HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, January 29, 2023

Johari Rotana yapanda hadhi ya nyota tano nchini


Hoteli ya Johari Rotana Tanzania imepanda hadhi na sasa kuwa hoteli nyota tano baada ya kukidhi vigezo vinavyohitajika kimataifa.

Rotana ni hoteli ya kisasa yenye kukidhi mahitaji yote ya wasafiri wanaoingia jijini Dar es Salaam kwa sababu ina vyumba vya hadhi ya nyota tano na vile vya kawaida takriban 193, nyumba za makazi zilizofanyiwa ukarabati na zenye samani maridadi 60, teknolojia za kisasa zilizomo ndani ya vyumba na burudani kadha wa kadha, na nafasi kubwa kwa ajili ya mapumziko au kufanyia kazi nyakati za mchana.

Iwe unasafiri haraka kwenda Dar es Salaam au unapanga kukaa zaidi jijini, Johari Rotana inatoa huduma ya vyumba vya aina kadhaa ili kukidhi mahitaji yako.
Miundombinu ya aina yake ya hoteli hiyo iliyopo karibu na fukwe za jiji hilo la kibiashara lenye shughuli nyingi zaidi nchini tayari ilikuwa ni hadhi ya nyota tano, ispokuwa huduma, ambazo ndiyo msingi wa hata upangaji wa madaraja na hadhi ya hoteli zote duniani.

Meneja Mkuu wa Johari Rotana, Joerg Potreck anakiri kwamba hadhi hiyo waliyoipata hivi karibuni inatokana na uwekezaji wao katika miundombinu ya kisasa iliyomo katika hoteli hiyo na timu ya watu sahihi.
“Hapa Rotana, tunaendesha mafunzo kwa timu ili kutimiza matarajio ya wateja na wanachangia kutengeneza mazingira yanayovutia hotelini. Ikiwa huduma ni mbaya sana, ni rahisi mtu kusema kwamba ni hoteli nzuri lakini ……na ndiyo maana tunafanya kazi kwa bidii ili kuweka kila kitu sawa,” asema Potreck.

Akizungumza kwa bashasha, Potreck anasema hoteli hiyo imekuwa kinara katika kutoa huduma bora kwa miezi minne mfululizo katika Jiji la Dar es Salaam ambaye anaeleza mafanikio hayo yametokana na kuwa na timu bora, bidii na kujituma.
“Uongozi wa Rotana unaamini kuwa ukiwa na timu yenye furaha, utakuwa na huduma nzuri na tunafanya mengi kwa timu zetu na haya yote yanawiana kikamilifu na vigezo vya hoteli ya nyota tano,” anaongeza Potreck ambaye anasisitiza kuwa huduma bora zina maana kubwa kuliko majengo tu.
 
Kuendana na kasi ya matarajio ya wateja
Kwa kuwa matarajio na mitazamo ya wateja inabadilika kwa haraka na kila wakati, Rotana itahakikisha inakwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ili kuendana na mahitaji yao tu, anaeleza Potreck.

Anasisitiza kuwa uongozi utakuwa tayari kukaa chini na kuumiza vichwa kwa ajili ya kuja na njia mpya za kuwaridhisha wateja wao wakubwa.
Meneja huyo anasema kuwa hoteli hiyo kwa bahati nzuri ina mtindo wake mahususi wa uboereshaji huduma na mifumo ya ufanyaji kazi inayoisaidia kupiga hatua kila iitwayo leo.
 
Mtindo huu ni muhimu kwa ajili ya kubadilisha uzoefu wa huduma kwa wateja na utawapa hamasa wamiliki wengine wa hoteli kufikiria namna ya kuboresha huduma zao huku wateja wakibaki na machaguo ya kutosha.

"Ulimwenguni kote, watu wanapenda kulinganisha bidhaa au huduma, kwa hivyo kama mshindani, lazima ujiweke tofauti kwa kutanua wigo. Angalia Nairobi, Nairobi ina hoteli nyingi za nyota tano ukilinganisha na Dar es Salaam na zote zinashindana ili kuwa bora zaidi.”

Anasema kuwa uwepo wa hoteli hiyo hapa jijini ambayo ni ya pili kwa hadhi ya nyota tano, imesaidia hoteli nyingine kuboresha huduma zao.
Kwa nini hoteli hiyo ipo Dar es Salaam pekee?
 
Potreck anasema kuwa Johari Rotana ni kampuni ya usimamizi ambayo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya hoteli duniani kote ambayo wateja wake lengwa ni wafanyabiashara na watu mashuhuri, kwa hivyo, bila shaka ungetarajia biashara ya aina hiyo kuwa katikati ya kitovu cha nchi husika.

Achilia mbali suala la mkakati wa kibiashara, hoteli hiyo inaangalia uwezekano wa kuingia makubaliano na mwekezaji yeyote anayekusudia kufungua hoteli katika makao makuu ya nchi, Dodoma ambapo hoteli hiyo itafanya kazi ya usimamizi kwa niaba yao kupitia chapa ya Johari Rotana.
“Inaweza kutokea tukakutana na mwekezaji ambaye ana mpango wa kufungua au kujenga hoteli mpya na pia anavutiwa na migahawa yetu, hivyo tunaweza kuendesha biashara nzima kwa niaba ya mmiliki ili kusimamia viwango vinavyohitajika katika biashara hiyo,” anaongeza Meneja.
Siri nyuma ya hadhi ya nyota tano
 
Kuna vigezo kadhaa vya kuzingatiwa kabla ya hoteli kupewa hadhi ya nyota tano na hii ni pamoja na; Huduma za vyumba kwa saa 24, usalama wa saa 24, aina za migahawa, vyakula vya ndani na nje ya nchi, hadhi ya vyumba kuanzia ukubwa hadi huduma zilizomo, miundombinu kwa ajili ya watu wenye ulemavu, bima, uwezo wa kudhibiti majanga ya moto na mengineyo, masuala ya usalama na afya mahala pa kazi na ajira zenye staha kwa wazawa.

"Sifa hizi zote tunazifahamu na ni rahisi sana kupata hadhi ya nyota tano kwenye makaratasi lakini kukidhi matarajio na mahitaji ya wateja ni jambo lingine. Na hapo ndipo suala la usimamizi linapokuja, na hapa Rotana tumekuwa tukitoa ujuzi mwepesi kwa wafanyakazi wetu kuboresha huduma.”
“Biashara ya hoteli ni mchezo wa kuridhisha wateja na najua ni kazi ngumu, nina zaidi ya miaka 40 katika biashara ya hoteli na uzoefu mwingi wa kimataifa. Nimekuwa katika nchi nyingi,” anaeleza Potreck ambaye anakiri kwamba uongozi wa hoteli hiyo umechagua wazawa na raia wa kigeni ili kuleta utofauti unaohitajika.
Anaongeza kuwa bila ya kuunganisha idara, timu, kujitoa, bidi na uvumbuzi bado ni ngumu kuendesha biashara ya hoteli. Na hili anadhani ndiyo moja ya changamoto zinazowakabili Watanzania wengi.

"Biashara ya hoteli ni biashara ngumu kwa sababu unahitaji kupambana ili mteja akuchague, hivyo, ukiamua kutokuchukua hatua yoyote, hauwezi kufanikiwa," anadokeza.

Kwa upande wake, Meneja Chapa wa Johari Rotana Tanzania, Edward anasema wanafuraha kubwa kufikia kilele cha mafanikio ya kazi yao.

"Hadhi yetu ya nyota tano haifahamiki tu na Wizara yetu ya Maliasili na Utalii bali inavuka mpaka hadi ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa imekidhi viwango vinavyohitajika katika sekta ya hoteli vya kikanda," anafafanua Edward.
 Edward anasema kwamba hadhi ya nyota tano ni mafanikio makubwa waliyoyapata na sasa wana kazi kubwa kuhakikisha wanailinda heshima hiyo kwa kuja na huduma zilizoboreshwa maradufu.

Kuhusu Rotana
Rotana Hotel Management Corporation (Rotana) ilianzishwa mwaka 1992, kwa ushirikiano kati ya wanafalsafa wawili wenye maono, Nasser Al Nowais na Selim El Zyr.

Ikifanya kazi kama Rotana, ilifungua biashara yake ya kwanza ya Beach Rotana Abu Dhabi mwaka 1993 na leo ni moja ya kampuni zinazoongoza za usimamizi wa hoteli ndani ya Mashariki ya Kati, Afrika, Ulaya Mashariki na Türkiye.

Rotana inachanganya uelewa wa kipekee wa utamaduni na jamii za Mashariki ya Kati na utaalamu wa pamoja wa timu ya watendaji inayochangia uzoefu wa miaka mingi wa kimataifa katika sekta ya huduma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad