HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 7, 2023

SHEIKH KIUNGIZA: IMANI YA WAISLAMU INAPINGA NDOA ZA WATU WA JINSIA MOJA

 

Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa (wa pili kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Msikiti wa Madina Ummul -Fatma Tungansanga uliojengwa Kijiji cha Kisiliga Kata ya Gumanga Wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa ufadhili wa Taasisi ya Istikaama. Kushoto kwake ni Kadhi wa Mkoa wa Arusha Sheikh Rajabu Kiungiza.

Na Dotto Mwaibale, Singida
KADHI wa Mkoa wa Arusha Sheikh Rajabu Kiungiza amesema msukumo wa imani uliopo ndani ya mioyo ya waislamu ndio unaowafanya waweze kupinga ndoa za kuoana kati ya mwanaume na mwanaume na mwanamke na mwanamke.

Sheikh Kiungiza aliyasema hayo jana katika hafla ya ufunguzi wa Msikiti wa Madina Ummul -Fatma Tungansanga uliojengwa Kijiji cha Kisiliga Kata ya Gumanga Wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa ufadhili wa Taasisi ya Istikaama.

"Hakuna kitu kinachotusukuma kuyapinga matendo hayo zaidi ya imani ya Mwenyezi Mungu tuliyonayo katika mioyo yetu na tukiwa na vitu hivi viwili yaani imani na ucha Mungu tutavishinda vita hivi" alisema Sheikh Kiungiza.

Alisema wale wote wanaowaingilia wanaume wenzao kwa matamanio badala ya wanawake na wanawake wanaofanya mapenzi ya jinsia moja badala ya wanaume ni watu wanaofanya ujinga kabisa mbele za Mwenyezi Mungu.

Sheikh Kiungiza alisema mtu mwenye akili hawezi kufanya uchafu huo ambao hata mbuzi hawaufanyi kwani huwezi kuona mbuzi mwanaume akimkimbiza mbuzi mwenzake mwanaume kwa ajili ya kufanya uchafu huo au mbuzi wakike akifanya hivyo dhidi ya mbuzi mwenzake wa kike.

"Inakuweje wewe mwanadamu ambaye Mungu amekutukuza na kuwa mwizi wa fadhira ambaye unaacha fadhira ulizofadhiriwa na Mungu na kufanya machafu hayo ambayo ni zaidi ya wanyama ambao hawayafanyi, ndugu zangu waislamu ni jukumu letu kupaza sauti ya kuyakataa mambo haya." alisisitiza Sheikh Kiungiza.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Istikaama Mkoa wa Singida, Khalfan Salum akizungumza kwa niaba ya wadhamini wa msikiti huo aliomba nyumba hiyo ya Mungu itunzwe na kufanyiwa usafi ili tija ipatikane kwa kile kilichokuwa kimekusudiwa na si vinginevyo.

Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema watu wanaojitoa kuhimarisha ujenzi wa nyumba za Mungu (misikiti) hawana cha kuogopa kwa kutoa kwao kwa hofu ya kufilisika na kuwa maskini ambapo aliwashukuru wafadhili hao na kuomba taasisi zingine ziige mfano huo.

Aidha Sheikh Nassoro alitoa angalizo kwa taasisi zenye kufadhili ujenzi wa misikiti kuacha tabia ya kutoa masharti kwa waumini kuhama katika madhehebu yao na kujiunga kwao na kuwa jambo hilo sio nzuri na hawatakuwa tayari kushirikiana na taasisi hizo.

Sheikh Nassoro alitumia nafasi hiyo kuwaomba Waislamu, wafadhili, watu binafsi na taasisi mbalimbali kumuenzi Mzee Sheikh Ali Majid ambaye ni kikongwe wa kwanza katika Manispaa ya Singida kujitoa na kuguswa kulitunza jengo la Masjid Taqwa kwa wakati huo.

Alisema mzee huyo aliguswa na hali iliyokuwa ikifanyika kabla ya kukamilika kwa jengo la msikiti huo ambapo baadhi ya watu walikuwa wakifanyia mambo yasiofaa na mzee huyo kwa mikono yake alikuwa akikata miba aina ya mitunduru na kuiweka kwenye milango na madirisha ili watu hao wasiweze kuingia.

"Ninacho waomba ndugu waislamu ni kuwa hivi sasa msikiti huo unataka kubadilishwa na kuwa wa kisasa zaidi wa ghorofa na ili kumuenzi Sheikh Ali Majid nawaomba mchango wa hali na mali ili tupate vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo kwani tayari tuna nondo 1800 ambazo zimepatikana kutoka kwa baadhi ya watu walioguswa na jambo hilo" alisema Sheikh Nassoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad