanapokuwa na changamoto ndani ya familia.

Pia katika mafunzo wanayopewa ni pamoja na kujiwekea akiba pale wanapofanya kazi... "Benki ya CRDB watawawezesha namna ya kuweka akiba kwaajili ya maisha yao ya baadae na sio kutumia fedha yote kama sehemu ya mshahara."

Kwa Upande wa Mnufaika wa mafunzo hayo, Martha Kavindi amesema kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kuwalea watoto pia kujiandaa kuwa wamama wa baadae.

Amesema wataweza kujua hatua za ukuaji wa mtoto kimwili, kiakili, kiroho na ukuaji wa kijamii na kujua watoto anaowalea wanapitia hatua zote kama walivyofundishwa.

Akizungumzia changamoto wanazokutana nazo ni pamoja na wazazi wa watoto kukosa nafasi hata ya kuwasikilia na kudai kuwa wamechoka.

"Hatupati muda wa kuongea na wazazi wa watoto changamoto walizonazo watoto katika makuzi yao, hasa wazazi wanakuwa bize na simu na muda mwingine wanasema wamechoka." Ameeleza Martha.

Kwa upande wa Lucy Lazer amesema kuwa amejifunza namna ambavyo ataweza kukaa na watoto, namna ya kucheza nao na namna ya kujua mabadiliko yake katika makuzi yake.

Wahadhiri wa Chuo hicho wametoa pia mafunzo ya Jinsi ya kukabiliana na misongo ya mawazo, matumizi sahihi ya fedha na kuweka akiba, usafi na mawasiliano kwa Wadada hao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad