HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 3, 2022

DIT YASAINI MAKUBALIANO YA KUENDESHA MAFUNZA YA PAMOJA NA TAASISI YA CQVIE YA CHINA





TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), imesaini makubalino ya kuendesha mafunzo ya pamoja na Taasisi ya Chongqing Vocation Institute of Engineering (CQVIE) ya China ambapo wanafunzi wa kitanzania watanufaika kwa kupata shahada na stashahada katika taasisi hiyo.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh.Profesa Adolf Mkenda amesema wanafunzi wa kitanzania watapata shahada ya Uhandisi Ujenzi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na stashahada ya Ujenzi kutoka Taasisi ya Chongqing Vocational Institute of Engineering (CQVIE) ya China.

Profesa Mkenda amesema programu hiyo inaanza mwaka huu ambayo itafanya mambo makubwa matatu ikiwemo kubadilishana wanafunzi, kubadilishana walimu pamoja na kuwaunganisha wanafunzi na viwanda kwa lengo la kujifunza zaidi.

Amesema DIT itasajili wanafunzi ambao watasoma katika taasisi hiyo kwa mwaka wa kwanza, mwaka wa pili na wa tatu watasoma mafunzo ya ufundi stadi katika chuo cha CQVIE China ambapo watatunikiwa stashahada ya Ujenzi na mwaka wa nne watarudi DIT ambapo watatunikiwa shahada ya Uhandisi Ujenzi.

Pia amesema kutakuwa na kipengele cha kubadilishana wakufunzi wa China na Watanzania ambao wataenda China kuangalia namna ambavyo wenzeo wanavyofundisha wanafunzi wao kubadilishana mawazo lakini pia DIT itapata wakufunzi toka China ambao watakuja kufundisha madarasani kwa pamoja kwa lengo la kuboresha.

Prof. Mkenda amesema programu hiyo itasaidia kuunganisha vizuri zaidi wanafunzi wanaoenda kusoma na maeneo ya kazi, akatolea mfano Kampuni kubwa ya nchini China inayofanya kazi za Ujenzi hapa nchini ijulikanayo kama Group 6 ambayo itashirikiana na DIT hasa kwa wanafunzi wanaotarajiwa kwenda kusoma masomo ya Uhandisi Ujenzi kupata fursa ya kwenda kujifunza kwa vitendo lakini kupata ajira watakapo hitimu.

Kwa maelezo ya Prof. Mkenda, programu hiyo itaanza na wanafunzi takriban 30 lakini jitihada zitaendelea kufanyika kuhakikisha kuwa idadi ya wanafunzi inaongezeka kwa kasi ili kuweza kupeleka wanafunzi wengi zaidi China.

Alisema juhudi hizo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kila mara anasisitiza elimu iandae wanafunzi ambao wataweza kujiajiri kirahisi hivyo aina hiyo ya mafunzo itaongeza uwezekano wa wanafunzi wanaomaliza kupata ajira ya moja kwa moja ndani na nje ya Tanzania .

Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la DIT, Dk Richard Masika alishukuru kwa makubaliano hayo baina Taasisi hizo na kuahidi watasimamia programu hiyo kwa ufanisi mkubwa ili kuhakikisha inakuwa endelevu ili kufungua milango mingine ya ushirikiano zaidi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad