HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 20, 2023

POLISI NI WADAU WAKUBWA WA WCF, KATIKA UTOAJI TAARIFA ZA MATUKIO YA AJALI ZA BARABARANI

  
MWANZA: Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani 2023.

Maadhimisho ya mwaka huu yanayo kwenda na kauli mbiu isemayo 'Tanzania Bila Ajali Inawezekana Timiza Wajibu Wako’ yamefunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) ambaye ametoa wito kwa watanzania wote kuzingatia sheria za barabarani zilizowekwa ili kupunguza ajali.

"Jukumu la usalama barabarani ni la kila mmoja wetu na sio Serikali pekee. Tushirikiane kwa pamoja kuonyana kila mmoja wetu anapovunja sheria za usalama barabarani kwa ajili ya kupunguza ajali na kuokoa maisha", alisema Waziri Mkuu wakati akifungua rasmi Maadhimisho hayo jijini Mwanza.

Sambamba na kufungua maonesho hayo, Mhe. Waziri Mkuu alikabidhi vyeti vya udhamini na ushiriki ambapo WCF ni mmoja kati ya wadau hao.

Akizungumza kwa upande wa WCF mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. James Tenga amesema Jeshi la Polisi limekua mshirika wa karibu na WCF katika kurahisisha utoaji wa fidia kwa wakati kwa wafanyakazi wanaopata ajali hususan za barabarani.

"Jeshi la Polisi limeendelea kuwa mshirika muhimu sana wa WCF. Polisi wamekuwa na msaada mkubwa sana katika utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa kutoa taarifa za uthibitisho wa ajali hususan za barabarani  na kuhakikisha haki inapatikana kwa wafanyakazi waliopata ajali wakiwa katika utimizaji wa majukumu ya kazi kulingana na mikataba yao ya ajira’. Amesema Tenga.

“ Kauli mbiu ya 'Tanzania Bila Ajali Inawezekana Timiza Wajibu Wako’ inaendana na majukumu ya Mfuko ya kuhakikisha  tunashiriki katika kupunguza ajali zinazotokana na kazi nchini, sambamba na kupunguza vifo kutokana na ajali za Barabarani kwa Wafanyakazi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi.”

"Tunategemea Ushirikiano wa WCF na Jeshi la Polisi kuendelea kuimarika ili kuongeza tija kwenye utoaji wa haki ya msingi ya fidia kwa wafanyakazi na kupunguza matukio ya ajali za barabani".

Maonesho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani 2023 yamefanyika kitaifa jijini Mwanza katika viwanja vya Furahisha ambapo taasisi mbalimbali za Umma na binafsi zimeshiriki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad