HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 13, 2023

Benki ya NMB yashinda Tuzo ya Benki Bora Tanzania 2023, Ruth Zaipuna kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Bora kwa miaka miwili mfululizo

  

Benki ya NMB imeandika historia nyingine baada ya kutwaa Tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa mwaka 2023 wakati wa mkutano wa Africa Bank 4.0 Summit uliofanyika jijini Nairobi, nchini Kenya kutokana na jitihada ma utendaji kazi wa benki hiyo katika kuimarisha uchumi wa Tanzania kwa kutoa suluhu za kidijitali na huduma bora.

Tuzo hiyo ilizingatia nyanja zote za utoaji wa bidhaa na huduma za benki ambazo zinazojumuisha utoaji wa huduma kwa wateja wa rejareja pamoja na utoaji wa huduma za kidijitali.

Katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Ruth Zaipuna pia alinyakua Tuzo ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu (CEO) Bora wa Tanzania 2023 kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kuibuka mshindi wa tuzo hiyo ya kifahari wakati wa mkutano wa mwaka jana.

Tuzo za Africa Bank 4.0 hutambua juhudi na uvumbuzi wa wadau vinara barani Afrika katika sekta za kibenki, huduma za kifedha pamoja na sekta ya bima.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo kwa niaba ya benki hiyo, Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay alisema Tuzo hiyo ya Benki Bora Tanzania 2023 ni ushahidi tosha wa dhamira ya benki hiyo katika kuendeleza ubunifu na kukidhi mahitaji ya wateja wake huku akihidhinisha kuwa inaendana na utamaduni wa ubora wa benki hiyo unaolenga kutoa huduma za kibunifu na kipekee kwa wateja wake sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa.

“Nina furaha kubwa kupokea tuzo hii kwa niaba ya benki. Kushinda tuzo hii inathibitisha kwamba tumeanza kufikia ndoto yetu ya kutoa huduma zenye viwango vya juu ambazo tumekuwa tukizitoa kwa maika nyingi . Natoa tuzo hii kwa wafanyakazi wenzangu wa benki ya NMB kwa jitihada zao na kujitolea kwao kwani jitihada zao zimeleta heshima hii kwa benki yetu. Tunaelewa umuhimu wa kutoa huduma za kipekee kwa wateja wetu hivyo tumekuwa tukibuni huduma mpya kila mara ilikuboresha na kuridhisha wateja wetu,” Akonaay alisema.

Akoonay alisema benki hiyo kwa miaka mingi imefanikiwa kuwa mstari wa mbele wa kutoa huduma bora kwa wateja wake, huku ikianzisha dhana za kibunifu ambazo pia zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji kazi wake.

“Kama kinara katika sekta ya kibenki hapa nchini Tanzania, tunajivunia kuwapa wateja wetu huduma za kibenki ambazo zinaendana na viwango vya kimataifa. Benki yetu ya NMB inaendelea kutengeneza fursa za kifedha kwa kila mtu na hu ndio msingi wa dhamira yetu. Tutaendela kuongeza nguvu zaidi ya watu wetu na rasilimali zetu ili kufanya kazi na kuongeza ushirikishwaji wa kifedha, "aliongeza.

Tuzo hizo mbili zimepatikana miezi michache baada ya benki hiyo kutangaza faida ya kihistoria baada ya makato kodi iliongezeka kwa asilimia 47 hadi shilingi bilioni 429 ukilinganishwa na bilioni 290 iliyopatikana mwaka 2021 na kuifanya banki ya NMB kushika nafasi ya 3 bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa faida.

Wakati huo huo, mali za benki hiyo zilifikia kilele cha zaidi ya shilingi 10 kutoka trilioni 5.5 miaka minne iliyopita huko msingi wa amana ukipanuka hadi trilioni 7.5 kutoka trilioni 4.2 trilioni katika miaka mitatu tu.

Matokeo mazuri ya kifedha ya mwaka 2022 yanaonyesha kasi kubwa ya utendaji kazi ambayo NMB imekuwa nayo katika miaka minne iliyopita na ubora katika utoaji wake wa huduma za Kibenki.

Akizungumzia tuzo ya Mkurugenzi Mtendaji Bora, katika taarifa fupi iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna jijini Dar es Salaam alisema, “Kwa unyenyekevu mkubwa, nakushukuru sana kuwa mpokeaji wa Tuzo ya Mkurugenzi Mtendaji Bora wa mwaka 2023 nchini Tanzania ambayo inatambua mafanikio na mchango wangu kama kiongozi. Najivunia kuendelea kuongoza taasisi yenye sifa kubwa ambayo inaendelea kujiweka katika nafasi kuendelea kuweka na alama ya kimataifa kwa ubora,”

Zaipuna alitoa tuzo hiyo kwa wafanyakazi wenzake wa Benki ya NMB, menejimenti, bodi ya wakurugenzi, wateja na wadau waoshirikiana na benki yake.

“Natumia muda huu kuwashukuru wadau wetu wote kwa kuendelea kushirikiana nasi na juhudi zao zimetuwezesha kuendelea kuhudumia jamii,” aliongeza.Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay (kushoto), akimpongezwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya BII World, Fahd Ali Akmal (kulia) baada ya NMB kushinda tuzo ya Benki Bora Tanzania 2023 pamoja na tuzo ya CEO Bora Tanzania iliyokwenda kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna.Hafla hiyo ilifanyika hoteli ya Radisson Blue iliyopo jijini Nairobi, Kenya mwishoni wa wiki iliyopita.Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay (kulia), akipokea tuzo ya CEO Bora Tanzania 2023 kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mauzo Kampuni ya Tribe, Katrina Harding kwa niaba Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna. NMB pia imeibuka mshindi wa Tuzo ya Benki Bora Tanzania 2023. Hafla hiyo ilifanyika hoteli ya Radisson Blue iliyopo jijini Nairobi, Kenya mwishoni wa wiki iliyopita. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Fintech Tribe Mo Harvey.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad