HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 21, 2023

RAIS MWINYI AZINDUA MATOKEO YA UTAFITI COVID 19

 

Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi akisalimiana na Ahmed Salim ambaye ni mtoto wa Amne Salim baada ya kumaliza kusoma hotuba yake wakati  wa hafla ya uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa Covid 19 uliofanywa na Chuo hicho  kwa ufadhili wa familia ya Amne Salim, ambaye alikuwa mke wa waziri Mkuu Tanzania,  salim Ahmed Salim.

Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi Ya uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa Covid 19 uliofanywa na Chuo cha Afya na Sayansi (MUHAS) kwa ufadhili wa familia ya Amne Salim, ambaye alikuwa mke wa waziri Mkuu Tanzania,  salim Ahmed Salim.
Baadhi ya watafiti na wadau kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) wakisikiliza hotuba ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi wakati wa hafla ya uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa Covid 19 uliofanywa na Chuo hicho  kwa ufadhili wa familia ya Amne Salim, ambaye alikuwa mke wa waziri Mkuu Tanzania,  salim Ahmed Salim
Mhadhiri wa Muhas, Alphoncina Kagaigai ambaye utafiti wake ulijikita kuangalia matatizo ya afya ya akili kwa wahudumu wa afya wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa matokeo ya Covid 19 uliofanyika leo Machi 21,2023 MUHAS



Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
SERIKALI imewaelekeza wataalamu wa afya kutumia matokeo ya tafiti ya Covid 19 kutunga sera bora zitakazosaidia kudhibiti ugonjwa huo na magonjwa ya mlipuko yatakayoweza kujitokeza baadae.

Pia imesema iko tayari kutumia matokeo ya tafiti za wanasayansi kwa maslahi ya taifa na kuongeza kasi ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

Rais Wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Machi 21, 2023 wakati wa akizindua matokeo ya utafiti wa Covid 19 uliofanywa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kwa ufadhili wa Amne Salimu.

"Ili matokeo ya tafiti yawe na tija yanapaswa kuwafikia watunga sera watakaohakikisha wanatunga sera bora zitakazotatua changamoto kwani ushauri wa kisayansi unaweza kuwa na tija zaidi ikiwa utatumika kwa wakati na si kukaa kwenye majarida ya kitaaluma pekee" amesema Rais Mwinyi.

Aidha amewataka wataalamu wa afya kutumia matokeo ya utafiti huo katika kuongeza kasi ya kudhibiti maambukizi ya Covid 19, Tanzania Bara na Zanzibar huku pia akiwahimiza watafiti wote kuhakikisha tafiti zao zinawafikia watumiaji na wataalamu wahakikishe wanatumia matokeo ya tafiti hizi kuboresha mifumo ya afya nchini.

Dkt. Mwinyi amesema utafiti huo umeonesha athari mbalimbali za Covid 19 hivyo, yapo mafunzo ambayo wakiyatumia vema yatawasaidia kupambana na ugonjwa huo na mengine yatakayokuja.

Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza familia ya Amne Salim kwa kuona umuhimu wa tafiti na kuelekeza ufadhili wao katika ugonjwa huo ili kuifanya serikali na watanzania kwa ujumla kuelewa tatizo hili hii ni mara ya kwanza kwangu kuona tafiti za wanasayansi kama hawa zinatolewa na familia binafsi, tumezoea tafiti hufanyika kutokana na misaada kutoka nje au fedha zaserikali."

Taifa bora linajengwa na watu wenye afya endapo watafanya utafiti zitakazobaini changamoto zinazowakabili na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali.

Amesema chuo hicho kimetumia fedha kama ilivyotakiwa katika kufanya utafiti huo kwa uwazi, weledi na uaminifu ambao utawasaidia kuongeza fursa za ufadhili kitaifa na kimataifa.

Amesema wataalamu wa chuo wamekuwa mstari wa mbele kuwashauri Wizara ya Afya Zanzibar katika kuunda na kuandaa miongozo mbalimbali ya kuboresha huduma.

"Tunaomba muongeze ushirikiano na taasisi zetu za Zanzibar na tutaendelea kuwapa ushirikiano kuhakikisha tunapiga hatua kuimarisha afya za watanzania. Nawapongeza kuwa kinara wa elimu ya juu kwa upande wa tiba na sayansi shirikishi, mnazidi kuaonga mbele kwa kuongeza kozi zenye uhitaji katika taifa letu na uzalishaji wataalamu wa afya wenye weledi na tafiti katika tiba." amesisitiza Rais Mwinyi.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda amesema serikali imetenga fedha kwa ajili ya watafiti mbalimbali nchini ili waweze kuchapisha tafiti zao katika majarida ya juu duniani.

Amesema watafungua dirisha la maombi mwishoni kwa mwezi huu na kwamba watakaoshinda watapewa Sh milioni 50 kama motisha ya kuwahamasisha kufanya tafiti zenye kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Naye, Mtoto wa Amne Salimu ambaye alikuwa mke wa Waziri Mkuu wa Tanzania, Salim Ahmed Salim, Ahmed Salim, amesema sababu za kuanzisha mfuko huo ni katika kusaidia jamii kukabiliana na ugonjwa wa COVID 19 ambao umesababisha vifo vya watu wengi ikiwemo mama yao, Amne.

Amesema ugonjwa huo umekuwa na athari kubwa kwa familia nyingi nchini Tanzania na duniani na kwamba utafiti wa kisayansi utasaidia katika kutoa taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo ikiwemo tabia, maambukizi na namna ya jamii kujikinga

Amesema msaada huo umetolewa kama kumbukumbu ya kifo cha mama yao, Amne na kwamba inakumbusha jukumu la kila mtu kuona anao mchango katika taifa na kukabiliana na majanga mbalimbali ya maradhi.

"Baada ya mama yetu kufariki dunia sisi kama familia tulikaa na kuona ni namna gani tutachangia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu na namna ya ambavyo Watanzania wataweza kunufaika na fedha tutakazozitoa." Amesema Ahmed.

Pia amesema wataendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia kwenye mfuko huo na kwamba kila mwaka watakuwa wanaongeza fedha za utafiti mpaka pale ugonjwa huo utakapokoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad