HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 6, 2022

MATUKIO YA UKATILI YANAZIDI KUONGEZEKA, LHRC YATOA MAPENDEKEZO

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 6, 2022 wakati Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kikitoa tamko la kuungana na watanzania na jamii ya kimataifa katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambazo huadhimishwa kuanzia   Novemba, 25 hadi Disemba 10 kila mwaka.
Afisa Mwandamizi Jinsia, Wanawake na Watoto, Getrude Dyabele akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo Desemba 6, 2022. Kushoto ni kurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga.

VITENDO vya Ukatili wa Wanawake na Watoto umeonekana kuongezeka, Kwa Mwaka 2021, matukio 23,685 ya ukatili dhidi ya wanawake yameripotiwa kwa mwezi Januari hadi Disemba ikiwa ni ongezeko la matukio 2,859 kwa mwaka Mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 6, 2022 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga wakati LHRC kikitoa tamko la kuungana na watanzania na jamii ya kimataifa katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambazo huadhimishwa kuanzia Novemba, 25 hadi Disemba 10 kila mwaka. Amesema kuwa Mikoa inayoongoza kwa ukatili dhidi ya wanawake katika ripoti iliyotolewa na Haki za Binadamu ni pamoja na Arusha, Manyara, Lindi, Tanga na Mkoa wa Kipolisi wa Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa Ukatili wa kijinsia unaohusisha ukatili wa kimwili, ukatili wa kingono, ukatili wa kisaikolojia, ukatili wa kiuchumi pamoja na ukatili wa kidijitali ambao nao umekuwa ukiwatesa wanawake zaidi. Katika taarifa ya haki za Binadamu ukatili wa kimwili na ukatili wa kingono umeongoza zaidi ya ukatili mwingine.

Katika taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia inayohusu tathimini ya jinsia nchini Tanzania 40% ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 wamepitia ukatili wa kimwili wakati 17% wamepitia ukatili wa kingono. Taarifa hiyo imeenda mbele kusema kuwa 44% ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamepitia ukatili wa kimwili pamoja au ukatili wa kingono kutoka kwa mwenza wao. Ukatili wa wenza umekuwa mkubwa sana sehemu za vijijini kwa 53% kuliko mijini 45%. Asilimia 30% ya wasichana wanapitia ukatili wa kingono kabla ya kufika umri wa miaka 18 huku 58% ya wanawake na 40% ya wanaume wakiamini kuwa mume ana haki ya kumpiga mke wake kwa sababu zozote.

Akizungumzia Mauaji ya wanawake amesema Mauaji ya wanawake sio kitu kipya duniani na Tanzania kwa ujumla kwani vitendo hivi vimeendelea kuongezeka siku hadi siku.

Katika Taarifa ya Jeshi la polisi mwaka 2022 iliripoti matukio 472, 544 kwa mwaka 2018, 487 kwa mwaka 2019, 531 kwa mwaka 2020 na 554 kwa mwaka 2021 ya mauaji ya wanawake kutokana ukatili wa wenza, uchawi na imani za kishirikina, mauaji yasiyo ya wenza mashambulio ya wanawake.

Anna amesema mauaji yote yanayotendwa na mwenza wa mhanga awe mume, mchumba, mpenzi au mtu ambaye tayari kaachana na mhanga. Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani ulionesha kuwa 35% ya mauaji Katika kulinganisha tafiti amesema taarifa za Haki za Binadamu za mwaka 2019, 2020 na 2021 ziliripoti matukio zaidi ya 50 ya mauaji ya wenza ambapo wahanga wanawake ni zaidi ya 95% mauaji ya wanawake yanayoendelea kuogezeka kwa kasi nchini Tanzania. Mwaka huu kumekuwa na matukio mengi ya mauaji ya wenza ikiwemo lile la Mwanza ambapo mume alimpiga mkewe risasi na yeye kujiua.

Mauaji ya wanawake yanayohusina na ukatili wa kingono amesema kuwa Mauaji hayo husababishwa na ukatili wa kingono ambao hupeleka mauaji ya mwathirika vitendo vingi vya ukatili wa kingono humuathiri zaidi mwanamke.

Vitendo hivi vyaweza kutokana na ubakaji wa watu wengi au ubakaji wa aina nyingine yeyote. Wanawake ambao ndio wahanga wa ukatili wa kingono zaidi hupoteza maisha kutokana na vitendo hivyo. Mwaka huu tuliona huko Mbeya binti aliyeuawa na kijana wakati akijaribu kumbaka.

Akizungumzia sababu za Mauaji hayo Wakili Anna amesema kuwa mauaji ya makusudi ya wanawake ni pamoja na wivu hasa pale inapohusu mwenza au mtu uliyeachana nae, kulazimisha tendo la ngono, pombe na ulevi, matatizo ya akili, umasikini, ukosefu wa uwezeshaji uchumi kwa mwanamke kitu kinachowafanya wanawake waendelee kuvumilia ukatili, ukosefu wa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na sheria, imani za kishirikina, mila na desturi zilizopitwa na wakati pamoja na kutokuwa na usawa wa kijinsia.

Hata hivyo amesema Sheria kandamizi ya mirathi ya kimila, sheria ya ndoa na kutokuwepo kwa sheria maalumu ya ukatili wa kijinsia au ukatili wa majumbani kumeendelea kuleta changamoto katika kupambana na vita dhidi ya ukatili na mauaji ya makusudi ya wanawake.

Pia amesema kutokuwepo kwa uhuru wa kiuchumi kwa wanawake wameendelea kuwa duni kiuchumi na kusababisha kuendelea kuwa wahanga wa ukatili kwani hushindwa kujisimamia na kujiteteta maana huogopa sehemu ya kuanzia. Hali hii huwafanya waendelee kuwa katika nafasi duni na kuendelea kufanyiwa ukatili.

Mila na desturi zilizopitwa na wakati, Tanzania bado inashikilia mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo bado zinaendelea kumkandamiza mwanamke. Mila hizi ni pamoja na ukeketaji, ndoa za mapema, ukatili wa majumbani na uhuru wa kumiliki na kurithi mali.

Licha ya hayo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa mapendekezo kwa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu hali za wanawake, watoto, wasichana na haki za binadamu kwa ujumla ili kuleta mabadiliko ya tabia. Pia Kuboresha huduma za jamii, haki na kuhakikisha wanawake wanapata msaada pale wanapofanyiwa ukatili ikiwemo kuwa na nyumba salama na huduma za kisaikolojia.

Aidha zitungwe sheria na Sera mahususi ya kupinga ukatili wa kijinsia au ukatili wa majumbani kwa ajili ya kuhakikisha usalama zaidi wa wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani.

Kurekebisha sheria zote kandamizi kwa wanawake ambazo zinaendelea kuleta changamoto katika ufikiwaji wa usawa wa kijinsia na ufurahiaji wa haki za wanawake. Hii ni pamoja na sheria ya ndoa na mirathi.

Akizungumzia mapendekezo ya sheria ya watoto wanaopata ujauzito kurudi shule amesema ili kukata gurudumu la umasikini litakaloendelea kuwaweka katika hatari ya kufanyiwa ukatili inatakiwa kurekebisha sheria zote zinazomnyima mtoto wa kike haki za kufurahia haki yake ya elimu ikiwemo sheria ya ndoa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad