HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 22, 2022

ARDHI SACCOS KUNUFAISHA WATUMISHI WA SERIKALI


Na. Hassan Mabuye, Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amekitaka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi kijulikanacho kama Ardhi SACCOS kuanzisha miradi itakayowanufaisha watumishi wa Umma hata baada ya kustaafu kwao.

Dkt. Kijazi Ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa pili wa Ardhi SACCOS uliyofanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Taifa tawi la mkoa wa Dodoma.

“Anzisheni miradi ya kiubunifu itakayosimamiwa na Ardhi SACCOS ambayo itawanufaisha watumishi wa Sekta ya Ardhi kwa kuwajengea uwezo wanachama wenu kumiliki viwanja na hata kuanzisha makampuni yatakayo wasaidia pindi wakatapo staafu kazi” Amesema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi amesisitiza kuwa angependa kuona SACCOS hii inawanufaisha watumishi kwa kuwa na mikakati ya muda mrefu ya miaka 5 hadi 15 ili kuwaepusha kujiingiza kwenye shughuli zisizo za kimaadili wawapo kazini na hata baada kustaafu.

Aidha, Dkt. Kijazi amewataka viongozi wa Ardhi SACCOS kukamilisha kwa haraka mradi wa Viwanja wa Mapinduzi A uliyopo jijini Dodoma kwani umechukua muda mrefu kukamilika, hivyo wakae na kutafutia ufumbuzi kikwazo cha kuchelewa kwa mradi huo.

Kijazi ameitaka pia SACCOS hii kuwakutanisha kwa pamoja watumishi wa Sekta ya Ardhi katika fani zote za Upimaji na Ramani, Mipango Miji, Uthamini wa Mali na Fidia na fani nyingine zote za sekta ya ardhi ili waweze kunufaika kwa kujiwezesha kiuchumi.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Ardhi SACCOS anayemaliza muda wake Bw. Wilson Luge amesema kuwa amepokea kwa mikono miwili maelekezo, ushauri na maoni ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi na watashirikiana na Menejimenti ya SACCOS hiyo kuyatekeleza maelekezo hayo.

“mara baada ya mkutano huu kufungwa tutashirikiana na Viongozi ambao watachaguliwa hivi karibuni kusimamia na kutekeleza maelekezo na ushauri aliyoutoa Mgeni Rasmi leo kwa Ardhi SACCOS kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake”Amesema Luge.

Ardhi SACCOS ni Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi ambacho kilianzishwa rasmi mwaka 2020 na kina usajili wa utayari na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania na ina wanachama takribani 331 nchi nzima. 
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi akiongea katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi cha Ardhi SACCOS katika ukumbi wa Maktaba ya Taifa tawi la mkoa wa Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi (aliyesimama kulia) akiongea katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi cha Ardhi SACCOS katika ukumbi wa Maktaba ya Taifa tawi la mkoa wa Dodoma.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi cha Ardhi SACCOS wakiwa katika Mkutano Mkuu wa uliyofanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Taifa tawi la mkoa wa Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi (katikati) akiwa na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi cha Ardhi SACCOS katika ukumbi wa Maktaba ya Taifa tawi la mkoa wa Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi (katikati) akiwa na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi cha Ardhi SACCOS katika ukumbi wa Maktaba ya Taifa tawi la mkoa wa Dodoma.

(Picha zote na Hassan Mabuye)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad