Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mbaraka Semwanza kwa Niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, amepokea ugeni kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam. Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo Dodoma leo tarehe 23 Februari, 2023.
Baada ya kupokelewa kwa Ugeni huo, Kamishna Semwanza aliwasilisha mada mbalimbali zilizohusu Historia ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Majukumu, Mafanikio, Changamoto pamoja na Jitihada za kutatua changamoto. Aidha kwa pamoja Maafisa wa Jeshi hilo pamoja na wanachuo hao walijadiliana mada hizo na masuala mengine mbalimbali ya Zimamoto na Uokoaji.
Kamishna Semwanza ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuliwezesha Jeshi hilo kadiri fursa zinapopatikana, “kupitia Serikali ya awamu hii tumeweza kupeleka maafisa kujifunza katika chuo hiki”, alisema Kamishna Semwanza.
Kwa upande wake Brigedia Jenerali Stephen Mnkande, Mkufunzi Mwandamizi wa Jeshi la Wananchi kamandi ya Nchi kavu kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi amesema, lengo la ujio wao ni kujionea namna Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linavyotekeleza Majukumu yake.
Brigedia Jenerali Mnkande akiambatana na Uongozi wa Chuo, Wakufunzi na Maafisa Wanafunzi kutoka Mataifa mbalimbali wakiwemo wenyeji Tanzania, amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa utendaji kazi mzuri licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.
Akitoa salamu za shukrani Kanali Omari Nammenge kwa niaba ya Uongozi wa Chuo, ameshukuru kwa Mapokezi mazuri na Uwasilishwaji wa Mada mbalimbali ambazo zimewajengea uelewa kuhusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mbaraka Semwanza, akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) wakati wa ziara ya kimafunzo ya wanafunzi wa chuo hicho Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jijini Dodoma Februari 23, 2023. (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)
Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mbaraka Semwanza (kushoto), akimkabidhi zawadi ya kizima moto cha awali (Fire Extinguisher) Meja Jenerali Wilbert Ibuge (kulia), wakati Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) ulipofanya ziara ya kimafunzo Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jijini Dodoma Februari 23, 2023. (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)
Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mbaraka Semwanza, akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) na Wanafunzi wa chuo hicho, wakati wa ziara ya kimafunzo ya Wanafunzi wa Chuo hicho Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jijini Dodoma Februari 23, 2023. (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)
No comments:
Post a Comment