HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 22, 2022

NDUHIYE AIPONGEZA SERIKALI KWA KUTEKELEZA MPANGO WA MAFUNZO YA WATUMISHI WA VIVUKO TEMESA

 



NA. Alfred Mgweno (TEMESA Dar es Salaam)

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Bwana Ludovick Nduhiye ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ulio chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha katika bajeti yake kwa ajili ya kuwapatia mafunzo muhimu Watumishi wa Vivuko kote nchini.

Nduhiye ametoa pongezi hizo mapema leo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mafunzo kwa watumishi 43 wa vivuko vinavyosimamiwa na TEMESA iliyofanyika katika Chuo cha Bahari nchini (DMI) kilichopo Posta jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa Serikali imetoa Fedha kwa ajili ya kuwapa mafunzo hayo kwakuwa inaamini katika kuwajengea uwezo watumishi wake na kuhakikishia usalama katika uendeshaji wa vivuko

Nduhiye amewataka watumishi hao wa vivuko kutambua kuwa wanalo jukumu la kujifunza kwa bidii ili kuongeza kiwango cha uelewa wao na kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi.

‘’Wote tunatambua malalamiko yanayotokana na ubovu wa vivuko mnavyovihudumia kutokana na kutokuwa na mipango mizuri ya Matengenezo Kinga na yale Matengenezo Rekebishi. Aidha, kuna malalamiko pia kuwa vivuko vyetu vinaendeshwa na manahodha wasio na sifa na hivyo kuathiri utunzaji bora wa vivuko vyetu, kwa ujumla ni matarajio yetu kuwa baada ya mafunzo haya tutaona maboresho makubwa katika uendeshaji wa vivuko vyetu nchini, hivyo ninawataka kuwa makini katika kupokea mafunzo mtakayopata na kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo na hivyo kuboresha huduma za vivuko nchini.’’ Alisema Nduhiye.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala huo Mhandisi Deogratius Nyanda, akizungumza katika hafla hiyo, amesema TEMESA imepewa jukumu na dhamana ya kutunza miundombinu ya usafiri ambayo inabeba uhai wa watu na hivyo kwa kuliona hilo, TEMESA imeonelea umuhimu wa kuweka juhudi katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa vivuko kote nchini ili kulinda usalama wa raia na mali zao.

Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA Lazaro N. Kilahala akizungumza wakati wa hafla hiyo, amesema TEMESA ina jumla ya vituo 22 vyenye jumla ya vivuko 33 kote nchini na kila kivuko kinapaswa kuwa na manahodha, mabaharia, wahandisi pamoja na mafundi wenye sifa zinazoendana na sheria zinazoongoza vyombo vya majini kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa mafunzo kwa mabaharia ya mwaka 1978 na hivyo katika kutekelea azima hiyo njema ya serikali, Wakala umewapa nafasi watumishi wake 43 kutoka kwenye vituo vya vivuko nchini kupata mafunzo ya taaluma hii ya vyombo vya majini.

‘’Vituo vilivyohusika kwenye Kanda ya Mashariki na Kusini ni Magogoni/Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam, Pangani/Pweni Mkoa wa Tanga, Mafia/Nyamisati Mkoa wa Pwani, Lindi/Kitunda Mkoa wa Lindi na Msangamkuu/Msemo Mkoa wa Mtwara, Kanda ya Ziwa tumetoa vituo vya Kigongo/Busisi, Nyakalilo/Kome, Kisorya/Rugezi, Bugolola/Ukara, Kayeze/Bezi, Luchelele/Ilunda vyote Mkoa wa Mwanza, aidha, watumishi wengine wa Kanda ya Ziwa ni kutoka vituo vya Kahunda/Maisome na Chato/Muharamba Mkoa wa Geita, Musoma/Kinesi na Iramba/Majita Mkoa wa Mara pamoja na Rusumo/Nyakiziba na Kasharu/Muganguzi Mkoa wa Kagera.’’ Alisema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa mafunzo hayo yamegawanyika katika makundi matano ambayo ni Mafunzo ya awali ya lazima (Mandatory Course) yatakayojumuisha watumishi 9, mafunzo ya wasaidizi wa Manahodha (Rating Navigation Deck) yatakayojumuisha watumishi 6 mafunzo ya wasaidizi wa wahandisi (Rating Engine Course) yatakayojumuisha mtumishi 1, Mafunzo ya Manahodha daraja la IV (COC Class IV Deck) yatakayojumuisha watumishi 10 pamoja na Uhuishaji vyeti (Revalidation Courses) ambayo yatajumuisha watumishi 17.

Mtendaji Mkuu ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuiwezesha TEMESA kutekeleza mafunzo haya muhimu na kuahidi kuwa Wakala utaendelea kutoa mafunzo hayo muhimu kadri ya mahitaji ili kuhakikisha vivuko vinahudumiwa na watumishi wenye sifa stahiki.

Wakati huo huo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo ameushukuru Wakala kwa kuendelea kuwa na ushirikiano wa karibu na Chuo hicho hasa upande wa mafunzo ya masuala ya usafirishaji wa majini na utoaji wa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya utaalamu wa ujenzi wa meli na vivuko.
Naibu Katibu Mkuu Ujenzi Mhe. Ludovick Nduhiye (wa pili kulia, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TEMESA Mhandisi Deogratius Nyanda kulia, Mtendaji mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Vivuko TEMESA Mhandisi Sylvester Simfukwe wakipata maelekezo ya vifaa maalumu vya kufundishia mafunzo kwa vitendo katika Chuo cha Bahari Nchini (DMI) ambapo watumishi 43 wa vivuko TEMESA watakuwa wakipatiwa mafunzo chuoni hapo.
Naibu Katibu Mkuu Ujenzi Mhe. Ludovick Nduhiye katikati akiwa Pamoja na baadhi ya mabaharia, manahodha Pamoja na watumishi wa vivuko ambao wanapatiwa mafunzo maalumu katika Chuo cha Bahari (DMI) kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi na utaalamu katika uongozaji wa vivuko.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad