HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, March 26, 2023

KINANA AHIMIZA VIONGOZI WA DINI KUWAJENGA WAUMINI KUHESHIMU IMANI ZA WENGINE

 MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema ni jukumu la viongozi wa dini kuwaunganisha Watanzania,

kudumisha amani, umoja na mshikamano.


Pia, ametaka kuendeleza utamaduni kuheshimu imani ya kila mmoja kwa kutazama mambo mazuri na sio changamoto chache zinazojitokeza.

Kinana aliyasema hayo leo Machi 26, 2023 wakati akizungumza katika hafla ya mashindano ya kuhifadhi na kusoma Kuraani tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Aswhabu al-Kahfi Islamic Centre, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Hivi sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameweka mkazo kwenye maridhiano na tuna taasisi ya maridhiano na amani mbayo imeunganisha dini na madhehebu mbalimbali nchini, lengo ni kudumisha umoja, mshikamano na amani katika taifa letu.

“Mimi ningependa kuwasihi viongozi wa dini, kila madhehebu, kila dini ni muhimu tushikamane…msitafute mapungufu ya kila mmoja, mtafute mema ya kila mmoja ili tuweze kushikamana,” alisema.

Kinana aliwasihi Watanzania kuzingatia na kutanguliza mambo mazuri ya kila mmoja kuondoa uwezekano wa kuibua migogoro isiyo na tija kwa ustawi wa taifa.

Awali akimkaribisha Kinana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo, alisema amani na maadili yanasisitizwa mahali popote kwani hata Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 imetaja ajenda ya amani na maadili.

“Leo tupo hapa tunafanya mashindano ya Kuraani tukufu bila ya changamoto yoyote, hii ni kutokana na maadili, amani na utulivu uliopo nchini,” alisema.


Katika mashindano hayo Jafo aliwataka viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dk. Samia kuleta maendeleo nchini.

“Rais Samia anafanya mambo mengi mazuri kazi yetu sisi tumuunge mkono kwa kutunza amani iliyopo ili yeye aendelee kuleta yale mazuri anayoyahitaji kuyafanya ndani ya Tanzania,” alisema.

Akitolea mfano wa faida ya amani na utulivu Jafo alisema tayari Rais Dk. Samia ameshatoa mabilioni ya fedha kutekeleza mradi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo ujenzi wake unakwenda kasi.
“Mradi huu unaenda vizuri kwa sababu kila njia ina mkandarasi anafanya kazi,” alisema.

Aidha, alisema kuanzia mwaka jana wanafunzi wote wa kidato cha kwanza walianza shule kwa pamoja na kulikuwa hakuna chaguo la pili kama ilivyozoeleka huko nyuma.

“Mambo hayo yote yanafanyika kwa sababu ya kuwepo kwa amani inayosababaisha miradi ya maendeleo,” alisema

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Omar aliwasisitiza wazazi na walezi kuitekeleza kaulimbiu ya mashindano hayo inayosema ‘Jambo limekuwa jambo, Qur’an ni mkombozi wa malezi’.

Alisema kaulimbiu hiyo inatakiwa itekelezwe kwa vitendo hususan kwa wazazi na walezi wa Kiislamu.
“Kila mzazi ashike nafasi yake ya kumlea mtoto wake katika maadili ya dini, akiifuata Qur’an Tukufu kwa kuwa ndio mwongozo bora wa malezi ya watoto na kuifanya jamii iwe na vijana hodari, wenye kumtii Mwenyezi Mungu,” alisema.

Katika mashindano hayo Bakari Hamadi (19) mwanafunzi wa madrasa ya Mjamma Rahmaan ya Mkuranga mkoani Pwani aliibuka mshindi katika kipengele cha kuhifadhi juzuu 30 na kuzawadiwa sh. milioni 2.5.


Pia, Hujaima Othman (8) mwanafunzi wa Madrasat Ibnu Makhtuum iliyopo Chamazi, alishika nafasi ya kwanza kwa upande wa juzuu tatu ambapo alizawadiwa sh. 300,000.
Ndg. Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Akihutubia  viongozi wa Dini ya Kiislam,Waumini,Washiriki  katika Mashindano ya Nane ya Kuhifadhi Quran Tukufu Mkoa wa Dar es Salaam yaliyoandaliwa na Taasisi ya Asw- haabul Kahfi Islamic Centre, ukumbi wa kimataifa wa Mwl Julius Nyerere,Machi 26,2023.(Picha zote na Fahadi Siraji )

Ndg. Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Akikabidhi zawadi kwa  Hujaima Othman (8) mwanafunzi wa Madrasat Ibnu Makhtuum iliyopo Chamazi, aliyeshinda nafasi ya kwanza kwa upande wa juzuu tatu ambapo alizawadiwa sh. 300,000.(Picha zote na Fahadi Siraji )

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad