HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 7, 2023

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LAMUAGA KIJESHI ALIYEKUWA KAMISHNA MSTAAFU MARTIN MBAGO JIJINI DAR ES SALAAM

Kamishna wa Usalama kwa Umma wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jesuald Ikonko akiweka shada la maua kwa niaba ya Watumishi wote wa Jeshi hilo, wakati wa kuuaga mwili wa Aliyekuwa Kamishna Mstaafu wa Zimamoto na Uokoaji Martin Mbago, Chanika Zingiziwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam tarehe 6 Machi, 2023. Mwili wa Marehemu Kamishna Mstaafu wa Zimamoto na Uokoaji Martin Mbago ukiwa mbele ya waombolezaji waliohudhuria ibada ya kutoa salamu za mwisho nyumbani kwa marehemu Chanika, Zingiziwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam tarehe 6 Machi, 2023.

Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mbaraka Semwanza akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo wakati wa kuuaga mwili wa Aliyekuwa Kamishna Mstaafu wa Zimamoto na Uokoaji Martin Mbago, Chanika Zingiziwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam tarehe 6 Machi, 2023.

Na Zablon I. Mangare
KAMISHNA wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mbaraka Semwanza akimuwakilisha Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, leo tarehe 6 Machi, 2023 ameungana na waombolezaji katika misa ya kuuaga Kijeshi Mwili wa aliyekuwa Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (1995-1996) Martin K. Mbago nyumbani kwa marehemu Chanika Zingiziwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi, Kamishna Semwanza alisema Marehemu Kamishna Mstaafu Mbago, alitumikia vyema na ni miongoni mwa waanzilishi ambao wamelitengeneza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa na Muonekano huu tunaouona hii leo, na kuongeza kuwa Marehemu alifanya kazi kwa uaminifu na weledi na kuwatengeneza Maafisa na Askari ili kuja kulitumikia Jeshi katika huduma za Kuzima moto na Uokoaji.

“…kwa Ujumla, Marehemu alifanya kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu, amewatengeneza Askari na Maafisa ili kuja kulitumikia Jeshi na Taifa kwa Ujumla katika kutoa huduma za kuzima moto na uokoaji katika dharura mbalimbali…” alisema Kamishna Semwanza.

Katika Misa hiyo ya Kuuaga mwili wa Kamishna Mbago, Viongozi mbalimbali walihudhuria ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Benard Mchomvu, Makamishna Jenerali Wastaafu, Makamishna Wastaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara na Kamishna Mstaafu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Ali Malimussy.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa shukurani za dhati kwa wote waliohusika katika kufanikisha zoezi la mazishi ya Mwili wa Marehemu Martin Mbago.

(Picha zote na Jeshi la Zimamoto wa Uokoaji)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad