takwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 18, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha waandishi wa habari.
Baadhi ya waataalamu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 18, 2023.
Mtaalamu wa Utafiti, Sera na Mipango kutoka Benki Kuu ya Tanzania(BOT), Suleiman Misango akitoa mada kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 18, 2023.
Baadhi ya waandishi wa habari wakichangia mada wakati wa Kikao kazi cha waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika Kikao Kazi jijini Dar es Salaam leo.
MFUMUKO wa bei za bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi hapa nchini ndani ya kipindi cha robo mwaka ya kwanza ya 2023 bado stahimilivu na hali hii inaakisi hali halisi kwa kuwa kufikia Machi mwaka 2023 baadhi ya maeneo nchini yatakuwa yameanza mavuno ya mazao ya chakula na hivyo kupunguza shinikizo la bei lililopo sokoni kwa baadhi ya bidhaa za chakula.
Hayo ameyasema Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa wakati akifungua kikao kazi cha Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 18, 2023. Amesema kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa umeendelea kubaki katika kiwango cha tarakimu moja (single digit inflation) ambapo hadi mwezi Desemba mwaka 2022, Mfumuko wa Bei wa Taifa ulikuwa asilimia 4.8 na wastani wa Mfumuko wa Bei kwa mwaka 2022 ulikuwa asilimia 4.3.
Amesema Malengo ya ndani ya nchi kiwango cha mfumuko wa bei kitakwenda sambamba na makadirio ya ukuaji wa uchumi. Ambapo uchumi unakuwa kwa asilimia 5.0 kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, asilimia 8.0 na nchi za SADC ni kati ya asilimia 3.0 hadi 7.0. licha ya kuwepo kwa mitikisiko ya kiuchumi iliyotokea Duniani hasa athari za UVIKO-19 na mgogoro wa Urusi na Ukrain kwenye mwenendo wa bei nchini, bado Tanzania inafanya vizuri kwa upande wa uthibiti wa bei za bidhaa na huduma za jamii.
Amesema kuwa mwenendo wa Mfumuko wa bei Nchini hutegemea mabadiliko ya bei za Bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi. Hivyo, badiliko dogo katika bei za bidhaa za vyakula linakuwa na athari kubwa zaidi kwenye mwenendo mzima wa Mfumuko wa Bei wa Taifa.
Kwa mantiki hiyo, Serikali imejipanga kuendelea kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kuleta tija katika uzalishaji, kuongeza kipato cha Mwananchi kwa kuwa Sekta ya Kilimo inaajiri takriban asilimia 65 ya Nguvukazi ya Taifa na hivyo kuleta unafuu wa bei kwa mlaji wa mwisho sokoni. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeongeza bajeti ya kilimo zaidi ya mara tatu katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2022/23.
Aidha, Dkt. Chuwa amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuweka mikakati itakayosaidia kupunguza mgandamizo wa kuongezeka kwa bei nchini ikiwa ni pamoja na Kuendelea kudhibiti upandaji wa bei za bidhaa za nishati kama umeme na mafuta ya diesel na petroli ili kupunguza gharama za uzalishaji pamoja na usafirishaji.
Amesema kuwa Serikali inaendeleza juhudi zitakazosaidia kuongeza uzalishaji wa bidhaa za nafaka, hasa mchele, mahindi na ngano kwa kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya mbegu bora na utoaji wa ruzuku kwa pembejeo za kilimo pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ili kuvutia sekta binafsi kwenye kilimo.
Dkt. Chuwa amesema serikali itauongeza uwezo na kuimarisha vituo vya Wakala wa Uhifadhi wa Chakula Tanzania ili kuwapunguzia wananchi makali ya maisha wakati wa uhaba wa bidhaa za vyakula katika baadhi ya maeneo nchini pamoja na Kuongeza idadi ya Maofisa Ugani katika sekta ya kilimo na kuendelea kuwawezesha vitendea kazi ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia ili kuwawezesha Wananchi wengi zaidi kupata huduma ya ushauri wa mbinu bora za kilimo.
Dkt. Chuwa amesema kuwa Maoteo yanaonesha kuwa, Mfumuko wa Bei wa Bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi utaendelea kupungua kutoka asilimia 9.7 mwezi Desemba, 2022 hadi asilimia 8.4 mwezi Machi, 2023.
Akifafanua kuhusiana na upandaji wa Bei amesema kuwa kunaupandaji bei Mzuri na mbaya, akizungumzia Upandaji Mzuri amesema kuwa kunamanufaa kwa uwekezaji na upandaji bei Mbaya ni ufungaji wa Shughuli za Uchumi.
Pia ametoa rai kwa wananchi kutumia neema ya mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini kulima mazao kwa wingi ili kufanya nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na kuwa na akiba ya chakula ya kutosha kwani suala hilo litakuwa na matokeo chanya kwenye mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula.
No comments:
Post a Comment